TAFAKARI YA MPAGAZE: Usipofanya lolote utaajiriwa na shetani






“Lakini yule aliyekabidhiwa talanta moja akaja, akasema, Bwana, najua wewe ni mtu mgumu; wewe huvuna pale ambapo hukupanda, na kukusanya pale ambapo hukutawanya. Niliogopa, nikaificha fedha yako katika ardhi. Chukua basi mali yako. Bwana wake akamwambia, wewe ni mtumishi mwovu na mvivu!” Usipofanya lolote utavuna matusi na fedheha. Kutofanya lolote ni uovu. Kukaa bila kufanya lolote unaweza kuajiriwa na shetani. Kutofanya lolote ni dhambi. Kutofanya lolote ni uasi. Kutofanya lolote ni uvivu. Kukaa kimya na wakati kuna shida mahali fulani ni dhambi ya kutofanya lolote. “Yeye aliye na uwezo wa kutenda pale ambapo haki haitendeki, lakini anakaa kando kiuvivu ana kosa sawa na aliyemchoma jirani yake kwa kisu”. Si kwamba mambo ni magumu ndio maana hatuthubutu kufanya kitu. Ni kwa sababu hatuthubutu kufanya kitu ndio maana mambo ni magumu,” alisema Seneca. Kutothubutu au kutojaribu ni kosa. Kwa kujaribu mara nyingi, tumbili hujifunza kuruka kutoka mtini.

 “Mtu ambaye hajiweki katika hali ya kujaribu, hafanyi lolote, hana chochote, na si chochote na atakuwa si chochote. Anaweza kukwepa mateso na huzuni, lakini hawezi kujifunza, kubadilika na kukua alisema Leo F. Buscaglia. Kama kila mtu angejitahidi kufanya lolote zuri dunia ingekuwa mahali pazuri pa kuishi. Badala yake tumekuwa watu wa kuzungumza na kupanga mambo kibao pasi pokutenda. Mvulana alimwambia baba yake, “Baba palikuwepo na vyura watatu wamekaa kwenye tawi la mti ambalo lilikuwa juu ya bwawa la kuogolea na chura mmoja aliamua kuruka kuingia kwenye bwawa, ni vyura wangapi waliobaki kwenye tawi? Baba yake alijibu, “Wawili.” “Hapana, kuna vyura watatu na mmoja ameamua kuruka, wangapi wamebaki?” Mtoto alizidi kumuuliza baba. Baba alijibu, “Nimepata jibu sasa, kama mmoja anaamua kuruka na wengine wataruka. Kumbe hakuna anayebaki kwenye tawi!” Mvulana alisema, “Hapana baba, jibu ni watatu. Chura aliamua tu kuruka. Hakuruka!” Uamuzi bila kutenda ni jambo la kawaida. Tuko vizuri katika kufanya maamuzi. Lakini mara nyingi tunaamua tu, na miezi baadaye tunakuwa bado kwenye tawi, bila kufanya lolote. Toka kwenye tawi na fanya kitu, epuka laana.

Ukikaa bila kufanya lolote basi shetani atakupa tu la kufanya na mwisho wa siku utajuta kuzaliwa. Ngoja nikupe mfano mmoja wa wanandoa waliopewa kazi na mchawi. Ilikuwa hivi, jamaa alienda kwa mchawi kutafuta utajiri. Yule mchawi alimwambia aende na mke wake. Alienda na mke wake. Mchawi alisema, “Mwanaume aingie kwanza kwenye nyumba.” Alipoingia kwenye nyumba mchawi alifunga mlango na kuanza kumpaka dawa.” Alimweka chale kwa kutumia wembe. Mwishoni alimpaka pilipili ambayo ilimfanya apige mayowe sababu ya uchungu. Alimwambia atoke nje mke wake aingie. Mke wake alipoingia mchawi alifunga mlango. Alichokifanya mchawi ni kumbaka huyo mwanamke. Mwanamke alipiga kelele. Mme wake alifikiri sasa anapakwa dawa yenye pilipili kama alivyopakwa yeye. Hivyo alimwambia mke wake, “Vumilia, tulia. Mke wake alifikiri kuwa mme wake ametoa kibali abakwe kama sehemu ya dawa ya utajiri.” Hiyo ndiyo faida ya kukaa bila kufanya lolote maana shetani anakupa la kufanya. 

 Na: Denis Mpagaze

Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

MJUE MTAKATIFU MARIA GORETTI