Wasomi watakiwa kuwa tiba ya ufisadi nchini
NAIBU Katibu Mkuu, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Simon
Msanjila amewaasa wahitimu wa Chuo Kikuu Katoliki Ruaha (RUCO) kuwa mabalozi
wazuri wa chuo hicho kwa kupambana na kukemea rushwa na ufisadi.
Prof Msanjila
ameyasema hayo mwanzoni mwa juma wakati wa mahafali ya tisa ya chuo hicho
yaliyofanyika kwenye viwanja vya chuo ambapo jumla ya wahitimu 1,583
wametunukiwa vyeti kuanzia ngazi ya astashahada, stashahada, shahada, shahada
za uzamili na uzamivu katika taaluma mbalimbali.
Amesema kwamba
wahitimu hao wanapaswa kuishi kwa kufuata maadili ya taaluma zao, kama ni
mwalimu akawe ni mwalimu wa mfano mwema na mwanasheria akawe mwanasheria wa
kweli.
“Tunafundishwa
katika kitabu cha Mithali 4:6 kwamba, Usimuache Elimu, naye atakuhifadhi,
umpende Elimu nae atakulinda,.Kwa vile elimu ni mwangaza na nuru kama ambavyo
tunavyofundishwa kwamba pasipo na nuru kiza hutawala. Mkajikinge na vishawishi
vinavyoweza kuwasababisha kupata maambukizi ya Ukimwi, mkazuie, kupambana na
kukemea rushwa na ufisadi na mkawe mabalozi wazuri wa chuo kikuu cha Katoliki
Ruaha,” ameasa.
Aidha amewataka
wahitimu hao kutobweteka na kuridhika na kiwango cha elimu ambayo wameipata
kwani dunia ya sasa ni ya ushindani mkubwa, wajenge dhana ya kutaka
kujiendeleza zaidi kwani elimu haina mwisho.
“Na kwa kusema kweli
Astashahada, Stashahada na shahada mtakazopewa ni changamoto katika kuendelea
kujifunza daima, msibweteke na mafanikio ya leo, mkumbuke kwamba ndani na nje
ya RUCU kuna fursa za kujiendeleza hata kufikia Shahada za Uzamili na Uzamivu
katika taaluma zenu mbalimbali”.
Prof. Msanjila
amesema serikali inavitaka vyuo vikuu vijikite na kujidhatiti kwenye fani na
maeneo ambazo vina uhakika vitakuwa bora kuliko vingine.
Amevitaka vyuo vikuu
viache tabia ya kujijenga kwa kuangalia tu fani au programu ambazo vitapata
wanafunzi wengi ili vipate fedha nyingi kupitia ada.
“Uhakiki wa vyuo
vyote uliofanyika siku za karibuni utatoa picha kwa kila chuo kama kinazingatia
ubora wa elimu na kama kina uwezo wa kudahili wanafunzi waliopo chuoni,
ninawashauri RUCU mjipime kuwa umahiri wenu upo kwenye fani zipi na mjiimarishe
huko badala ya kutaka kutanuka kwa kuchukua kila kitu, msijaribu kuwa
University of everything.” Amesema Prof. Msanjila na kuongeza kuwa “ Wakati
RUCU ikijipima umahiri tambulishi wenu kama chuo (University Niche) mzingatie
pia mtazamo wa serikali ya awamu ya tano inayolenga kujenga uchumi wa viwanda,
hivyo wito wangu kwa chuo, katika program zake zitolewazo chuoni, haina budi
kuwa na uelekeo huo.
Kabla ya kuanza kwa
mahafali hayo, kulikuwa na ibada ya Misa Takatifu ambayo imeongozwa na Askofu
wa Jimbo Katoliki Iringa Mhashamu Tarcisius Ngalalekumtwa na Homilia imetolewa
na Askofu Alfred Maluma wa Jimbo Katoliki Njombe huku akiwataka wahitimu hao
kutumia talanta zao vizuri.
Askofu Maluma
amesema wahitimu hao wanapaswa kuwa na ndoto na watamani kufanya vitu vionekane
na watambue kwamba ujana wao ni mtaji wa kuanzia pale walipo ili walete faida
kwao na kwa jamii nzima.
“Nyie si watalanta
moja hapana, nyie ni wa talanta 2 na tano, fanyieni kazi yale yote mliyoyapata
hapa, mtazaa matunda, mkilinda utu wenu mtaishi vizuri,” Amesma Askofu Maluma
na kusisitiza kuwa “elimu, ujuzi na yote mliyopata mlipokuwa hapa RUCO iwafae
kwenu wenyewe na muwe vyombo vinavyofaa kwa jamii na ulimwengu mzima.”
Akitoa neno kwenye
mahafali hayo Askofu Ngalalekumtwa amewataka wahitimu hao kutumia muda wao
vizuri chuoni hapo “mtambue ya kwamba elimu ina gharama kubwa na kama mmepata
bahati ya kuwa hapa someni kwa bidii na siyo kufanya mambo yasiyofaa.”
Comments
Post a Comment