TAHADHARI YATOLEWA KUELEKEA KONGAMANO LA VIJANA KANDA YA ZIWA GEITA
MLEZI wa Vijana Wakatoliki
Wafanyakazi (Metropolitani) Kanda ya Mwanza Padri Paschalis Buberwa amewatahadharisha
vijana watakaohudhuria kongamano la Kanda kuvaa mavazi yenye maadili.
Kongamano hilo linatarajiwa
kuwakusanya takribani vijana wakatoliki 2000 kutoka Kanda ya Jimbo Kuu Mwanza
yaani mikoa ya Kanda ya Ziwa ambapo watapata mafundisho ya kiimani, semina za
kimaisha kwa ujumla na pia ujasiriamali kuwawezesha vijana kuwa na shughuli za
vipato vya kujikimu kimaisha.
Akizungumza katika mkutano wa maandalizi
ya Kongamano hilo mapema wiki hii jimboni Geita, Padri Buberwa wa Jimbo
Katoliki Bukoba amesema kuwa miongoni mwa mavazi anayohofia kuvaliwa na vijana
ni pamoja na suruwali mtepesho, sketi fupi, nguo za kubana kwa wavulana
na wasichana.
Amesema mavazi hayo yanapaswa
kukemewa kwa vijana wote, siyo kwenye Kongamano tu bali mahali popote kwa vazi
la mtepesho tafsiri yake ni kujitangaza ushoga kwa anayevaa.
Walezi mbalimbali walikutana katika
makao makuu ya Jimbo Katoliki Geita kutoka majimbo ya Mwanza, Shinyanga,
Musoma, Geita, Bukoba, Bunda, Rulenge Ngara na Kayanga kuandaa Kongamano hilo
litakalofanyika tarehe 15-19 Juni jimboni Geita.
Wajumbe mbalimbali wameonesha
matumaini makubwa kwa Kongamano hili lijalo huku wakibainisha kuwa ni fursa
pekee ya kuwapatia vijana dira ya kimaisha na kiroho na kwamba linawapatia
mwamko mpya juu ya Uinjilishaji wa Vijana katika Kanisa la Tanzania.
Comments
Post a Comment