MTWARA: MASHIRIKA YA KITAWA YAASWA KUSHIRIKIANA
Mashirika ya kitawa yanayofanya kazi jimboni Mtwara, yametakiwa kudumisha ushirikiano, uelewano na kuvumiliana wakati yanapotekeleza wajibu wao wa maisha ya kitawa.
Wito huo umetolewa hivi karibuni na Askofu wa Jimbo Katoliki Mtwara Mhashamu Askofu Titus Mdoe, wakati wa adhimisho la misa takatifu ya nadhiri za daima na za muda kwa masista watatu wa shirika la masista wabenediktini wa Bikira Maria Msaada wa wakristo Ndanda iliyofanyika katika Kanisa la Bikira Maria Msaada wa Wakristo abassia ya Ndanda.
Askofu Mdoe amesema utume wao wa kitawa uwasaidie wafanye kazi kwa umoja ili wapate mafanikio, kwani ni umoja pekee ndio silaha muhimu itakayoleta matunda bora ya kazi.
“Mtawa ameitwa kwa nafasi yake ndani ya jumuiya ya kitawa na tunatakiwa tuilinde tunu hii ili tupate mafanikio,” amesema Askofu Mdoe.
Amewataka watawa hao kila mmoja apende wito alioitiwa sambamba na kupalilia mahusiano na maelewano miongoni mwao na jumuiya zingine za kitawa.
Katika nafasi hiyo amewahimiza watawa wote kuendelea kupanda miito, kuheshimu miito yao na kuheshimu maisha ya jumuiya.
Masista waliofunga nadhiri za kwanza ni Sr. Maria Veronica Chiledi OSB na Sr. Maria Makrina Ngole OSB na nadhiri za daima Sr. Maria Glads Mkundachuma ASB
Kwa upande wake mama mkuu wa shirika hilo la Bikira Maria Msaada wa Wakristo Ndanda, Sr Maria Calitas Swai OSB ameomba wazazi, ndugu na jamaa kuwaombea waliofunga nadhiri, huku akisisitiza wazazi kuwatoa vijana wao katika miito.
Na Jimmy Mahundi, Mtwara
Comments
Post a Comment