‘Jamii isiyowajibika chanzo cha mmomonyoko wa maadili’
IMEELEZWA
kuwa kukithiri kwa vitendo vinavyoashiria mmomonyoko wa maadili nchini
kunachangiwa na kutowajibika kwa wazazi, walezi na jamii kwa ujumla.
Hayo yameelezwa na Askofu
Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki Dar es salaam, Mhashamu Eusebius Nzigilwa,
alipokua anaongea na watoto waliopo katika mahabusu ya watoto Upanga jijini Dar
es salaam, kabla ya kutoa zawadi za Krismas, zilizotokana na michango ya Watoto
wa Shirika la Kimisonari la Utoto Mtakatifu, Dekania ya Mtakatifu Yosefu.
Askofu Nzigilwa amesema kuwa
kitendo cha watoto kuwa mahabusu au gerezani na kukithiri kwa watoto wa mitaani,
ni ishara kuwa kuna watu wazima, iwe wazazi, walezi au jamii, haijawajibika,
jambo linalopaswa kupatiwa ufumbuzi wa haraka.
“Kuna picha iliyojengeka kwa
watu wengi ambayo siyo sahihi kuwa watu waliofungwa siyo wema. Picha hii haina
uhalisia, huko mtaani kuna watu wengi ambao wanatenda uovu kila kukicha. Kwa
uwepo wenu hapa wanaopaswa kulaumiwa siyo ninyi, bali kuna watu wazima
hawajawajibika” ameeleza.
Aidha Askofu Nzigilwa amesema
kuwa utoaji wa zawadi hizo za Krismas uliofanywa na watoto wa kipapa, umetokana
na malezi wanayopatiwa watoto hao ya kumpenda Mungu na jirani, hasa wenye
mahitaji na waliozuiliwa.
“Zawadi hizi ni ukarimu wa hawa
watoto, siyo sisi maaskofu au wazazi wao. Kazi yetu sisi ni kuwalea ili wawe na
moyo wa kujitoa. Hivyo nawapongeza watoto hawa ambao hufanya matendo haya ya
upendo kila mwaka, nah ii leo wamejigawa katika makundi na wametembele sehemu
6” ameongeza.
Katika hatua nyingine Askofu
Nzigilwa ameagiza kufanyika kwa tathmini na upembuzi yakinifu ili kuona
uwezekano wa kuchimba kisima kwa ajili ya kutatua changamoto ya upatikanaji wa
maji, ambayo inakabili mahabusu hiyo kwa muda mrefu.
Askofu Nzigilwa amemuagiza
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Walei Parokia ya Mtakatifu Maurus Kurasini, Bwana
Melkiori Ngonyani, kushirikiana na uongozi wa mahabusu hiyo katika kufanya
tathmini ya awali, na iwapo watabaini uwepo wa maji chini ya ardhi, waamini
watahamasishwa kuchangia ili kumaliza changamoto hiyo.
“Mshirikiane katika kupima
tuone kama kuna maji, baada ya hapo tutawaomba waamini na nina uhakika
watachangia na kumaliza kabisa changamoto hii ya maji. Hivyo kuhusu suala la changamoto
ya maji naomba hilo tulibebe sisi” amesema.
Awali akielezea changamoto
zinazoikabili mahabusu hiyo, Afisa Mfawidhi wa Mahabusu hiyo Ramadhan Yahaya
amesema kuwa baadhi ya kero zinazohitaji kupatiwa suluhisho ni ukosefu wa dawa
na upungufu wa maji safi na salama kwa ajili ya matumizi ya kila siku.
“Tangu nimekuja kituo hiki
miaka mitatu iliyopita, kituo kinakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa maji.
Tunadaiwa bili kubwa zaidi ya Sh. Milioni 5, hadi kupelekea kukatiwa huduma ya
maji” ameeleza Bwana Yahaya.
Comments
Post a Comment