REDIO MARIA YASHEREHEKEA MIAKA 21 YA UINJILISHAJI MAKINI
Vyombo vya Mawasiliano
vya Kanisa nchini, vimeshauriwa kuwa makini katika kuandaa na kutangaza habari zake,
ili kuepuka kutoa habari ambazo zinaweza kuipotosha jamii, badala yake viandike
habari za kuimarisha mahusiano mema na zenye mashiko.
Wito huo umetolewa na Askofu
wa Jimbo Katoliki Mbeya Mhashamu Evarist Chengula (I.M.C) wakati akifungua rasmi
Hija Takatifu kwa Mahujaji, wanaoshiriki Hija kuelekea Sherehe za Miaka 21 ya Redio
Maria Tanzania, inayoendelea katika ukumbi wa shule ya Sekondari ya wasichana
Loleza Mkoani Mbeya.
Askofu Chengula amesema
kuwa suala la kutangaza Habari kwa njia ya vyombo mbalimbali ni hamu ya Kristo
mwenyewe, kutawanya habari zake katika ulimwengu wote, jambo ambalo hata wakristo
wa kwanza walifanya kazi hiyo ya kupeleka habari njema katika nyakati zao.
Amesema kuwa Redio
Maria Tanzania ilianzishwa hapa nchini kutokana na msukumo uliotolewa kwenye Sinodi
ya kwanza ya Afrika yenye kuhamasisha utangazaji wa habari njema kwa njia ya
vyombo vya habari katika nchi za Afrika na ulimwengu mzima.
Aidha Askofu Chengula
amewataka wakristo, marafiki na wadau wa Redio Maria Tanzania, kumshukuru Mungu
na kufurahi kwa pamoja katika kufanya sherehe za miaka 21, tangu kuanzishwa kwa
Redio hiyo na kwamba uwepo wake umedhihirisha kweli Sauti ya Kristo katika
jamii, pamoja na makundi mbalimbali ya wahitaji kwa kuwapatia Habari njema.
Kwa Upande wake
Mkurugenzi wa Matangazo Redio Maria Tanzania Padri John Maendeleo, CSSp,
amebainisha kuwa wadau wa Redio hiyo hapa nchini, waendelee kujitoa kwa hali na
mali katika kuhakikisha wanashiriki katika uendeshaji wa chombo hicho ili
Injili inayohubiriwa mahali hapo iwafikie walio wengi zaidi huku akiwaalika
kushiriki maadhimisho ya miaka 21 tangu kuanzishwa kwa Redio hiyo hapa nchini.
Hija hiyo iliyoanza
Juni 27 mwaka huu itamalizika Julai 2, imewashirikisha mahujaji wapatao 150,
kutoka katika Majimbo ya Singida, Mpanda, Zanzibar, Mtwara, Iringa, Ifakara,
Mbinga, Moshi, Jimbo Kuu Katoliki Arusha, Mwanza, Songea, Dar es Salaam na wenyeji
Jimbo katoliki Mbeya.
Mahujaji hao wamepata
nafasi ya kushiriki semina mbalimbali kutoka kwa mapadri ambapo Padri Cyrilo
Mwalyolyo ambaye ni Mkurugenzi wa Walei Jimbo Katoliki Mbeya, ametoa mada inayohusu
Nafasi ya Mlei katika Kanisa, padri Lucas Wakuganda, akatoa mada inayohusu
Mkristo na Visakramenti huku padri Frank Mnyema akatoa mada ya Mkristo na
Ushirikina na padri Thelesphory Mtweve akatoa Mada ya Mkristo na Uchumi.
Mbali ya kufunga na
Kusali, Mahujaji hao wamepata nafasi ya kutembelea maeneo ya Hija ikiwa ni
pamoja na kupanda Mlima Loleza, kwenye Kimondo huko Mbozi na Daraja la Mungu
huko Kiwira.
Kilele cha Maadhimisho
ya Miaka 21 ya Uinjilishaji wa Radio Maria Tanzania, kinatarajiwa kufanyika Julai
2 mwaka huu, katika Kanisa Kuu la Kiaskofu la Mtakatifu Anthoni Padua, lililopo
Mbeya Mjini ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri Mkuu Mstaafu Bw. Mizengo
Kayanza Peter Pinda.
Comments
Post a Comment