Shukuru usikufuru
INGAWA tuna mioyo midogo lakini inaweza kubeba jambo kubwa
nalo ni shukrani. “Tunapotoa kwa furaha na kupokea kwa shukrani, kila mtu
anabarikiwa,” alisema Maya Angelou. Kuna
methali isemayo, “Asiyeshukuru kwa jambo dago apewalo hatashukuru kwa jambo
kubwa.” Leo hii wakatoliki sehemu zote duniani wanaandamana kusherehekea sherehe
inayojulikana kama “Mwili na Damu ya Kristo.”
Kwa jina lingine sherehe hii
inajulikana kama “Sherehe ya Ekaristi Takatifu.” Neno “Ekaristi” linatokana na
neno la Kigiriki ambalo linamaanisha shukrani. Ni sherehe inayohusu kumshukuru
Mungu na utamaduni wa kushukuru. Kushukuru ni kitovu cha sherehe hii. Shukuru
kwa kila jambo. Sherehe ya Leo ya wakatoliki inahusu utamaduni wa kushukuru.
Waluhya wana methali isemayo, “Nyama choma haiwezi kuwa tamu ukamsahau
aliyeichoma.”
Methali hii inakazia kuwa na
utamaduni wa kushukuru. Kama umepewa siyo siri. Watu wanaona jinsi Mungu
alivyokubariki na hivyo kwa mantiki hii wakatoliki wanaandamana hadharani
kuonyesha shukrani yao.
Sherehe hii inapata nguvu kutoka
katika maneno ya Biblia, “Ndipo Wayahudi wakaanza kubishana kati yao: Anawezaje
huyu kutupa mwili wake, tule?’ Yesu akaambia, ‘Kweli nawaambieni, msipokula
mwili wa mwana wa Mtu na kunywa damu yake, hamtakuwa na uhai ndani yenu.”
(Yohane 6: 52-53) Jambo hili la kula mwili na kunywa damu ya Yesu lilizua utata
mkubwa katika historia ya Kanisa Katoliki. Mwanzoni wakristo walishitakiwa kuwa
ni watu wala watu. Ni kama Wayahudi waliojiuliza, “anawezaje huyu kutupa mwili
wake?”
Jambo hili linaeleweka hivi. Kama
maji na madini yangekuwa na uwezo wa kusema yangeiambia mimea usipokunywa maji
na kula madini hamtakuwa na uhai ndani yenu. Kama nyasi na maji vingekuwa na
uwezo wa kusema vingewaambia wanyama kama ng’ombe na mbuzi msipokula majani na
kunywa maji hamna uhai ndani yenu. Katika msingi huu kwa vile binadamu ana
mwili na roho Yesu alisema msipokula mwili wangu na kunywa damu yangu hamtakuwa
na uhai ndani yenu. Kushiriki katika
karamu ya Bwana ni muhimu.
Leo hii tunapewa changamoto ya
kushiriki. Katika neno kushiriki tunapata neno ushirikiano. “Tunapomshukuru
Mungu kwa kiokombe kile cha baraka, je, huwa hatushiriki damu ya Kristo? Na
tunapoumega mkate, je, huwa hatushiriki mwili wa Kristo? Kwa kuwa mkate huo ni
mmoja, sisi, ingawa ni wengi, tu mwili mmoja; maana sote twashiriki mkate
huohuo.” (1 Wakorintho 10: 16-17) Basi kushiriki kwetu kusiishie Kanisani
tushiriki katika Jumuiya Ndogo Ndogo. Tushiriki katika maendeleo ya Taifa.
Suala la sherehe ya leo na shukrani
lina msingi wake katika Biblia. “Saa ilipotimia, Yesu akakaa kula chakula
pamoja na mitume wake…Kisha akatwaa kikombe akashukuru, akasema, ‘Pokeeni,
mgawanyiane…halafu akatwaa mkate, akashukuru, akaumega, akawapa akisema, “Huu
ni mwili wangu unaotolewa kwa ajili yenu. Fanyeni hivi kwa kunikumbuka.” (Luka
22: 14-19) Yesu alishukuru alipochukua mkate na divai.
Ekaristi inamaanisha shukrani na mkate
na divai hutumika. Wakristo ambao wanashiriki kumbukumbu ya Karamu ya Mwisho ya
Yesu kwa kuandamana leo wanakumbushwa kuwa na utamaduni wa kushukuru maana ndio
kiini cha sherehe ya leo.
Hellen Keller ambaye alikuwa kipofu
na kiziwi aliandika hivi: “Kila mara nimefikiria ingekuwa baraka kama kila mtu
angekuwa kipofu na kiziwi kwa siku chache wakati wa siku zake za kwanza za utu
uzima. Giza lingemfanya akiri uzuri wa mwanga; ukimya ungemfundisha furaha ya
sauti.” Kuna vitu ambavyo tunavyo lakini
hatukiri uzuri wake na umuhimu wake mpaka tumevipoteza. “Hatuna budi kupata
muda wa kutulia na kushukuru watu ambao wameleta tofauti katika maisha yetu,”
alisema John F. Kennedy.
