Kanisa Katoliki latathmini hali ya uchumi nchini
Wachumi waombwa kutoa takwimu zenye uhalisia
Wadau wataka uchumi unaojali masikini na mazingira
IMEELEZWA
kuwa ukuaji wa uchumi usiojali uhifadhi wa mazingira, maliasili na utu wa kila
mwananchi ni pigo ambalo haliakisi uhalisia wa ukuaji huo.
Hayo yamebainishwa na wadau wa
masuala ya uchumi na mazingira katika Kongamano la kitaaluma la siku mbili,
lililojadili juu ‘Mchango wa mafundisho jamii ya Kanisa Katoliki katika kukua
kwa uchumi na maendeleo ya jamii’ lililofanyika katika Chuo Kikuu Kishiriki cha
Stella Maris Mtwara.
Akitoa mada katika Kongamano
hilo Askofu Gervas Nyaisonga wa Jimbo Katoliki Mpanda, amesema kuwa kukua kwa
uchumi ni lazima kuendane na ari ya kutunza mazingira, matumizi ya rasilimali
yenye kujali na kuheshimu mpango wa Mungu wa uumbaji na moyo wa kugawana sawa
mapato yatokanayo na rasilimali hizo.
“Ili kuwa na uchumi wenye tija
na maendeleo endelevu, ni lazima tutoke kwenye dhana ya kusema ‘nini ninataka’
na kujikita katika dhana ya ‘nini Mungu anataka’. Vinginevyo tujiandae kulipa
deni la kuharibu Ekolojia, na kusababisha utu wa mwanadamu ukose maana”
ameeleza Askofu Nyaisonga, ambaye kitaaluma ni mwana Jiografia.

“Kama wakristo, tumeipokea
dunia kama Sakramenti ya Ushirika, ambayo tunapaswa kushirikishwa na Mungu na
vizazi vijavyo. Hivyo, tunapaswa kubadili mtazamo wetu dhidi ya mazingira.
Tuyaone mazingira kama kaka au dada yetu. Uzuri wa mazingira humdhihirisha
aliyeyaumba” ameeleza.
Kwa upande wake mtaalamu wa
uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino Mwanza (SAUT), ameeleza kuwa
takwimu za kukua kwa uchumi hazina uhalisia kwa kuwa hazijumuishi uharibifu wa
hali ya juu unaofanywa na shughuli za uzalishaji.
Ameongeza kuwa ukuaji wa uchumi
unaowaacha nyuma maskini na wanawake hauna uhalisia, na hivyo kuwataka wanaotoa
takwimu za kukua kwa uchumi kujumuisha athari za mazingira zinazoletwa na kukua
kwa uchumi.
“Uchumi wetu unakua sana kwa
kuwa kiwango cha uharibifu kiko juu pia. Uchumi unakua kwa kasi kwa sababu
tunatumia mno rasilimali zetu. Lakini tumewahi kujiuliza gharama za uharibifu
tunaoufanya kwenye mazingira yetu? Tumejiuliza gharama za matatizo
tunayoyazalisha kwa watu wengi ambao wengi wao ni maskini? Kama hatuangalii
gharama hizi basi kipimo chetu cha kukua kwa uchumi siyo sahihi” ameeleza.
Ameongeza kuwa kukua kwa uchumi
hakuzingatii mahitaji ya vizazi vijavyo, na kuonya kuwa uharibifu wa rasilimali
utaleta hatari na balaa. Pia ametoa angalizo kuwa kazi ya mwanadamu ni kuwa
waangalizi wa rasilimali kwa ajili ya manufaa ya vizazi vingine.
Akitoa mchango wake katika
kongamano hilo mdau wa mazingira na Balozi Mstaafu John Kambona amesema kuwa elimu
ya utunzaji wa mazingira inapaswa kuwekwa kwenye mtaala wa elimu, ili iwe
sehemu ya utamaduni wa mtanzania.
“Somo hili likiwekwa kwenye mtaala litawainua
watoto wetu kuliko kuwafundisha ‘pie’. Pia liwekwe kwenye sala ili itukumbushe
kuwa kukata miti ni dhambi” amesema.
Comments
Post a Comment