Shirika la Imaculate Heart of Sister Africa lampoteza Mtawa wa kwanza Musoma

Shirika la Imaculate Heart of Sister Afrika (IHSA) limempoteza Mtawa wa kwanza aliyefunga nadhiri za kwanza za utawa katika Jimboni Musoma Sr.Maria  Bernadeta Abel, aliyefariki akiwa na umri wa miaka 90 ya kuzaliwa na miaka 60 ya utawa, Juni 16 mwaka huu baada ya kuugua.

Sr.Maria Bernadeta ambaye alifunga nadhiri za kwanza Mei 3,1957 amekuwa ni chachu ya miito ya utawa Jimboni Musoma na amekuwa kielelezo na alama isiyofutika ndani ya shirika hilo, kwa kuwa ni moja kati ya watawa ambao waliishi kwa imani wakimtegemea Mungu.

Akihubiri wakati wa ibada ya kumuombea marehemu Sr.Bernadeta Abel iliyofanyika katika Kanisa la Novisiati Makoko, Padri John Bosco Kiyuga wa parokia ya Myamiongo amesema kuwa, wakristo wanatakiwa kuiga mfano wa Sr.Bernadeta kwa kuishi maisha ya furaha muda wote yanayompendeza Mungu, kwa kuwa muda wa mwanadamu kuishi hapa duniani ni mfupi sana.

Padri Kiyuga amesema kuwa wazazi na walezi katika familia wanatakiwa kuweka misingi mizuri na imara kwa watoto wao kama ambavyo familia ya Abel iliweka msingi imara kwa Sr Bernadeta kwani hata alipokuwa akikutana na vikwazo vingi katika safari yake ya utawa hakuwahi kukata tamaa, kwa kuwa alijua kuwa anafanya kazi ya Mungu na siku moja atapata tuzo huko mbinguni.

“Shirika poleni sana kwa kupoteza na Jimbo tumepoteza  mtu muhimu Sr.Bernadeta amesaidia sana katika ukuaji wa imani na miito katika Jimbo letu la Musoma, kupitia yeye tunajifunza pia kuishi maisha ya furaha na ya kumtegemea Mungu,”amesema Padri kiyuga.

Kwa upande wake Mama Mkuu wa Shirika hilo, Sr.Maria Lucy Magumba amesema kuwa  hakika hawatamsahau Marehemu Sr.Maria Bernadeta Abel, kwani alikuwa ni mnyenyekevu, mwenye moyo wa huruma, mvumilivu na aliyependa kusema asante kwa kila jambo alilofanyiwa hata katika umri wake wa uzee alifurahia sana uzee wake na hakupenda kumkwanza mtu, alikuwa ni mtu mwenye furaha muda wote na hata kifo chake alikitabiri.

Wakitoa salamu sa rambirambi baadhi ya waamini waliomfahamu marehemu Sr.Maria Bernadeta Abel akiwemo aliyekuwa waziri wa Kazi, ajira na Vijana Gaudencia Kabaka wamesema kuwa marehemu alikuwa ni mfano bora wa kuigwa na watawa wengine pamoja na walei wengine kwani hata katika kazi za mikono alikuwa anajituma sana, na alikuwa muinjilishaji mzuri wa huduma za kiroho.



Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

MJUE MTAKATIFU MARIA GORETTI