“Shirikishaneni kumaliza maradhi ya kiroho” Askofu Mkude
MOROGORO, “Moyo
mlionao wa kushikana mikono na kutatua yanayowakabili mwilini kama magonjwa na
kadhalika muwe na ushirikiano huo huo kutatua maradhi ya rohoni yanayowakabili.”
Rai hiyo
imetolewa hivi karibuni na Askofu wa Jimbo Katoliki Morogoro Mhashamu Telesphor Mkude alipokuwa akihubiri
kwenye maadhimisho ya hija ya Wanawake Wakatoliki Tanzania(WAWATA)
iliyoazimishwa katika parokia ya Mgeta.
Askofu Mkude amesema
binadamu wamekuwa wepesi kusaidiana kwenye mambo ya mwilini kama magonjwa,
sherehe na mengineyo yahusuyo mwili lakini ushirikiano huo haupo kwenye kutatua
magonjwa ya kiroho.
“Kuna watu
wanaumwa na magonjwa ya rohoni hivyo mtu anapokuja na kukueleza jambo lake
msikilize kwa makini wengine misaada wanayotaka siyo ya fedha, chakula wala
mavazi ila wanataka wasaidiwe kiroho na amani yao ipatikane,” amesema Askofu
Mkude.
Amesema mtu
ambaye shida yake ni ya kiroho ni lazima itatuliwe kiroho na usikatishwe tamaa
katika shida aliyonayo kwa kuwa umeshindwa kuitatua wewe mpeleke ngazi za juu
ili asaidiwe kutatua.
“Unaposhindwa
kutatua shida ya mtu ya kiroho usimkatishe tamaa kwa kumwambia hii haiwezekani,
badala yake mpeleke ngazi za juu ili asaidiwe inawezekana wewe msaada wako ndio
umeishia hapo lakini shida yake ikikutana na mtu wa masuala ya kiroho
inatatulika,” amesema Askofu Mkude.
Pia amesisitiza
wale ambao wapo na shida za kiroho wasikubali kukatishwa tamaa wanapotafuta
utatuzi wa shida zao na badala yake waende ngazi kwa ngazi bila kuchoka mpaka
wapate ufumbuzi ili wawe na amani mioyoni mwao.
Comments
Post a Comment