Katika hadithi za Aesop kuna hadithi juu ya mtumwa aliyeitwa
Androcles ambaye alitoroka toka kwa Bwana wake na kukimbilia msituni. Alipokuwa
akitangatanga alikutana na simba ambaye alikuwa amelala chini akinguruma na
kutoa sauti ya uchungu. Mwanzoni alitaka kukimbia lakini aligundua simba
hakumfukuzia. Alirudi nyuma na kumwendea. Alipomkaribia, simba alionyesha kwato
zake au mguu wake ambao ulikuwa umevimba na ukitoa damu.
Androcles aligundua palikuwepo na
mwiba mkubwa ambao ulikuwa umeingia ndani na ulikuwa unamsababishia maumivu
makali. Aliutoa mwiba huo na kuufunga vizuri mguu wa simba ambaye aliweza
kusimama na kulambalamba mkono wa Androcles kama mbwa. Simba alimpeleka
Androcles kwenye pango lake na kila siku alimletea nyama ya kula na kuweza
kuishi. Lakini baadaye Androcles na Simba walikamatwa.
Androcles alipewa adhabu ya kutupwa
kwenye kibanda cha simba huyo ambaye siku nyingi aliwekwa kwenye kibanda bila
chakula. Mfalme na watu wa ikulu ya mfalme walikuja kushuhudia simba akimrarua
Androcles. Simba aliachiliwa kutoka katika kibanda chake na kumwendea huyo
binadamu akinguruma. Alipomkaribia Androcles alimtambua na kuanza kulamba lamba
mikono yake kama mbwa rafiki.
Mfalme alishangaa alimuomba
Androcles amueleze maana ya hayo yote. Androcles alimweleza mfalme kila kitu.
Mtumwa alisamehewa na kuachwa huru na
simba aliachiliwa arudi msituni. Hayo ni matunda ya kutenda wema kwa Androcles
na kushukuru kwa simba. Shukrani ni mtaji. Shukrani ina malipo.
Hata unapokosewa unajifunza kitu
fulani. “Msamaha wa kweli ni pale unapoweza kusema, ‘Nashukuru wa uzoefu huo,’”
alisema Oprah Winfret. Biblia inatwaambia: “Shukuruni katika kila jambo; maana
hayo ni mapenzi ya Mungu kwenu katika Kristo Yesu” (1 Wathesalonike 5: 18).
Rick Warren katika kitabu chake Maisha
Yanayoongozwa na Malengo alikuwa na haya ya kusema juu ya haya hiyo: “Mungu
anakutaka umshukuru kwamba atatumia matatizo yako kutimiza malengo yake.”
Kusema kweli kutomthamini mwenzako
ni kukufuru maana kushukuru ni kuthamini. Kutoshukuru ni kosa kubwa kuzidi
kulipa kisasi. “Kutoshukuru ni kosa la kudharauliwa zaidi ya kulipa kisasi,
ambacho ni kulipa baya kwa baya, wakati kutoshukuru ni kulipa baya kwa wema,”
alisema William Jordan. Tujenge utamaduni wa kushukuru. Afrika yenye utamaduni
wa kushukuru inawezekana.
Kushukuru ni kumsifu Mungu. Mungu
kama amekujalia watoto, akili, utajiri, amani moyoni, jina jema, mke, mme,
mshukuru ukimsifu. Zingatia maneno haya, “Mtukuzeni Bwana pamoja nami, na tuliadhimishe jina lake
pomoja .” (Zaburi 34:3) Mkumbuke Mungu. Hakuna haja ya kujidai sana sote ni
“CHAKUPEWA.” “Nani amekupendelea wewe? Una kitu gani wewe ambacho hukupewa? Na
ikiwa umepewa, ya nini kujivunia kana kwamba hukupewa?” (1 Wakorintho
4:7). Kuna methali isemayo, “Aliyekupa
wewe kiti ndiye aliyenipa mimi kumbi.” Na aliye na kidogo akitumie kupata
kikubwa.
Kushukuru ni kuthamini zawadi
uliyopewa. Kama Mungu ametupa zawadi ya amani, kushukuru ni kuthamini zawadi
hiyo. Kama Mungu amekupa zawadi ya mke, shukuru ni kuthamini zawadi hiyo. Kama
Mungu amekupa zawadi ya mme, shukuru ni kuthamini zawadi yaani mme. Kama unamshukuru Mungu kwa kuwa
Mkenya, basi itendee Kenya mambo mazuri. Kama unamshukuru Mungu kwa vile wewe
ni mtanzania itendee Tanzania mambo mazuri.
Kushukuru ni kuomba tena. Ukipata
shukuru. Kuna Baba mmoja ambaye alikuwa anatembea kando ya Bahari ya Indi na
mtoto wake wa kiume. Mara wimbi likamchukua mtoto wake wa kiume lakini
akaokolewa na mvuvi Msamaria mwema. Badala ya kushukuru Baba huyo alimuuliza
mvuvi, “Mtoto wangu alikuwa na kofia umeiweka wapi?”
Huo ni ukosefu wa shukrani. Sherehe
ya Ekaristi ambayo inamaanisha shukrani ni changamoto kwa wakristu wote kuwa na
moyo wa shukrani na sio na moyo wa punda. Shukrani ya punda ni mateke
Comments
Post a Comment