Askofu Rwoma: Msitoe wala kushiriki kutoa mimba
Askofu wa jimbo katoliki Bukoba Mhashamu Desiderius Rwoma amewataka
wanawake wote wakristo nchini kukataa kupokea shinikizo lolote la kutoa mimba
wakiiga mfano wa Bikira Maria alivyokubali kumleta duniani Mkombozi wao Yesu
Kristo.
Askofu Rwoma ametoa rai hiyo wakati wa mahubiri yake kwa
niaba ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania kwenye adhimisho la misa takatifu ya Krismasi
kitaifa iliyofanyika katika kanisa kuu la jimbo katoliki Bukoba.
“Kataeni aina yoyote ya ushawishi ama sababu zozote zile
ambazo zinaweza kuwasukuma kukubali kutoa mimba, ukitoa mimba licha ya kumkosea
Mwenyezi Mungu na kiumbe kisicho na hatia, pia umelikosesha taifa pengine mtu
ambaye angechangia katika maendeleo yake,” amefafanua.
Amesema Yesu Kristo aliyezaliwa ni mkombozi wa kila mtu,
hivyo kuzaliwa kwake ni furaha kubwa na wakristo hawana budi kusherehea kwa
kufurahi kwani imefunuliwa neema ya Mungu inayowakomboa wote.
“Krismasi ni kipindi cha neema na fursa adhimu ya kufurahi,
kubaki na neema hizi alizotuletea Yesu, basi tuwe na shukrani pia kuthamini
kile ambacho Mwenyezi Mungu ametujalia katika siku hii muhimu,” amesisitiza
Askofu Rwoma amesema watoto ni zawadi pia mali ya Mungu siyo
ya wanadamu, akimaanisha kwamba ni jukumu la kila mkristo kuhakikisha kuwa
anaipokea na kuithamini zawadi ya mtoto aliyopewa pasipo kuidhuru ama kuipoteza
akisema kuwa kufanya hivyo ni kumkufuru Mwenyezi Mungu.
“Endapo Bikira Maria angeshawishika kwa namna yoyote
kutokumzaa mtoto Yesu nini kingetokea kwa dunia ya leo?, nani angekuja
kutukomboa?, nani angetufariji katika mateso kadhaa tunayopitia kila siku?,
nawasihi mzingatie mfano huu pia mmuishi Mama yetu Bikira Maria kwa kitendo
chake cha ujasiri na upendo kwetu wote.”
Amewataka wanaume wote duniani kuwaheshimu na kuwathamini
wanawake kwa mfano wa Bikira Maria wakizingatia alivyouletea ulimwengu mkombozi
Yesu Kristo.
Aidha Askofu Rwoma amewakumbusha watanzania kuishi kwa
amani, Baraka, upendo na rehema ili kuendelea kuilinda amani iliyopo ambayo kwa
miaka kadhaa imekuwa ikitamaniwa na mataifa mengi ambayo yameteseka kwa siku
nyingi kutokana na migogoro isiyokoma.
Akizungumzia baadhi ya wananchi wenye tama ya mali na
mafanikio ya harakaharaka, Askofu Rwoma amekemea vikali tabia hiyo kwani
husababisha kwa kiwango kikubwa kuwanyima wanyonge haki ya kupata maendeleo,
huduma za kijamii na hata kuishi kwa amani.
“Tuthamini ufukara kwani utajiri na fahari vinapita tu, haya
yote siyo kikwazo cha wewe kuingia mbinguni, la msingi hapa ni kupokea kwa
unyenyekevu yote tunayoelekezwa kwa namna yoyote ile pia kuridhika na
tukipatacho kwani kinatoka kwa Mwenyezi Mungu, kufanya hivyo kutampendeza yeye
na hatimaye tutakuwa katika mazingira mazuri zaidi,” amesema Askofu Rwoma
Askofu Rwoma pia amekemea vikali tabia ya uharibifu wa
mazingira iliyokithiri katika maeneo mbalimbali nchini akiitaka jamii kuacha
mara moja tabia hiyo kwani isipokoma italiingiza taifa katika ukame, njaa na
kusababisha vifo na migogoro isiyo ya lazima.
Ameitaka serikali kufanya jitihada za kina kukomesha hali
hiyo ya uharibifu wa mazingira na ikiwezekana itoe adhabu kali kwa wote
watakaoendelea na tabia hiyo inayotishia uhai wa wanadamu na viumbe hai
vingine.
Na Bernard James
Comments
Post a Comment