Mwezi Juni ni wa heshima kwa Moyo Mtakatifu wa Yesu (2)
HAPO
ndipo Bwana wetu Yesu Kristo alipomwambia Mtakatifu Margareta Maria Alakoki
kuwa ataiweka siku maalum ya kufanya malipizi ya pekee kwa kufidia madharau na
mabaya mengine yote yaliyokuwa yametendwa dhidi yake. Siku hiyo ndio ile Ijumaa
ya kwanza inayofuata, baada ya sherehe ya Mwili na Damu ya Bwana wetu Yesu
Kristo kama ilivyokwisha kudokezwa hapo awali.
Ibada
ya heshima kwa Moyo Mtakatifu wa Yesu inaidhinishwa rasmi na Papa:
Baada ya kifo cha Margareta Maria Alakoki hapo tarehe ya 17 ya mwezi wa Oktoba,
mwaka wa 1690, Mashirika ya Kitawa tu ndiyo yaliyokuwa yameruhusiwa na Roma
kuadhimisha misa maalum kwa heshima ya Moyo Mtakatifu wa Yesu. Lakini kuanzia
mwaka 1856 Baba Mtakatifu Pius wa 1X aliliruhusu Kanisa Katoliki kwa jumla wake
popote ulimwenguni kuwa na adhimisho la Misa Maalum kwa heshima ya Moyo
Mtakatifu wa Yesu.
Baba Mtakatifu Pius wa
X aliamuru ile ibada ya kuuweka wakfu ulimwengu wote kwa Moyo Mtakatifu wa Yesu
iliyofanywa kwanza na Papa Leo wa X111
irudiwe kila mwaka. Baba Mtakatifu Pius wa X1 katika Waraka wake wa
Kipapa wa tarehe ya 8 ya mwezi wa Mei, mwaka wa 1928 “Miserentissimus
Redemptor”-Mwokozi aliyejaa huruma- alikiri kuwa ni kweli Bwana wetu Yesu
Kristo alikuwa amejidhihirisha mwenyewe alipomtokea Margareta Maria Alakoki na
kutoa ahadi za neema kwa wale watakaouheshimu moyo wake.
Waraka huo wa Baba
Mtakatifu Pius wa X1 ulikuwa unarudia
tena na tena yale mazungumzo kati ya Bwana wetu Yesu Kristo na Mtakatifu Margareta
Maria Alakoki yakithibitisha umuhimu wa kuuheshimu Moyo huo wa Bwana wetu Yesu
Kristo kwa fidia ya dhambi zetu.
Siku ya kumbukumbu ya
miaka 100 ya kuanzishwa kwa sherehe ya Moyo Mtakatifu wa Yesu iliyozinduliwa na
Baba Mtakatifu Pius wa 1X, Baba Mtakatifu Pius wa X11, aliwaeleza waamini
Wakatoliki wote kwa kinaganaga sana, katika Waraka wake wa Kipapa “Haurietis
aquas” wa mwezi Mei, mwaka wa 1956 umhimu wa ibada hii ya Moyo Mtakatifu wa
Yesu.
Baba Mtakatifu Benedikti wa XVI
alimpelekea barua ya pongezi Padri Kolvenbach, Mkuu wa Majesuiti, kwa
kumbukumbu ya miaka 50 tangu ulipotolewa ule Waraka wa Kipapa “Haurietis aquas”
na Baba Mtakatifu Pius wa IX. Baba Mtakatifu Benedikti wa XVI alikuwa
ameongelea, katika barua ile ya pongezi, kwa marefu na mapana, umuhimu wa kuwa
na ibada hii ya Moyo Mtakatifu wa Yesu.
Mwanzo
wa Ibada ya Moyo Mtaktifu wa Yesu na kuenea kwake: Ingawa dalili ya ibada
hii ya Moyo Mtakatifu wa Yesu ilianza kuonekana kuanzia kwenye karne ya kumi na moja na kumi na mbili kule Bara la
Ulaya, hapa nchini kwetu Tanzania
iliingia kwenye kati ya mwaka 1917 na mwaka 1919. Ibada ya Moyo Mtakatifu wa
Yesu ilianza na utoaji wa heshima kwa Madonda Matakatifu ya Bwana wetu Yesu
Kristo na hasa utoaji wa heshima kwa lile Donda lake la ubavuni.
Mtakatifu Bernardo wa
Klervo (1090-1153) anaonekana kujitokeza mara nyingi zaidi katika hizo karne za
mwanzo wa hiyo ibada. Hata hivyo inaonekana ni mashirika ya nyumba za kitawa tu
yaliyoanza kujitokeza sana katika uzingatiaji wa ibada hii. Mashirika
yaliyokuwa yamejitokeza zaidi ni yale ya Kifransiskani, Kidominikani, Kijesuiti
na ya Kibenediktini.
