DESEMBA 9 RASMI SIKU YA KULIOMBEA TAIFA....
KUFUATIA
kutolewa kwa kibali kutoka kwa Baba Mtakatifu, Desemba 9 ya mwaka 2016 na ya
kila mwaka, ambayo ni kumbukumbu ya siku ya uhuru wa Tanganyika, imeidhinishwa kuwa ni siku maalum ya kufanya
Misa Takatifu ya kuliombea Taifa la Tanzania.
Hayo yameelezwa na Katibu Mkuu
wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Padri Raymond Saba, ambaye
ametoa rai kwa waamini nchini kutumia fursa hiyo kwa ajili ya kusali kujiombea
wenyewe na kuiombea Tanzania na viongozi wake.
“Kuanzia Desemba 9 ya mwaka huu
na kuendelea, tutaanza kufanya Ibada maalum ya kuliombea Taifa letu. Tutakuwa
na Misa Takatifu ambayo imeratibiwa rasmi kwa kibali cha Baba Mtakatifu, kwa
ajili ya kuliombea Taifa letu lililowekwa chini ya ulinzi wa Mama Bikira Maria.
Hivyo nitoe wito kwa waamini, tukutane makanisani tusali, kujiombea sisi
wenyewe na Taifa letu. Tuanze adhimisho hili kwa sala” ameeleza Padri Saba.
Akielezea sababu za kuchaguliwa
kwa Desemba 9 kuwa siku ya kuombea Taifa, siku ambayo ni kumbukumbu ya uhuru wa
Tanganyika, Padri Saba amesema kuwa mara baada ya Tanganyika kupata uhuru wake
mwaka 1961, Baba Mtakatifu Yohane XXIII aliandika sala kwa ajili ya kuliombea
Taifa la Tanzania na alilikabidhi Taifa
hilo chini ya ulinzi wa Bikira Maria.
“Na ikumbukwe kuwa mwaka 1984
Papa Yohane Paulo II alitoa hati maalum kwa ajili ya Kanisa la Tanzania, kwamba
linaweza siku hiyo ya Desemba 9, tunapofanya kumbukumbu ya uhuru wetu, tufanye
adhimisho kwa heshima ya Mama Maria ambaye amewekwa kuwa mlinzi wa Taifa letu”
amesema.
Aidha ameongeza kuwa kwa hati
hiyo ya mwaka 1984 Baba Mtakatifu ameipatia Tanzania uwezo na mamlaka ya kuwa
na Ibada maalum ya Misa Takatifu ya Masifu kwa ajili ya heshima ya Mama Bikira
Maria, mlinzi na msimamizi wa Taifa la Tanzania.
Kufuatia taarifa hiyo, Padri
Saba ametoa rai kwa wakristo wakatoliki, kila mara kumkimbilia Mama Maria ili
aweze kuilinda Tanzania na kuiepusha na laana na balaa zinazoweza kuikabili.
Pia amewaasa watanzania kutumia
fursa hiyo kuwaombea viongozi wa serikali, vyama na wa dini ili wadumu katika
kutenda haki na kumthamini kila mtu.
“Tuwaombee viongozi wetu wawe na hekima,
busara na upendo. Kila aliye kiongozi, awe wa serikali, vyama na dini, adumu
katika misingi ya haki inayojenga amani” ameongeza.
Comments
Post a Comment