Ufalme wa Mungu uko kati yenu! Kiini cha Habari Njema ya furaha!

Tubuni, kwa maana Ufalme wa Mungu umekaribia ni mwaliko wa Yohane Mbatizaji, maneno ambayo pia yalitumiwa na Yesu alipokuwa anaanza utume wake huko Galilaya. Ni ujumbe ambao ulichukuliwa pia na Mitume wa Yesu kama chemchemi ya maisha yao ya kimissionari. Yohane Mbatizaji anatambulishwa na Mwinjili Mathayo kama mtangulizi anayemwandalia Yesu njia, kazi itakayoendelezwa na Mitume wa Yesu, yaani utangazaji na ushuhuda wa furaha ya Injili inayojikita katika uwepo wa Ufalme wa Mungu kati ya watu wake. Huu ndio ujumbe mahususi wa utume wa Kikristo.
Haya yamesemwa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, Jumapili ya pili ya Kipindi cha Majilio, tarehe 4 Desemba 2016 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Wamissionari wa nyakati zote wanatumwa kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu kati ya watu wa mataifa, sanjari na kuandaa njia ili Kristo Yesu aweze kukutana na watu wake. Ufalme wa Mungu au Ufalme wa mbinguni unajikita katika maisha ya uzima wa milele. Lakini, Yohane mbatizaji anawatangazia watu kwamba, Ufalme wa Mungu uko uko katika yao na unaonesha ukuu wake katika uhalisia wa maisha ya watu kila siku, hasa pale unapopokelewa kwa imani na unyenyekevu, unakuwa ni chemchemi ya upendo, furaha na amani!
Toba na wongofu wa ndani ni sharti muhimu la kuingia na kushiriki katika mchakato wa ujenzi wa Ufalme wa Mungu, changamoto inayopaswa kufanyiwa kazi kila siku ya maisha ili kutokumezwa na malimwengu. Hii ndiyo tamaa ya mali na uchu wa madaraka kiasi hata cha kuwadhalilisha wanyonge; ni hali ya kupenda anasa kupita kiasi. Badala yake, waamini wanaalikwa kwa namna ya pekee kabisa kumwandalia njia Kristo Yesu anayekuja kati yao ili kuwakirimia furaha bila ya kuwaondolea uhuru wao.
Kwa kuzaliwa kwa Yesu Kristo Mkombozi wa dunia huko mjini Bethlehemu, kunamwezesha Mwenyezi Mungu kuchukua nafasi na kukaa kati ya watu wake, ili kuwakomboa kutoka katika ubinafsi, dhambi, mauti na rushwa mambo ambayo yanakuzwa na kuendelezwa na Shetani anayewataka watu kutafuta ufanisi wa mambo yao kwa udi na uvumba; kutafuta madaraka kwa nguvu zote, hata kiasi cha kuwakanyaga maskini na wanyonge bila kuangalia makunyanzi yao; ni uchu wa mali pamoja na kutafuta anasa za kila aina kwa gharama yoyote ile!
Baba Mtakatifu anakaza kusema, Noeli ni Siku kuu kubwa ya furaha ya ndani ni tukio la maisha ya kiroho, linalohitaji maandalizi makini ya maisha ya kiroho, kwa kuongozwa na mwaliko wa Yohane Mbatizaji itengenezeni njia ya Bwana, yanyoosheni mapito yake kwa kuchunguza dhamiri ili kuondokana na mambo yote yale yanayokwamisha ujio wa Kristo katika nyoyo za waamini kwa kuwangusha dhambini na hivyo kuharibu mahusiano kati yao na Mungu pamoja na jirani zao.
Bikira Maria, awasaidie waamini kuweza kujiandaa vyema ili kukutana na upendo wa Mungu katika maisha yao, ili hatimaye, kukutana na Yesu ambaye katika mkesha wa Noeli amejifanya mdogo sana kama mbegu iliyoanguka ardhini! Yesu kwa hakika ni mbegu ya Ufalme wa Mungu. Baba Mtakatifu anawatakia waamini wote maandalizi mema katika kipindi hiki cha Majilio kwa kutubu na kumwongokea Mungu kila siku ya maisha yao.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

MJUE MTAKATIFU MARIA GORETTI