Halmashauri ya Walei Sumbawanga waaswa kushirikiana
WAAMINI wa Jimbo Katoliki Sumbawanga wamefanya
ufunguzi wa Jubilei ya miaka 50 ya kituo cha Halmashauri ya Walei na vyama vya
kitume jimboni humo.
Akiongoza mamia ya waamini katika uzinduzi wa
jubilei ya kituo cha walei jimboni Sumbawanga iliyofanyika hivi karibuni
sambamba na sikukuu ya mashahidi wa Uganda katika Kanisa la Katandala lililo katika
jengo hilo la walei, Askofu wa Jimbo Katoliki Sumbawanga Mhashamu Damiani Kyaruzi amesema kuwa kituo cha walei jimboni humo ni cha kwanza
katika majimbo yote tangu kupandwa kwa mbegu ya imani nchini Tanzania.
Askofu Kyaruzi
amesema kuwa Kanisa lilikabidhiwa mikononi mwa walei toka Mtaguso wa
pili wa Vatikani juu ya hati ya harakati za kitume, majukumu na wajibu wa walei
ambapo kwa misingi hiyo walei ni mitume na wamisionari, kwa maana hiyo Kanisa
ni la walei huku makreli na watawa
wakiwa ni wahudumu tu ndani ya Kanisa.
Aidha Askofu Kyaruzi amekemea tabia ya viongozi
mbalimbali pamoja na walei katika Kanisa wanaopinga na kukwamisha juhudi za
maendeleo zinazofanywa na vyama vya kitume katika kwa sababu mbalimbali ambapo
ametoa kauli mbiu ya jubilee ya walei inayosema “Ni wajibu wetu kufundishana imani, kufundishana imani ni wajibu wetu”.
“Kwa namna zozote zile asiwepo padri yeyote, mtawa
wala mlei mwenyewe anayeweza kuzuia na kuzima maendeleo na shuguli za walei
katika Kanisa,” Amesema Askofu Kyaruzi.
Akieleza historia ya kuanzishwa kwa huduma za walei
jimboni Sumbawanga Mkurugenzi wa walei jimboni Padri Didas Nandi amesema kuwa kituo
hicho kilianza mwaka 1967 na Mkurugenzi wa kwanza wa utume wa walei na vyama
vya kitume padri Gerald Nolf kwa idhini ya Askofu wa kwanza mzalendo hayati Mhashamu
Kalolo Msakila.
“Kituo kimekuwa kikitoa huduma mbalimbali za kiroho na kimwili kwa
walei kama vile ibada na misa, semina, mikutano, makongamano na sherehe
mbalimbali za ndoa, kipaimara pamoja na huduma za malazi kwa walei wanaotoka
maeneo mbalimbali ya Jimbo na nje.” Amesema padri Nandi.
Wakieleza changamoto mbalimbali zinazokwamisha
kusonga mbele ya shughuli mbalimbali za kimaendeleo za walei, Mwenyekiti wa
jubilei hiyo Joachim Luis amesema kuwa ushirikiano duni wa maparoko, viongozi
wa parokia na jumuiya ni moja ya sababu zinazozorotesha na kukwamisha mipango
ya walei katika Jimbo.
Kamati mbalimbali zimeanzishwa jimboni humo kusaidia
kufufua imani kwa waamini, kuimarisha utume wa walei jimboni, ili kusimamia
maendeleo ya walei ndani ya Jimbo ikiwa ni pamoja na ujenzi wa jengo jipya la
walei litakalokuwa na ghorofa 3 huku likikadiriwa kugharimu kiasi cha shilingi
bilioni nne (4), ambapo tayari ujenzi huo umekwisha kuanza.
Comments
Post a Comment