Balozi mstaafu azipa kwaya somo zito

MOROGORO, waamini wakatoliki wametakiwa kukataa kupeperushwa huku na kule kwa kufuata mafundisho tofauti ambayo yapo kinyume na utaratibu wa kanisa katoliki.
Rai hiyo ameitoa Balozi mstaafu wa Tanzania nchini Urusi Dr Jaka Mwambi hivi karibuni alipokuwa akizindua Albamu mbili za video za kwaya kuu ya Mtakatifu Patris jimboni Morogoro.
Mwambi amesema waamini wa kanisa katoliki wanatakiwa wasimame imara na wanachokiamini na kukataa kupelekwa pelekwa na kufuata mafundisho ambayo hayahusiani na misingi ya kanisa katoliki.
“umefika wakati sisi wenyewe kusimama thabiti na imani yetu ya kanisa katoliki na tusikubali kupeperushwa huku na kule kwa mafundisho ya kigeni ambayo yapo kinyume na utaratibu wa kanisa takatifu katoliki,” amesema Dr.  Mwambi.
Amesema imani haba ndiyo inafanya baadhi ya waamini wakatoliki kuhangaika huku na kule na wanapofika huko walikopotelea hukuta hali ni tofauti na vile walivyotarajia kwa kukuta walivyotangaziwa havipo, pale ndipo unakuta wengine wanapotea moja kwa moja na wengine wakifanikiwa hurudi kundini.
Wakati huohuo amewataka wanakwaya wa kwaya kuu ya kanisa la Mtakatifu Patris kutumia sauti zao vyema kumtukuza Mungu na si vinginevyo kwani anayemwimbia Mungu husali mara mbili.
“acheni kutumia sauti zenu kutukuza na kusifu mizimu, matambiko na wachawi, badala yake tumieni vipawa ambavyo Mungu amewapatia kumtukuza yeye kwa nyimbo na sala, kufanya hivyo ni kujisafishia njia machoni pa Mungu,” amesema Dr. Mwambi.

Balozi Mstaafu Jaka Mwambi amesema kama unatumia sauti kufanya vitu ambavyo havimpendezi Mungu, huko ni kumdhihaki, kumkufuru na kumchukiza tena kwa kukusudia.

Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

MJUE MTAKATIFU MARIA GORETTI