Mariathon 2017 yavuka malengo
Uongozi wa Redio Maria
Tanzania umewashukuru wadau wake wote, waliopo ndani na nje ya nchi kwa
kuiwezesha redio hiyo kufikia malengo yake, kupitia Kampeni ya Mbio za Mama
Maria (Mariathon 2017), kwa kufanikiwa kukusanya kiasi cha shilingi milioni
480.
Akizungumza na Blog hii juma hili Rais wa Redio Maria Tanzania, Bw. Humphrey Kira amesema
kuwa, katika Kampeni hiyo kwa mwaka 2017, waliadhimia kukusanya kiasi cha
shilingi milioni 450,000, kwa kipindi cha wiki 6, japo walitambua haitakuwa
kazi rahisi kutokana na hali halisi ya uchumi ilivyo.
“Hakika utume wa
Uinjilishaji unaofanywa na Redio Maria Tanzania na dunia nzima ni utume wa
kipekee sana, kwani mambo mengi yanayotukia yanazidi akili za kibinadamu. Redio
hii inaongozwa zaidi na nguvu ya Kimaria, Marian Spirit, maana hata ukiangalia
hali halisi ya uchumi wa wadau wetu siyo nzuri, lakini kwa nguvu za Mungu,
malengo tuliyoyapanga yamefikiwa na kupitiliza,” amesema Kira.
Akifafanua matumizi waliyolenga
kuyatekeleza kutokana na kiwango walichokuwa wamejipangia katika kampeni hiyo,
Bw. Kira ameyataja kuwa ni pamoja na kulipia Masafa (50,000,000), Matumizi ya
Mwezi Mei (90,000,000), Kuchangia Mfuko wa Umisionari (150,000,000) na Vifaa
vya kuboresha Mitambo (160,000,000).
Aidha, Rais huyo wa
Radio Maria Tanzania, kupitia Gazeti hili la Kiongozi ameendelea kutoa wito
wake kwa wadau wa Radio hiyo, waelendee kutenga muda wao adimu kwa kuipenda na
kusikiliza vipindi mbalimbali vinavyorushwa na Redio Maria Tanzania, ili kila
mmoja aweze kushiriki jukumu la
Uinjilishaji na zaidi sana kuuchuchumilia utakatifu ambao kila mmoja
anauhitaji.
Kwa upande wake
Mkurugenzi wa Matangazo Redio Maria Tanzania, Padri John Maendeleo wa Shirika
la Roho Mtakatifu, ameendelea kuwaalika mapadri watawa na walei mbalimbali
wenye ujuzi kuitumia Radio Maria Tanzania, katika kuwalisha wasikilizaji wake
Kiroho na Kimwili kwa kushiriki kuandaa vipindi na vikarushwa na radio hiyo.
“Napenda kuwaalika
Mapadri, watawa wenzangu, walei na wote wenye ujuzi mtumie radio hii kuandaa
vipindi ili kwa pamoja tutekeleze lile agano la Kristo la kuhubiri habari njema
kwa watu wote mpaka nje ya mipaka yetu,” amesema Padri Maendeleo.
Mbio hizo za Mama Maria,
Mariathon 2017 zilizinduliwa rasmi Aprili 28 mwaka huu, na kufungwa Juni 16
mwaka huu na rais wa Redio Maria Tanzania, Bw. Humphrey Julius Kira. Mbio hizo
zilishirikisha Majimbo/mikoa 14 Bara na Visiwani, ambapo Jimbo Kuu Katoliki Songea
ambalo Mariathon ya mwaka jana 2016 lilikuwa la mwisho, mwaka huu limeshika
nafasi ya kwanza Kitaifa, likichukuwa nafasi hiyo toka kwa Jimbo Katoliki Mbeya
ambalo limeshuka na kushika nafasi ya 8.
Nafasi ya Pili
imechukuliwa na Jimbo Mtwara, huku Moshi likishika nafasi ya 3, Iringa(4), Mbinga(5),
Arusha(6), Mpanda(7), Singida(9), Zanzibar(10), Mwanza(11), Dar es Salaam(12) na
mikoa mingine imeshika nafasi ya 14.
Kiasi hicho cha
shilingi milioni 480 kilichokusanywa kwa majuma 6 kimepatikana kupitia njia
zifuatazo, Money box, Vibubu, Bahasha, Michango Binafsi na Harambee mbalimbali
zilizofanywa kwenye Parokia mbalimbali za majimbo tajwa hapo juu, 100200
kupitia mitandao ya air tel money, tigo pesa na m-pesa, ambapo Parokia ya Roho
Mtakatifu Segerea imefanikiwa kwa mara nyingine tena kutetea nafasi yake ya kwanza
kama ilivyokuwa Mariathon ya mwaka jana.
Mbio hizi za Mama Maria
huzihusisha Redio Maria zote ulimwenguni kila mwaka mwezi Mei ambao ni Mwezi wa
Rosari Takatifu, na hii hufanyika kwa heshima ya Mama Bikira Maria, ikiwa na
lengo la kuhamasisha uchangiaji kwa ajili ya kuendeleza Utume wa Radio Maria
Tanzania na Ulimwenguni kote.
Comments
Post a Comment