Mauaji ya kimbari Rwanda! Kanisa: kumbu kumbu na msamaha!
Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu
imekuwa ni fursa ya kutafakari kwa kina na mapana kuhusu Kanisa Katoliki na
mauaji ya kimbari nchini Rwanda, ili kuomba msamaha, tayari kwa waamini na watu
wote wenye mapenzi mema kujikita katika huruma na upendo wa Mungu unaoganga na
kuponya majereha ya maisha ya mwanadamu, tayari kuanza upya katika haki, amani,
upendo na msamaha wa kweli.
Askofu Philippe Rukamba, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki
Rwanda kwa niaba ya Kanisa Katoliki, lakini zaidi kwa wakleri, watawa na
waamini walioshiriki kwa namna mbali mbali kwenye mauaji ya kimbari nchini
Rwanda yaliyotokea kati ya Mwezi Aprili hadi Julai 1994 na kupelekea zaidi ya
watu laki nane kupoteza maisha yao. Hii ni kumbu kumbu yenye machungu makubwa
kwa maisha na utume wa Kanisa, lakini inawakumusha waamini na watu wote wenye
mapenzi mema hasa wale walioguswa na kutikiswa na mauaji ya kimbari kuanza
mchakato wa huruma, ili kuambata upendo wa Mungu unaoganga na kuponya machungu
ya ndani yanayomsibu mwanadamu!
Askofu Rukamba ameyasema haya kufuatia waraka wa kichungaji
uliotolewa na Baraza la Maaskofu Katoliki Rwanda kama sehemu ya hitimisho la
Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu kwa kuomba msamaha
kwa niaba ya Kanisa kutokana na baadhi ya watoto wake kushiriki katika mauaji
ya kimbari nchini humo! Maaskofu wanasema, lengo la waraka huu wa kichungaji ni
kusaidia mchakato wa uponyaji wa madonda ya vita ya wenyewe kwa wenyewe na
hatimaye, mauaji ya kimbari.
Maaskofu wanaomba msamaha kutokana na mauaji haya ya kimbari
ambayo kimsingi yalikwenda kinyume cha amri ya upendo kwa Mungu na jirani. Ni
mauaji ambayo yamefumbatwa katika ukabila usiokuwa na mvuto wala mashiko,
changamoto kwa sasa ni kujenga umoja na mshikamano wa familia ya Mungu nchini
Rwanda. Itakumbukwa kwamba, Baba Mtakatifu Francisko wakati wa maadhimisho ya
Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu alikazia kwa namna ya pekee, umuhimu
wa kukimbilia na kuambata msamaha na huruma ya Mungu kwa njia ya toba na
wongofu wa ndani.
Comments
Post a Comment