Yaliyojiri kwenye mkutano wa Baraza la Makardinali Washauri

Baraza la Makardinali washauri kuanzia tarehe 12 – 14 Desemba 2016 limekuwa na mkutano wake chini ya uongozi wa Baba Mtakatifu Francisko, isipokuwa Jumatano, tarehe 14 Desemba 2016 ilimbidi kutoa katekesi yake siku ya jumatano kuhusu matumaini ya Kikristo! Wajumbe wamejadili kwa sehemu kubwa mabaraza ya Kipapa mintarafu Katiba Mpya ya Kitume inayotarajiwa kuchapishwa hivi karibuni na Baba Mtakatifu Francisko. Mabaraza yaliyopembuliwa kwa kina na mapana ni Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu; Sekretari kuu ya Vatican, Baraza la Kipapa kwa ajili ya Maaskofu pamoja na Baraza la Kipapa la Makanisa ya Mashariki. haya yamebanishwa na Dr. Greg Burke, Msemaji mkuu wa Vatican.
Mambo makuu ambayo yamejitokeza kama sehemu ya mchakato wa mageuzi yanayopaswa kutekelezwa na Vatican kwa wakati huu: Umissionari na dhana ya Sinodi. Itakumbukwa kwamba, Baraza la Makardinali limekwisha hitimisha uchambuzi wake kwa Mabaraza mengine kama vile: Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa, Baraza la Kipapa la Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume, Baraza la Kipapa la kuwatangaza waamini kuwa wenyeheri na watakatifu pamoja na Baraza la Kipapa la kuhamasisha Umoja wa Wakristo. Mapendekezo yote yamekwisha wasilishwa kwa Baba Mtakatifu Francisko ili aweze kuyatolea maamuzi.
Kwa namna ya pekee, Baraza la Makardinali limetumia muda mrefu ili kuangalia utendaji wa Mabaraza Mapya ya Kipapa yaliyokwisha kuundwa na Baba Mtakatifu Francisko. Kardinali Kevin Farrel, Rais wa Baraza la Kipapa laWalei, Familia na Maisha amepembua kwa mapana nafasi na dhamana ya waamini walei katika maisha na utume wa Kanisa. Amewaalika wajumbe, kusoma na kuutafakari Waraka wa kichungaji wa Papa Francisko kwa Kardinali Marc Ouellet, Rais wa Tume ya Kipapa kwa ajili ya Amerika ya Kusini.
Kardinali Peter Turkson, amewasilisha mpango kazi wa Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Endelevu kwa Binadamu linalounganisha Mabaraza makuu manne ya kipapa yaani: Haki na Amani; Cor Unum; Huduma za Kichungaji kwa wafanyakazi katika sekta ya afya; Wahamiaji na Watu wasiokuwa na makazi maalum. Kardinali Turkson alikuwa ameandamana na Askofu mkuu Silvano Maria Tomasi ambaye amekiri kwamba, Baraza jipya la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Endeldevu kwa Binadamu ni utekelezaji wa maamuzi yaliyotolewa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican katika Waraka wao kuhusu “Kanisa katika ulimwengu Mamboleo” “Gaudium et spes”.
Kwa upande wake Kardinali Sean O’Malley, Mwenyekiti wa Tume ya Kipapa kwa ajili ya Ulinzi kwa watoto wadogo na Kardinali George Pell amefafanua hatua msingi zilizochukuliwa na Sekretarieti ya Uchumi mjini Vatican ambayo iko chini ya uongozi wake. Mheshimiwa Padre dario Edoardo ViganĂ², Mwenyekiti wa Sektretarieti ya Mawasiliano amewasilisha mambo msingi yaliyokwishafanyika kama sehemu ya mchakato wa mageuzi makubwa kwenye vyombo vya mawasiliano ya jamii vinavyomilikiwa na kuendeshwa na Vatican, mkazo ukiwa ni kwa ajili ya majiundo endelevu kwa wafanyakazi katika tasnia ya mawasiliano mjini Vatican. Mkutano mwingine wa Baraza la Makardinali Washauri utafanyika kuanzia tarehe 13- 15 Februari 2017.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

MJUE MTAKATIFU MARIA GORETTI