Jitaabisheni kutafuta wokovu wa roho zenu!
Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la
Costantinopoli anasema, Mungu ni upendo na mwingi wa huruma na msamaha mambo
ambayo yamefumbatwa kwa namna ya pekee katika Wosia wa Kitume wa Baba Mtakatifu
Francisko “Amoris laetitia” yaani “Furaha ya upendo ndani ya familia”, upendo
unaoshuhudiwa katika maisha na utume wa Baba Mtakatifu Francisko kwa kuwajali
maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii kutokana na sababu
mbali mbali za maisha.
Ni ushuhuda ambao ameonesha kwa kujali na kuthamini utu na
heshima ya wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta usalama, hifadhi na maisha bora
Barani Ulaya kama ilivyojionesha wakati wa safari yake kwenye Visiwa vya Lesvo,
nchini Ugiriki. Hawa ni watu wanaokufa maji kila kukicha kwenye bahari ya
Mediterannia, kiasi kwamba, sauti yak ilio chao kwa sasa ni kero na usumbufu
kwa Jumuiya ya Kimataifa! Lakini hawa ni watu walioumbwa kwa sura na mfano wa
Mungu wanapaswa kuheshimiwa na kusaidiwa kwa hali na mali kama binadamu!
Patriaki Bartolomeo wa kwanza anayasema yote haya kwa kufanya
tafakari ya kina mintarafu Wosia wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko “Furaha
ya upendo ndani ya familia” wosia ambao kimsingi unafumbata tunu msingi za
Injili ya ndoa na familia. Wakati viongozi hawa wawili walipotembelea kambi ya
wakimbizi na wahamiaji huko Ugiriki, walikutana na uso za huzuni kutoka kwenye
familia ambazo zimelazimika kuzikimbia nchi zao kutokana na vita, kinzani na
dhuluma mbali mbali changamoto kwa viongozi wa Jumuiya kuhakikisha kwamba,
wanaunganisha uongozi na huduma kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wao na wala
si vinginevyo!
Huduma na uongozi pia ni changamoto kwa waamini ili kuhakikisha
kwamba, wanakuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya upendo kwa jirani
zao. Baba Mtakatifu Francisko katika Wosia wake wa kitume, Furaha ya upendo
ndani ya familia anapembua kwa kina na mapana umuhimu wa upendo katika maisha
na utume wa wanandoa na familia. Anagusia changamoto zinazowakabili wanandoa
katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia; malezi na
makuzi ya watoto; talaka na changamoto ya ndoa za watu wa jinsia moja. Haya ni
mambo yanayogusa undani wa utakatifu wa maisha ya mwanadamu na Injili ya uhai
dhidi ya utamaduni wa kifo.
Patriaki Bartolomeo wa kwanza anasema, katika miezi ya hivi
karibuni, Wosia huu wa kitume umechambuliwa na kupepetwa kama mpunga ili
kuangalia Mafundisho tanzu ya Kanisa, mchango wake katika sera na mikakati ya
shughuli za kichungaji; mabadiliko yaliyojitokeza katika sheria za Kanisa na
uelewa wake kwa wakati huu. Wakati huu, Mama Kanisa anapojiandaa kwa ajili ya
kuadhimisha Fumbo la Umwilisho yaani Siku kuu ya Noeli, Neno wa Mungu
alipofanyika mwili na kukaa kati ya watu wake katika mambo yote akawa sawa na
binadamu isipokuwa hakutenda dhambi, ni wakati wa kutambua na kuenzi huruma na
upendo wa Mungu katika maisha ya mwanadamu na wala si kuangalia tu kanuni
maadili na Sheria za Kanisa ambazo zimetungwa na binadamu wenyewe!
Ni kweli ulimwengu mamboleo una changamoto na matatizo yake
mintarafu maisha ya ndoa na familia, lakini waamini wakumbuke kwamba, Mwenyezi
Mungu ni chemchemi ya: huruma, upendo na maisha! Mambo msingi yanayopewa
kipaumbele cha pekee na Baba Mtakatifu Francisko katika Wosia wake wa kitume,
“Furaha ya upendo ndani ya familia”. Anafafanua kwa kina na mapana tasaufi ya
maisha ya ndoa na familia katika ukweli na uwazi kwa kujikita katika huruma ya
Mungu inayoganga na kuponya majeraha ya maisha ya mwanadamu. Kila mwanadamu
anapendwa na kuthaminiwa na Mungu, kumbe, hakuna sababu msingi ya kumtenga mtu
na huruma pamoja na upendo wa Mungu anakaza kusema Patriaki Bartolomeo wa
kwanza.
Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu
anaendelea kuchambua Patriaki Bartolomeo wa kwanza, Baba Mtakatifu Francisko
amebahatika kukutana na kuzungumza na familia za wakimbizi na wahamiaji,
mwaliko kwa waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuwa kweli ni vyombo
na mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu. Papa Francisko anawaalika watu
kujifunga kibwebwe ili kuwajibika kikamilifu kwa ajili ya wokovu wa roho zao
wenyewe kwa kujikita katika Amri za Mungu, kanuni maadili na utu wema mambo
yanayofumbatwa katika tasaufi ya maisha ya ndoa na familia.
Patriaki Bartolomeo anahitimisha tafakari yake kuhusu Wosia wa
Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko, Furaha ya upendo ndani ya familia kwa
kusema udhaifu wa kibinadamu, usiwe ni kikwazo cha kumwilisha utimilifu wa
huruma na umoja unaobubujika kutoka katika Fumbo la Utatu Mtakatifu.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
Comments
Post a Comment