Maaskofu watoa angalizo kuhusu mwelekeo wa nchi
·
Wahimiza
utawala wa sheria, haki, amani na uwajibikaji
·
Watahadharisha
kukithiri kwa uharibifu wa mazingira
KATIKA kusherehekea Sikukuu ya Noeli nchini, baadhi ya Maaskofu wa
Kanisa Katoliki Tanzania wamewataka watanzania kujenga na kudumisha misingi ya
haki, amani, upendo, umoja na mshikamano wa kitaifa, na kuachana na matendo ya
giza yanayosababisha rushwa, ufisadi na utendaji wa kazi unaofanywa kwa mazoea.
Akitoa
homilia yake katika Misa ya Krismasi ndani ya Kanisa la Bikira Maria wa Fatima
lililopo Geita, Askofu Flavian Kassala wa Jimbo Katoliki Geita amesema kuwa
kila mtanzania anapaswa ajione kuwa ni chanzo cha amani.
Askofu
Kassala ameonya kuwa kisiwepo kisingizio
chochote kwa mtu yeyote kuvuruga amani ya nchi ambayo imekuwa zawadi kubwa na
ya kipekee kutoka kwa Mwenyezi Mungu.
Ametoa
mfano wa nchi zilizo katika vita, ambako watu wanavyoishi kwa shida kubwa huku
maelfu ya watu wakipoteza maisha, na hivyo akatoa wito kila mtu kuhakikisha
anakuwa chanzo cha amani kuanzia ngazi ya familia.
Aidha
Askofu Kassala amewahimiza wazazi wote katika familia zao kuwa chanzo cha habari
njema ili watu wauige mwenendo mwema, na hatimaye familia zao zibaki daima katika amani ambayo
ni zawadi kubwa inayoletwa na Kristo anayezaliwa kama mfalme wa amani.
Askofu Shao aonya wanaopinga mapambano
dhidi ya rushwa
Kwa upande wake Askofu wa Jimbo
Katoliki Zanzibar Mhashamu Agustino Shao amewaonya watu wenye nia ya kukwamisha
jitihada za Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais John Magufuli ambayo
inapambana na vitendo vya rushwa na
ufisadi, ili kuiwezesha nchi kufikia maendeleo endelevu yenye tija kwa kila
mtanzania.
Aidha amesema kuwa jambo la
msingi kwa Serikali ni kujikita katika utawala wa sheria, kuzingatia haki, amani
na uwajibikaji bila ubaguzi, na kuwa watanzania wenye mapenzi mema wataendelea
kuunga mkono jitihada za serikali hiyo.
Askofu Mapunda atahadharisha kukithiri kwa uharibifu wa mazingira
Askofu wa Jimbo Katoliki Singida
Mhashamu Edward Mapunda amewakumbusha watanzania kuwa wana dhamana na wajibu wa
kulinda, kutunza na kuendeleza mazingira ‘nyumba ya wote’ ili kuepuka athari za
mabadiliko ya tabianchi zinazowaathiri watu wengi.
Amesema kuwa kwa sasa nchi
inakumbwa na uhaba mkubwa wa mvua kutokana na uharibifu wa mazingira. Ametoa
rai kuwa matukio mbali mbali ya maisha iwe ni fursa ya kupanda mti na kuboresha
mazingira kama mwendelezo wa kazi ya uumbaji ambayo mwanadamu amekabidhiwa
kuitekeleza.
Askofu NiweMugizi aonya wanaoyumbishwa kiimani
Kwa upande wake Askofu Severin
NiweMugizi wa Jimbo Katoliki Rulenge-Ngara, amewataka watanzania kutubu na
kumwongokea Mungu ili kuondokana na vitendo na maisha ya dhambi na giza kwa kutambua
uwepo wa Mungu kati yao.
Aidha Askofu NiweMugizi ameonya
tabia ya waamini ambao kila kukicha wanakimbilia kwenye makanisa yanayoahidi
miujiza ya njia za mkato katika maisha.
Amesema kuwa kinachowakimbiza
waamini hao ni kutaka fedha za haraka bila ya kufanya kazi, upwonywaji wa
magonjwa na ibada zisizo na utulivu. Ameeleza kuwa kuzaliwa kwa Yesu Kristo,
Mwana wa Mungu, iwe ni fursa kwa waamini kutambua uwepo endelevu wa Mungu
katika maisha nao na kwamba, wanapaswa kutubu na kumwongokea Mungu, bila kukata
wala kukatishwa tama.
Askofu Mkude akemea matabaka
Askofu wa Jimbo Katoliki
Morogoro Mhashamu Telesphory Mkude amebainisha kuwa nidhamu, uadilifu, na
uwajibikaji vitaondoa matabaka
yaliyokuwa yanaanza kujengeka nchini kwa kuwa na tofauti kubwa kati ya matajiri
na maskini.
Comments
Post a Comment