WARAKA MZITO WA BABA ASKOFU SEVERINE NIWEMUGIZI KWA WATANZANIA HUU HAPA..
Heri ya Krismasi!
Tunaadhimisha
sherehe za kuzaliwa Bwana Yesu Kristo mwaka huu 2016 kukiwa na hisia na mitazamo
mbali mbali ya watu wa makundi tofauti katika jamii yetu, juu ya hali ya maisha
ya mtanzania leo. Hii ni hasa baada ya kusikia toka kwa watu mbali mbali
tathmini za hali halisi ilivyo mijini na vijijini. Licha ya tetemeko la ardhi
lililotikisa huku Kagera mwezi Septemba na njaa pia katika baadhi ya wilaya
mkoani Kagera, baadhi ya watumishi wa umma hasa waliozoea kufanya kazi kwa
mazoea na bila kuzingatia nidhamu na maadili ya utumishi wao wameishi kwa hati
hati wasijue kutumbuliwa kwao kutakuwa lini na tokea wapi! Wafanya biashara nao
biashara zao zimepiga miayo kwa sababu ya kutochanganya kama ilivyozoeleka huko
nyuma, wengi wanasema hali ni ngumu, pesa haikamatiki! Viongozi wa makanisa nasi
tumejikuta tukikimbizana na viongozi wa serikali kuulizana nao kama ubia wa
sera ya PPP (Public-Private-Partnership) bado unaishi au la. Milango yao na
masikio havikufunguliwa kwa urahisi. Mahospitali yetu yako taabani hasa kwa
suala la watumishi, karibu yaende ICU licha ya makubaliano mazuri baina ya
serikali, makanisa na wadau wengine binafsi katika huduma za afya yaliyopo
kwenye makaratasi.
Nimefika
kwa kinyozi wangu nikamuuliza: vipi hali? Akajibu kuwa hali ni ngumu sana,
waliozoea kuleta familia kunyoa kwake mara kwa mara hawaendi tena kwani hawana
pesa, karibu anafunga kazi hiyo; naye ameapa kura ikipigwa tena atafikiria mara
mbili nani wa kumpa kura yake. Upo mzaha sasa kuwa sote tuko tunaisoma namba
kwa jinsi nchi inavyoendeshwa kwa kasi, anayeshika usukani akiwaacha njiani
hata wa ndani wake! Wengine wanapumua kama vifaru waliojeruhiwa. Na mwandishi wa
habari mmoja ameniuliza nina neno gani la faraja kama mchungaji kwa wote hawa
Krismasi hii? Nikamjibu kuwa wasiwe na hofu, Yesu amekuja, ni Mungu pamoja
nasi. Wakiwa naye huyu basi mengine yote si kitu! Akachangamka kwa neno hilo
naye.
Mwandishi
wa habari mwingine akanichokoza akiuliza mimi naona changamoto gani nchini kwa
sasa ambazo Kristo amekuja kupambana nazo? Nimemjibu kuwa bila shaka zipo
nyingi duniani na hapa nchini kwetu. Zipo za kiuchumi, za kisiasa, za kijamii, na
za kidini. Mzunguko wa pesa umekuwa mgumu, mifuko ya wengi iko tupu. Walikuwapo
watu kadhaa waliozoea kuzipata kifisadi na kuzimwaga katika mzunguko. Kufungwa
kwa mifereji iliyosaidia kuzipata kumeathiri wengi. Hata mama Ntilie anaonja
kibano hicho! Kisiasa kuna aina fulani ya mnyauko au kupooza kwa shughuli za
kisiasa, hili mnalifahamu kwa mapana sababu zake; kijamii tunashuhudia kila
siku mapambano ya wafugaji na wakulima pande mbali mbali za nchi; kuna watu
kuporwa ardhi; ukatili wa kijinsia; shida za maji vijijini; ugumu wa malezi ya
watoto waitwao wa dijitali; watanzania wengi maskini kutokuwa na bima ya afya,
nk. Kidini, ni dini na makanisa yanayoahidi kuleta utajiri, kutenda miujiza,
kuponya magonjwa na kuondoa kero zote za maisha mara moja na kutoa burudani za
nyimbo za Injili ndizo zinazong’ara na kufuatwa na wengi, tofauti na makanisa
yale yanayokazia kuabudu kwa moyo (Mt 15:8; Lk 21:34; Yn 4:23; Efe 6:6; Kol
3:23), heri nane (Mt 5:3-12), kujitahidi kuingia mbinguni kupitia njia
nyembamba (Mt 7:3), kujikana, kubeba msalaba na kumfuata Bwana (Mt 16:24; Lk
9:23). Watu wengi wanataka njia pana na isiyo na shida au msalaba! Kwa changamoto
zote hizi Kristo aliyezaliwa ulimwenguni ndiye jibu! Mtu anaweza kuniuliza kwa
vipi? Ukweli ni kuwa kama wanadamu wakimsikiliza kwa makini Yesu na kwa makini
wakafuata ushauri wake changamoto zote zitapata majibu sahihi au suluhu ya
kudumu!
