"TUWE MAKINI NA MATUMIZI YA SIMU" WAAMINI WAASWA


Waamini wametakiwa kutambua madhara yatokanayo na matumizi mabaya ya simu za mkononi hali inayodhorotesha uchaji kwa waamini wanapokuwa katika nyumba za ibada hasa kushindwa kupokea mafundisho ya kiroho kwa ufasaha kwa sababu ya kuitii simu kuliko neno la Mungu. 

Wito huo umetolewa na Padri George Mwaluko wa shirika la Damu Azizi ya Yesu wakati akiongoza ibada ya misa takatifu katika Kanisa la Mtakatifu Fransisco wa Sale parokia ya Dumila jimboni Morogoro akiwaasa waamini na wote wenye mapenzi mema kutafakari upya matumizi ya simu za mkononi.

Aidha Padri Mwaluko amesema kuwa katika ulimwengu wa maendeleo ya sayansi na teknolojia asilimia kubwa ya watu wanatuma simu za mikononi ambazo zinasaidia katika mawasiliano japo wakati mwingine huleta changamoto kwa watumiaji.

Sambamba na hayo padri Mwaluko amewakumbusha waamini kuwa waangalifu na matumizi ya simu za mkononi hivyo ni wajibu wao kutenga muda maalumu kusoma maandiko matakatifu badala ya kutumia muda mwingi katika simu.

“Tunavyoitii simu tuwe waangalifu kutafakari kilichopo nyuma ya simu, katika matumizi yake ila niwakikishie kwamba kama chombo cha mawasliano simu ni chombo kizuri ila tuchunguze hatari ya hizi nguvu mbili tuzingalie zimeleta nini katika maisha yetu, tusipokuwa makini tunapoteza uchaji kwa sababu hata katika makanisa hakuna haja ya kuandikiwa matangazo katika nyumba zetu, mfano zima simu yako fungua moyo wako,” amesema padri Mwaluko.
 
Hata hivyo padri Mwaluko amesema kuwa simu za mikononi zitaendelea kuwa dira na miongozo wa maisha endapo zitaendelea kutumika katika matumizi chanya yenye tija katika jamii na Kanisa kwa ujumla.

“Tukiangalia kwa haraka simu ndio inayotushauri na kutuongoza kwa siku kuelekeza nini cha kufanya, kwa hiyo ni vyema tukiingia kanisani tukumbushwe na mistari ya maandiko matakatifu maana muda mwingine tunajiaminisha kwamba Roho Mtakatifu hana nguvu kwetu lakini sio kweli."

Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

HISTORIA YA SHEREHE YA MOYO MTAKATIFU WA YESU