Wakristo watahadharishwa juu ya manabii wa uwongo.
ASKOFU
Bruno Ngonyani wa Jimbo Katoliki Lindi amewataka wakristo kujihadhari na
manabii wa uwongo wanaofika kwa kisingizio kuwa wana uwezo wa kuponya magonjwa
na kutoa fedha bure.
Askofu Bruno Ngonyani ameyasema hayo hivi karibuni katika
Dominika ya pili ya majilio wakati akihubiri katika Kanisa kuu la Mtakatifu
Matias Mulumba mjini Songea.
Amesema waamini wengi wamekuwa wakitekwa na baadhi ya
wahubiri wanaojifanya wana uwezo wa kuponya magonjwa na kuwapatia fedha.
“ Tuwe waangalifu na wahubiri wanaosema wana uwezo wa
kuponya magonjwa na kutengeneza pesa, tusiamini kila roho, tuzijaribu kama
zimetoka kwa Mungu au la, kama ametoka kwa Mungu tumwamini na kama hajatoka kwa
Mungu tuachane naye,” amesema Askofu Bruno Ngonyani.
Ameongeza kuwa, Yesu Kristo alisema angalieni mtu
asiwadanganye, maana manabii wengi wa uwongo watatokea na kuwadanganya wengi
msiwasadiki. Amesema Mungu anaruhusu mwanadamu apate maradhi na anataka abandukane
nayo kwa njia halali.
Pia amewataka waamini kuwa na imani thabiti isiyoyumbishwa
na kuishi kama Yesu Kristo, alivyoishi, kumtambua
na kumkiri Yesu Kristu aliye Bwana, mwalimu na kiongozi katika maisha ya
Imani ya kikristo.
Akiwa jimboni Songea Askofu Bruno Ngonyani ameongoza misa
takatifu ya mazishi ya Sister Maria Bernada Mbepera OSB wa shirika la Mtakatifu
Agnes Chipole, ambapo amesema,”sisi ni raia wa mbinguni na msingi wa muungano
wetu na Yesu Kristo ni ubatizo, ambamo tunapata hadhi na kufanyika kuwa watoto
wa Mungu na warithi wa mbingu, hapa duniani tunakaa kwa muda tu na ikifika
wakati tutapaswa kuondoka kwenda mbinguni kwenye makao ya kudumu.”
Sr. Bernada alikuwa muuguzi na mkunga na amewahi kufanya
kazi ya utume katika hospitali ya Peramiho na Ikelu iliyopo katika jimbo la
Njombe. Pia alikuwa mtu wa sala, mtii, mpole, mnyenyekevu, mwenye kujituma,
mcheshi, mpenda amani, mvumilivu katika mateso,na mpenda kutoa na kupokea
ushauri.
Alizaliwa mwaka 1977, akajiunga na shirika la Mtakatifu
Agnes Chipole mwaka 1997, alifunga nadhiri za kwanza mwaka 2004 na nadhiri za
daima mwaka 2013.
Comments
Post a Comment