‘Matendo yenu yasiwakwaze waamini’ Ask. Nzigilwa awaasa watawa
WATAWA
nchini wamekumbushwa kubadilika kimtazamo kwa kuachana na mambo ya ulimwengu,
kwa kuwa wao wana wajibu wa kuutakatifuza wakati na kuubadilisha ulimwengu ili
uendane na mpango wa Mungu.
Rai hiyo imetolewa na Askofu
Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki Dar es salaam Mhashamu Eusebius Nzigilwa katika
Sherehe za kuweka nadhiri za daima na Yubilei ya mika 25 ya watawa wa Shirika
la Fransisko wa Asizi, wa Jimbo Kuu Katoliki Dar es salaam.
Askofu Nzigilwa ametahadharisha
kuwa endapo watawa hawatakuwa makini watajikuta ulimwengu unawabadilisha ili
waendane na matakwa ya ulimwengu badala ya wao kuubadilisha ulimwengu ili
uendane na mpango wa Mungu.
“Tunaishi kwenye ulimwengu
wenye mambo mengi ya kisasa, ulimwengu unaokwenda na wakati na kutoa nafasi
ndogo kwenye mambo ya kimungu. Na tusipojiangalia hata sisi tunaweza
kuchukuliwa katika ulimwengu huo. Tunataka na sisi tuonekane wa kisasa. Ninyi
siyo wa ulimwengu ingawaje mmetolewa katika ulimwengu huu. Msikubali kukumbwa
na malimwengu. Tusiwakwaze waamini. Tusifanye vitu ambavyo waamini hawatarajii
kuviona kutoka kwetu” ameeleza.
Aidha Askofu Nzigilwa amewatia
nguvu watawa hao kwa kuwakumbusha kuwa katika kila wito Mungu ameweka neema za
kutosha katika kutekeleza wito huo kwa hiyo wasiogope, bali washirikiane na
neema hiyo na kazi ya Mungu wataifanya kwa ufanisi mkubwa.
Pia amewataka kuendelea kutoa
huduma zao kwa upendo ili wanaopokea huduma hizo waone tofauti kutokana na
kuhudumiwa na watu wanaompenda Mungu.
“Daima watu wamefurahia huduma
zenu, na wamependa watoto wao au wao wenyewe wahudumiwe katika taasisi zenu.
Mnafanya huduma hizo katika mikono na macho ya Kristo. Huduma zenu lazima
zionekane tofauti, ili wanaopewa huduma waone kuwa wanahudumiwa na mtu anayempenda
Mungu na kujali watu. Upendo wa Mungu uongoze huduma mnazotoa kwa watu na kwa
jamii. Ndiyo maana wengi wanapenda kupata huduma zenu” ameongeza.
Comments
Post a Comment