Kanisa nchini Marekani kuonesha mshikamano na Wahamiaji
Maaskofu wa Marekani wameiteuwa tarehe 12 Disemba, sikukuu ya
Bikira Maria wa Guadalupe, kuwa ni siku ya kuonesha mshikamano kwa wakimbizi na
wahamiaji, waliofika nchini humo katika harakati za kutafuta maisha bora. Lengo
ni kuonesha dhahiri hali, hofu na mahitaji ya wakimbizi na wahamiaji nchini
humo. Kardinali Daniel DiNardo, Askofu mkuu wa Galveston-Houston na Mwenyekiti
wa Baraza la maaskofu Marekani anasema: wakati Kanisa linaelekea kusherehekea
sikukuu ya Noeli, waamini wanakumbushwa kutambua kwamba Kristo Yesu hakuzaliwa
katika hali ya ufahari nyumbani kwao, bali katika pango ugenini. Hivyo ni
muhimu kuwajali wageni na wahitaji.
Siku hiyo itakuwa siku ya sala, na maadhimisho ya ibada mbali
mbali za liturjia katika majimbo ya marekani. Katika mtandao pia kuna sala ya
Rozari iitwayo Umoja katika tofauti, unity in diversity. Rozari hiyo ina
sala zinazowahusu wakimbizi na wahamiaji. José Horacio Gomez, Askofu mkuu wa
Los Angeles na Mwenyekiti msaidizi wa Baraza la maaskofu Marekani anasema: ni
muhimu kujitafakari kwamba hali itakuwaje kwa wakimbizi, wahamiaji na wageni
iwapo sera za wahamiaji zitabadilishwa dhidi yao. Lengo la Kanisa nchini
Marekani ni kutetea haki msingi za wahamiaji, wakitambuliwa kuwa ni binadamu
wenye kustahili heshima kwa utu wao na kusaidiwa.
Katika mshikamano huo, ambapo Kamati ya Baraza la maaskofu kwa
ajili ya Kanisa la Amerika ya kusini inaadhimisha miaka 50 ya ukusanyaji wa
misaada kwa ajili ya Amerika ya kusini, mwaka huu miradi 204 itapatiwa misaada
ya jumla ya dola milioni 4. Miradi hii inahusu maandalizi ya walei, waseminari,
watawa, shughuli za kitume, uchungaji kwa wafungwa na kwa vijana. Katika hiyo
miradi, upo pia ule wa ujenzi wa makanisa ya Equador yaliyoharibiwa na tetemeko
la ardhi mwezi Aprili mwaka huu 2016.
Eusebius L. Elizondo, Askofu msaidizi wa Seattle na Mwenyekiti
wa kamati ya Baraza la maaskofu Marekani kwa ajili ya Kanisa Amerika ya kusini
anasema kwamba: shughuli za kichungaji na elimu vinapaswa kupatikana kwa wote,
lakini kwa walio wengi Amerika ya kusini hawapati huduma hizo kwa sababu za
kigeografia au kiuchumi. Misaada hiyo inapeleka imani na matumaini kwa wale
walio mbali na wenye kuhitaji. Ni misaada inayofanikishwa kwa ukarimu wa
waamini wakatoliki nchini Marekani. Kwa miaka ya karibuni, misaada mingi
ilielekezwa katika kuijenga upya Haiti baada ya tetemeko la mwaka 2010, na
mingine nchini Ufilipini.
Na Padre Celestine Nyanda
Idhaa ya Kiswahili, Radio Vatican.
Comments
Post a Comment