UFAFANUZI WA ADHABU YA UTOAJI MIMBA HUU HAPA

BAADA YA Papa Fransisko kutoa barua ya kitume ‘Misericordia et misera,’ yaani Huruma na amani, ameeleza kuwapa mamlaka mapadri waungamishi wote kuondoa adhabu na kusamehe dhambi ya kutoa mimba.
 Kufuatia utaratibu huo mpya, baadhi ya waamini wamepokea  taarifa hiyo kwa hisia tofauti huku baadhi wakiona kuwa Kanisa linalegeza baadhi ya sheria zake hivyo kusababisha dhambi ya utoaji mimba kuongezeka duniani.
Mtaalamu wa Sheria za Kanisa Askofu Severine Niwe-Mugizi ambaye ni Askofu wa Jimbo Katoliki Rulenge-Ngara ameeleza kuwa, tafsiri ya sheria hiyo ni Kanisa kupeleka Huruma ya Mungu karibu na waamini wake.
“Papa kabla hajafanya maamuzi ya jambo lolote anafanya tafakari ya kina. Anasali na kuomba Roho amuangazie afanye maamuzi sahihi kwa faida ya watu wake.
Katika Kanisa Katoliki kuna sheria zimewekwa kwa ajili ya nidhamu na nyingine zimewekwa kwa ajili ya kulinda imani.
Japokuwa tuna sheria hizi lakini hakuna dhambi inayomshinda Mungu. Ingekuwa leo Yesu amesimama halafu akaja mtu kumuomba msamaha kwa kutoa mimba, je, Kristo asingemsamehe?
Hakika angesamehe kwani hakuna dhambi kubwa inayomshinda Mungu. Kama hakuna dhambi inayomshinda Mungu kwanini Padri asiungamishe? Padi hasimami kama padri katika sanduku la maungamo, bali anamwakilisha Kristo mwenye mamlaka ya kusamehe dhambi.
Kanisa lisibaki kuwa mahakama ya kumhukumu mtu aliyetoa mimba na kushangilia jinsi anavyoteseka na dhambi hiyo bila kutubu? Kanisa ni mama. Waamini waone mahali salama pa kukimbilia katika madhaifu na unyonge wao. Liwakumbatie wote na kutoa msamaha kwani lengo moja la Kanisa ni kufikisha watu mbinguni si motoni.” Ameeleza Askofu Niwe-Mugizi.

Aidha ameeleza kuwa, Papa Fransisko anataka uwajibikaji wa mapadri katika kusamehe dhambi kwani wao ni wawakilishi wa Kristo. Anamtaka Padri awajibike akiwa anamtazama Kristo mwenye huruma.
“Hata kama mapadri wangeambiwa wasiungamishe mnafikiri hiyo dhambi haitatendeka kwa sababu lazima mtu akamtafute Askofu? Tena kijiografia katika jimbo muamini kumtafuta Askofu pengine inaweza kuwa changamoto kwani Askofu katika jimbo ni mmoja tu, lakini mapadri wapo karibu na waamini hivyo ni rahisi muamini akapata huruma ya Mungu kupitia kwa padri kuliko kuteseka na dhambi hiyo milele na kuacha kupokea sakramenti mbalimbali hususani ya Ekaristi Takatifu,” amefafanua.
Sheria hiyo haijahalalishwa wala kuondolewa kwani ilikuwa ni sheria ya Kanisa inayoelekeza dhambi ya kutoa mimba kuwa kuondolewa kwake ni kwa mamlaka fulani.
Hivyo kama zilivyo dhambi nyingine ni sawa muamini akaenda kwa padri akaungama kwani Kristo Mchungaji mwema anawapokea wote wanaorudi kwake hata kama walikuwa wamepotea. Jambo la msingi ni kutubu na kuacha dhambi.
Kanuni sheria za Kanisa, zinaitambua dhambi ya utoaji mimba kuwa ni moja ya makosa makubwa dhidi ya uhai wa mwanadamu, hasa katika hali ya unyonge wake. Kwa sababu hiyo adhabu iliyopo ni kwa wahusika kujitenga na Kanisa, hivyo kujizuia kupokea Sakramenti yeyote mpaka adhabu hiyo iondolewe. Adhabu ya namna hiyo katika Kanisa, ni Askofu au padri aliyeteuliwa na Askofu ndiye mwenye mamlaka wa kuiondoa adhabu hiyo, siyo katika taratibu za mahakama kikanisa, bali katika Sakramenti ya kitubio. Mamlaka ya kuitoa adhabu hiyo kimahakama, nje ya Sakramenti ya Upatanisho, ni mahakama kuu ya Kanisa.
Tangu mwaka 1983 adhabu hiyo ilipowekwa na sheria kanuni za Kanisa, kumekuwa na magumu mengi na mahangaiko kwa upande mwingine, pale ambapo inakuwa vigumu kumpata Askofu kwa wakati au mapadri wachache walioruhusiwa kutoa adhabu hiyo. Hali kama hii ilisababisha waamini waliojutia dhambi hiyo, kujikuta wakikaa muda mrefu kabla ya kupata kuondolewa adhabu hiyo.
Kumbe Mama Kanisa sasa anawapatia mamlaka kisheria mapadri wote waungamishaji, kuweza kuondoa adhabu hiyo, na kisha kumuungamisha mhusika. Ieleweke vizuri hapa kuwa, kuna tofauti kati ya dhambi na maungamo, kosa na adhabu.



Comments

Post a Comment

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

MJUE MTAKATIFU MARIA GORETTI