Kwetu
huku Ngara na kuelekea Biharamulo nimesema changamoto kubwa ni UHARIBIFU WA
MAZINGIRA. Hakuna aliye na huruma na sisi: mazingira yanaharibiwa kwa kasi ya
ajabu kwa kukata miti na kuchoma mkaa kwa namna ya kutisha mbele ya macho ya
viongozi wetu. Kisingizio ni kuwa hakuna nishati mbadala! Vyanzo vingi vya maji
vimekauka kutokana na hujuma hii ya kibinadamu; tuna ng’ombe wilayani Ngara
huenda wengi kuliko sehemu yoyote Tanzania ingawa eneo la wilaya ni dogo huenda
kuliko wilaya zote nchini. Hatuwezi kupona jangwa na mmomonyoko wa ardhi.
Tumelia na kupiga kelele lakini hakuna anayetuhurumia. Uharibifu umehalalishwa,
maana ulisikia wanaokamata ng’ombe kwenye hifadhi za Burigi wanasimamishwa
kazi! Barabara ninayopita nitake nisitake kama mchungaji kwenda kwenye parokia
zangu za Biharamulo inatisha kwa uharibifu. Magari makubwa yanaanguka
yakijaribu kupita pembeni mwa barabara kwa kukwepa kupita juu ya lami yenye
mashimo kama mapango. Barabara ya Nyakanazi-Lusahunga-Rusumo inatisha, ingawa
ni muhimu sana kwa uchumi wa nchi hii ukizingatia bidhaa za thamani kubwa zinazopitishwa
humo kwenda Burundi, Rwanda, DRC na hata Uganda! Mbaya zaidi sasa mazingira
yanachafuliwa kwa marundo ya chupa zilizovunjika, zikimwagwa pembeni mwa
barabara usiku na magari makubwa yasiyofahamika! Ukitaka naweza kukutumia picha
za hali hii ninayoizungumzia. Usalama wetu na mali zetu Ngara daima ni tete
hasa kutokana na kupakana na nchi jirani zenye migogoro ya ndani isiyoisha. Uumbaji
wa Mungu unalia, nasi tunalia, lakini machozi yetu ni kama ya samaki majini,
hakuna anayetusikia wala kutuhurumia. Sisi wafuasi wa Kristu tunabaki kusema tu
NJOO KWETU MASIHA utuokoe na uharibifu huu na hofu zetu.
Ni
matarajio yangu kuwa ujio wa Kristu utagusa mioyo ya wahusika wote, awazibue
masikio wasikie kilio, awafumbue macho waone, awape moyo wa huruma wauonee
huruma uumbaji wa Mungu ulioharibiwa sana; Neno lake liwachome sindano wahalifu
ili kutibu dhamiri zao; viongozi nao waone aibu kwa kukaa kimya au kuona
uharibifu unaotendeka kama vile ni mambo ya kawaida, au kama vile hakuna la
kufanya ili kunusuru mazingira yetu. Kilichofanyika kwa misitu tokea Nyakahura
ngazi Saba, Busiri hadi Lusahunga wilayani Biharamulo ni
maafa kwa mazingira! Sote tunashuhudia mabadiliko ya tabia nchi na madhara yake
kwa hali ya hewa na bado tunawachekea tu waharibifu wa mazingira!
Paulo
Mtume kupitia Waraka kwa Tito (2:11-14) ametuambia katika mkesha wa
Noeli kuwa neema ya Mungu iwaokoayo wanadamu imefunuliwa kwetu. Yesu Kristo
ndiye neema hiyo. Amekuja kutufundisha kuukataa uovu na tamaa za kidunia, ili
tuishi kwa kiasi, haki na usawa. Kuharibu mazingira kwa kisingizio chochote
kile ni uovu usiopaswa kukubalika wala kuvumilika. Kuna wenzetu ni wakulima
wazuri sana wa mpunga, lakini ni adui wa miti ati kwa sababu miti inawapokea
ndege wanaokula mazao yao. Shida ni kuwa wao ni wepesi wa kuhama inapotokea
maeneo kuharibika kwa sababu ya kazi za kibinadamu zinazoleta ukame. Wanahama
na kwenda kwingineko na kuendelea na uharibifu ule ule! Nawasihi wabadilike na
kuwa rafiki wa mazingira. Wajue kama wao wanavyohitaji kuhifadhiwa maisha yao,
vivyo hivyo mazingira yanahitaji kuhifadhiwa ili nayo yamhifadhi binadamu. Uumbaji
wa Mungu nao unahitaji ukombozi. Paulo mtume analieleza hili vizuri akisema “kwa
maana viumbe vyote pia vinatazamia kwa shauku nyingi kufunuliwa kwa wana wa
Mungu; kwa maana viumbe vyote pia
vilitiishwa chini ya ubatili…viumbe
vyenyewe navyo vitawekwa huru na kutolewa katika utumwa wa uharibifu” (Rum
8:19-21). Tumefunga mwaka wa Yubilei ya huruma ya Mungu tarehe 20 mwezi Novemba
, lakini sasa ni fursa ya kuendelea kudhihirisha upendo na huruma kwa watu na mazingira
yetu pia.
