ASKOFU SHAO: URITHI PEKEE WA MTOTO NI ELIMU


 


ASKOFU wa Jimbo Katoliki Zanzibar Augustino Shao amewataka wazazi kuwekeza katika sekta ya elimu kwa kuwasomesha watoto wao katika shule ambazo zinatoa elimu bora ili waweze kumudu ushindani wa soko la ajira.

Amesema urithi pekee kwa mtoto ni elimu hivyo ni jukumu la kila mzazi kuhakikisha mtoto wake anapata elimu bora ambayo itamwezesha kukabiliana na changamoto za utandawazi zinazojitokeza siku hadi siku.
Askofu  Shao ameyasema hayo kwenye Misa Takatifu  ya kutoa Daraja Takatifu la ushemasi kwa Fratel Abeil Ignus Ndomba iliyofanyika katika Parokia ya Wete  Pemba.
Amesema kutokana na kutambua umuhimu wa elimu katika maendeleo ya nchi na wananchi wake ,  Kanisa litaendelea kuiimarisha skuli yake iliyoko Tomondo Unguja ili iweze kutoa elimu bora kuanzia ngazi ya msingi hadi sekondari .
Amesema shule hiyo imekuwa ikitoa wanafunzi bora kwani ina Vifaa vya kutosha , mazingira bora ya kufundishia, walimu bora na wanaoingia kazini kwa wakati .
“Ni lazima kila mzazi kupima ubora wa elimu wanayopewa watoto wao  na kuacha kuridhika na elimu inayotolewa bure kwani inakabiliwa na changamoto mbali mbali ”amesema .
Aidha ameeleza kuwa shule inayomilikiwa na Kanisa hilo ya Tomondo imejipatia umaarufu kwani imezingatia viwango na idadi ya wanafunzi katika darasa moja , tofauti na shule zinazotoa elimu bure ambazo zinakuwa na msongamano mkubwa  wa wanafunzi katika darasa moja.
Naye mkurugenzi wa Miito jimboni humo Padri John   Mfoi amewataka wazazi kusimamia pamoja na kufuatilia maendeleo ya watoto wao ili kujua mwenendo wao na kusaidia kutatua changamoto  za kielimu zinazowakabili.
Amesema elimu ndiyo njia pekee inayoweza kumkomboa mwananchi kutoka katika wimbi la umaskini wa kipato , hivyo ni jukumu lao kuhakikisha wanajenga utamaduni wa kuwa karibu na walimu , kamati ya shule na wadau wengine wa elimu .
“Ni vyema wazazi na walezi kujenga utamaduni wa kufuatilia maendeleo ya watoto wao kwani elimu ndiyo ambayo inaweza kumkomboa mwananchi kutoka katika wimbi la umaskini,”alieleza.

Katika nasaha zake , paroko wa Parokia ya Wete , Padri Beatusi Babu amemtaka Shemasi Abeil kufanya kazi kwa uhuru na kuyakemea matendo maovu bila ya woga ili aweze kuitumikia vyema jamii.

Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

MJUE MTAKATIFU MARIA GORETTI