Vyanzo vya hukumu za kesi za ukatili wa watoto kuchelewa vyabainishwa
“TATIZO la
jamii kushindwa kutoa ushahidi kwenye kesi zinazohusu ukatili dhidi ya watoto
na wanawake ni kichocheo cha kutosikilizwa ama kuchelewa kwa kesi hizo na
watuhumiwa kutochukuliwa hatua za kisheria.
Hayo yamesemwa na Naibu Msajili wa
Mahakama Kuu Kanda ya Moshi, Bernad Mpepo wakati wa kikao na watetezi wa haki
za binadamu kilichoandaliwa na shirika lisilo la kiserikali la kutetea haki za
binadamu na jinsia mkoa wa Kilimanjaro (KWIECO).
Amesema kesi nyingi zinachukua muda
mrefu na nyingine kufutwa kutokana na kukosekana kwa ushahidi jambo
linalowanyima haki waathirika wa ukatili huo.
Awali akitoa taarifa kwa wadau wa haki
za binadamu wakiwemo polisi, wanasheria, maofisa ustawi wa jamii na wataalamu
wa sheria toka nchini Kanada, Mkurugenzi wa Kwieco, Elizabeth Minde amekosoa
Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971.
Minde ameiomba Serikali kufanya
marekebisho ya sheria zinazochangia kuongeza matukio ya kikatili ikiwemo sheria
hiyo na sheria nyingine kandamizi pamoja
na kuwawezesha kitaalamu waendesha mashtaka na maofisa ustawi wa jamii ili
kurahisisha utendaji na upatikanaji wa haki kwa waathirika wa ukatili nchini.
Amesema Sheria ya Ndoa ya Mwaka 1971
inamtambua mtu mwenye umri kuanzia miaka 14 kuwa anaweza kuolewa jambo ambalo
linakinzana na Katiba ya Tanzania inayomtambua mtu mzima kuwa ni kuanzia miaka
18.
Minde amesema umri wa miaka 14
umebainika kuwa na changamoto kubwa kwa wasichana wanaoolewa na wengine
kuozeshwa bila ridhaa yao kwa lengo la wazazi wa msichana kupata mali kutoka
upande wa muoaji wakati kwa umri huo wasichana wengi bado hawajapevuka vizuri
kuweza kutumikia majukumu ya ndoa.
Naye mwanaharakati
wa haki za binadamu kutoka shirika la NAFGEM, Francis Selasini amesema ipo haja
kwa mahakimu kupewa mafunzo maalumu ya taratibu za kisheria hasa katika kesi
zinazohusiana na haki kwa wanawake na watoto, madaktari na wauguzi pamoja na maafisa ustawi wa jamii
wanaohudumia watoto na wanawake ambao wamekuwa wakifanyiwa vitendo mbalimbali
vya kikatili.
Comments
Post a Comment