Emmanueli,
Mungu pamoja nasi atubadilishe mioyo yetu itake kutenda mema daima. Yesu Kristu
ni mwanga ulioingia ulimwenguni kufukuza giza. Hata jua linapotua yeye anabaki
akiangaza akili na mioyo. Ndiyo maana yeye ndiye tumaini pekee ulimwengu unaweza
kutegemea. Licha ya changamoto nyingi zinazoweza kumtatiza mwanadamu, akiwa na
imani katika Kristo Yesu anaweza kutembea mbele akiwa na matumaini kwamba
hatimaye atashinda yote magumu. Kristo amekuja ili atushike mkono na tutembee
kumwelekea Mungu atoaye uzima wa milele mwisho wa safari. Ukidumu mikononi
mwake Yesu una uhakika wa kufika kwa Mungu. Hii ni hata kwa asiye Mkristo.
Mfano mzuri ni kiongozi mkubwa wa India Mahatma Gandhi muumini wa dini ya
Kihindu aliyewahi kusema kwamba “Yesu Kristo ni mmoja wa walimu wakubwa
binadamu amewahi kupata”.
Gandhi
alimtambua Yesu kuwa ni mwana wa Mungu katika maana kuwa ni katika maisha yake
Yesu kuna ufunguo wa ukaribu wake na Mungu, na kwamba Yesu alieleza roho na
mapenzi ya Mungu kuliko mtu mwingine yeyote angeweza! Alikiri kuwa Yesu
hakuhubiri dini mpya bali maisha mapya, akiwaalika watu kutubu. Gandhi alikiri
kuwa Yesu alileta sheria mpya: “Amri yangu ndiyo hii, mpendane kama
nilivyowapenda ninyi” (Yn 15:12). Pia alikiri kuwa Kristo alimpa funzo kubwa
kwamba ukweli ndiyo jambo la msingi la kwanza kutafuta maishani: “tena
mtaifahamu kweli, nayo kweli itawaweka huru” (Yn 8:32). Lakini pia alimfunza
kujitoa bila kujibakiza pasipo kutegemea kurudishiwa chochote. Haya ni mambo
ambayo mtu yeyote bila kujali dini au kanisa ujifunze kwa Yesu Kristo. Kwako
wewe Mkristo naamini shuhuda huyu asiye Mkristo lakini shabiki wake Kristo
anakufumbua macho zaidi utambue ni nani uliye naye maishani. Hivyo imarisha
kumpenda zaidi, kumthamini na kuzingatia atakayokufundisha mtoto Yesu.
Kuzaliwa
kwa Kristo kuna maana gani kwangu na kwako leo? Kuzaliwa kwa Yesu kuna maana
kuwa: 1)Uzazi wa Yesu umetimiza maaguzi ya manabii: kwamba ulikuwa mpango wa
Mungu, hivyo uzazi wake ulikuwa wa kimungu; 2)Mrithi wa kiti cha Ufalme wa
Daudi amezaliwa (Lk 1:32-33); 3)Furaha imeingia duniani (Lk 2:14,20,25-32):
wachungaji walifurahi; mzee Simeoni naye alifurahi kuona wokovu umefika;
4)Mwokozi amefika atakayelipa fidia ya wokovu wa binadamu (Mk 10:45; Lk 1:21;
19:1-10); 5)Shetani atashindwa (Mwa 3:15; 1 Yoh 3:8; Ebr 2:14). Matokeo ya
kushindwa shetani ni: 6) Amani inaweza kuingia mioyoni mwetu (Isa 9:6-7; Lk
2:14; Kol 2:19-20); 7)Njia ya kuingia mbinguni imewekwa wazi (Yn 3:16, kila
amwaminiye hatapotea; 14:5-6, Yeye ndiye njia, ukweli na uzima). 8)Hatimaye
Yesu atarudi tena katika utukufu i)kutukaribisha kwake (Yn 14); ii)kufufua wafu
(1 Thes 4:13-18); iii)kubatilisha mauti (1 Kor 15:25-26); iv)kukusanya wateule
wake (Mt 24:31); v)kuhukumu ulimwengu (Mt 25:31-46) na vi)kuwatuza waaminifu
wake: kila mtu kulipwa kadri ya matendo yake (Mt 16:27). Nikijua maana hii ya
kuzaliwa Yesu Kristo napata ujasiri wa kumpokea na kuwa tayari kumfuata,
nikiomba anishike mkono katika safari ya kwenda kwa Baba. Najawa furaha, amani
na nguvu ya kuishi kwa matumaini. Nakusihi nawe usipoteze fursa hii.
Amani
ya Bwana iwe nawe leo na daima. Amina.
+Severine
NIWEMUGIZI
Askofu
wa Jimbo la Rulenge-Ngara
Comments
Post a Comment