Shinyanga washauriwa kusomesha watoto wa kike
ASKOFU wa Jimbo Katoliki Shinyanga
Mhashamu Liberatus Sangu ametoa wito kwa jamii kuwekeza zaidi katika
elimu kwa kuwasomesha watoto wa kike na kuacha mila na desturi mbaya ya kuwaozesha
kwa tamaa ya ng’ombe.
Akiongea na wazazi na walezi katika
mahafali ya 18 ya kidato cha nne ya shule ya sekondari ya Don Bosco iliyopo
Didia jimboni Shinyanga, Askofu Sangu ameitaka jamii kuwekeza zaidi kwenye
elimu kwa kutoa upendeleo kwa wasichana kwa sababu ukimwelimisha
mtoto wa kike umeelimisha taifa.
Askofu Sangu amesema familia bora
hutokana na mama aliyeelimika na kuitaka jamii kuacha mila na desturi mbaya
zilizopitwa na wakati za kuwaozesha watoto wa kike katika umri mdogo kwa ajili
ya tamaa ya mali na ng’ombe.
Amesema katika ukanda wa mkoa wa
Shinyanga unaokabiliwa na changamoto ya mauaji ya vikongwe na watu wenye
ulemavu wa ngozi ( albino ) kwa imani za kishirikina kutokana na ujinga
na tamaa ya mali jamii inatakiwa kupiga vita vitendo hivyo kwa
kuwekeza kwenye elimu inayowajenga watu kwenye uelewa.
“ Ujinga ni mbaya sana hasa
kwa nyakati hizi ndiyo unaosababisha baadhi ya watu kuwaua wenzao
kwa imani za kishirikina, huwezi ukamtafuta Mungu kwa ujinga, tunahitaji
elimu ya ukombozi itakayotusaidia kumjua Mungu katika
maisha yetu,” amesema Askofu Sangu.
Askofu Sangu amewaasa vijana
wanaohitimu elimu yao kuishi kwa matendo mema na wawe mitume wa
upendo kwa wazazi na walezi wao na mahala popote
watakapoishi na wawe chimbuko la maendeleo ya kiroho na kimwili
huku akiwataka wasibweteke na elimu hiyo bali wajiendeleze zaidi.
Naye Mkuu wa shule ya Sekondari ya
Don Bosco yenye wanafunzi mchanganyiko wa kiume na kike Padri Richard
Mtui katika taarifa yake amesema jumla ya wanafunzi 176 wamehitimu kidato cha
nne na kuwataka kutumia malezi na elimu waliyoipata vizuri
katika kupambana na changamoto mbalimbali katika maisha yao.
Kwa upande wake Padri Mathias
Isaka amewataka wazazi na walezi kuendelea kuwasaidia watoto hao katika
kuwajenga kiroho na kimwili juu ya kuwaasa, kuwakemea, kuwaonya kwa
sababu dunia ya sasa vijana wanakabiliwa na changamoto nyingi ili wasiweze kujiingiza katika makundi maovu yenye
tabia mbaya miongoni mwa jamii.
Comments
Post a Comment