Aliyekuwa wa kwanza kabisa kuweka msingi
wa kiteolojia wa ibada hii alikuwa mtawa
mmoja wa shirika la Kijesuiti aliyeitwa Kasper Druzbicki (1590-1662). Kasper
Druzbicki, katika kitabu chake “Meta Cordium- Cor Jesu” yaani, “lengo la mioyo
yetu ni Moyo wa Yesu,” ndimo kulikokuwa msingi wa Kiteolojia wa ibada hii ya
Moyo Mtakatifu wa Yesu.
Muda mfupi baada ya
Kasper, alijitokeza Jean Eudes aliyetunga hata sala za ibada kwa Moyo Mtakatifu
wa Yesu na akapendekeza kuwe na sikukuu maalum kwa ibada hiyo. Jean Eudes
alikuwa pia shabiki sana wa heshima kwa Moyo safi wa Bikira Maria.
Jinsi muda ulivyozidi
kupita mgawanyo wa heshima zake kwa mioyo hii miwili ilizidi kuwa wazi zaidi na
ilipofika tarehe ya 31 ya mwezi Agosti mwaka 1670 uamuzi wa kuwa na sherehe
mbili tofauti ulikuwa umefikiwa na kulianzishwa rasmi sikukuu ya Moyo Mtakatifu
wa Yesu.
Hata kabla ya kujitokeza Mtakatifu
Margareta Maria Alakoki (1647-1690) ambaye Bwana wetu Yesu Kristo alikuwa
ameamua kumtumia zaidi katika kuendeleza ibada ya heshima kwa moyo wake,
kulikuwa na watakatifu wengine kadhaa pamoja na Wenyeheri ambao pia walihusika
kwa namna moja au nyingine katika kuikuza ibada hii hasa kwa kujihusisha
wenyewe katika kuizingatia.
Baadhi ya watakatifu na
Wenyeheri hao ni kama Mtakatifu Lutgarda(1298); Mtakatifu Mektilda(1298);
Mtakatifu Getruda(1301); Mwenyeheri Maria wa Moyo Mtakatifu (1863-1899);
Mwenyeheri Estelle Faguetta (ca1840) na wengine.
Baada ya uchunguzi wa Kanisa Katoliki kwa
muda wa kutosha kama ilivyo kawaida yake, ibada hii ya Moyo Mtakatifu wa Yesu,
iliidhimishwa rasmi kama ilivyokwisha kudokezwa hapo awali na ikaendelea kuenea
katika nchi mbalimbali Tanzania ikiwa
moja ya nchi hizo.
Kuanzia kwenye miaka ya 1850 hivi, vikundi
vya waamini, mashirika ya kidini na hata majimbo ya nchi yamejitoa wakfu kwa
Moyo Mtakatifu wa Yesu. Mwaka 1873 nchi ya Ecuador, ilikuwa nchi ya kwanza
ulimwenguni kujitolea wakfu kwa Moyo Mtakatifu wa Yesu.
Ahadi kwa wenye mazoea ya kuwa na ibada ya
Moyo Mtakatifu wa Yesu: Kuna ahadi lukuki zilizotolewa na
Bwana wetu Yesu Kristo kwa wale watakaokuwa na mazoea ya kufanya ibada kwa
heshima ya Moyo Mtakatifu wa Yesu. Ahadi
alizozitoa kupitia kwa Mtakatifu Margareta Maria Alakoki zilikuwa kumi
na mbili na ziliorodheshwa na kupangwa katika jedwali hapo mwaka 1863.
Mwaka 1882 alitokea
mfanyabiashara mmoja wa taifa la Kimarekani aliyegharamia kuzitasfiri na
kuziandika ahadi zile zote katika lugha 238 na zikasambazwa ulimwenguni kote.
Mwadhama Adolph
Kadinali Perrand hakupendezwa na kile kitendo cha usambazaji wa ahadi hizo
katika zile lugha kwa sababu baadhi ya ahadi zilikuwa na maneno ambayo yalileta
maana tofauti na alivyotaka kueleza Mtakatifu Margareta Maria Alakoki. Mwadhama
Adolph Kadinali Perrand akaagiza ahadi zichapwe kwa kutumia maneno yale yale ya
asili aliyoyatumia mwenyewe Mtakatifu Margareta Maria Alakoki.
Comments
Post a Comment