Ujumbe wa Papa Francisko wa Siku ya 50 ya Kuombea Amani Duniani 2017
Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe Mosi, Januari, Sherehe ya
Bikira Maria Mama wa Mungu anaadhimisha Siku ya Kuombea Amani Duniani.
Maadhimisho ya Siku ya 50 kwa Mwaka 2017 yanaongozwa na kauli mbiu “Kutotumia
nguvu: mtindo wa siasa ya amani”. Baba Mtakatifu anaelezea kuhusu vita,
kinzani na mipasuko ya kijamii duniani; umuhimu wa kutangaza na kushuhudia
Habari Njema ya Wokovu; Wajumbe na mashuhuda wa amani duniani; umuhimu wa
kuzamisha mizizi katika siasa za kutotumia nguvu, mwishoni, Baba Mtakatifu
anatoa mwaliko kwa familia ya Mungu duniani pamoja na kuhitimisha ujumbe wake!
Mwanzo mwa Mwaka mpya wa 2017 Baba Mtakatifu anapenda kuwatakia
watu wote heri, baraka na amani kwa kutambua kwamba, wote wameumbwa kwa sura na
mfano wa Mungu. Utu na heshima ya watu wanaoishi katika maeneo ya vita unapaswa
kuheshimiwa na kuthaminiwa, kwa kushinda kishawishi cha kutumia siasa ya vita.
Miaka 50 iliyopita, Mwenyeheri Paulo VI alituma ujumbe wa amani kwa familia ya
Mungu duniani kwa kuonesha kwamba, amani ni chachu ya maendeleo ya watu na
kwamba, kinzani, misigano na utaifa usiokuwa na mashiko ni mambo yaliyokuwa
yanatishia amani. Kumbe, vita, migogoro na kinzani mbali mbali zinaweza
kupatiwa ufumbuzi kwa kujikita katika: sheria, haki, usawa, upendo; ukweli na
uhuru, tunu ambazo zinaonesha umuhimu wa pekee hata katika ulimwengu mamboleo.
Kwa namna ya pekee, Baba Mtakatifu Francisko anapenda kukazia
kutotumia nguvu kuwa ndio unaopaswa kuwa ni mtundo wa maisha ya kisiasa ili
kujenga na kudumisha amani duniani na anamwomba Mwenyezi Mungu awasaidie watu
kuchota tunu hizi msingi kutoka katika undani wa maisha yao. Upendo na amani
ziwe ni tunu ambazo zitasaidia kujenga na kudumisha mahusiano ya binafsi,
kijamii na kimataifa. Huu ni mwaliko wa kuondokana na utamaduni wa kulipizana
kisasi na kwamba, wahanga wanaweza kuwa ni wadau wa mchakato wa kutotumia nguvu
kwa ajili ya ujenzi wa amani katika medani mbali mbali za maisha, ili kweli
maamuzi, mahusiano, matendo na nguvu zote za kisiasa ziweze kujielekeza huko.
Baba Mtakatifu anakaza kusema, Karne ya 20 iligubikwa na vita
kuu ya dunia, vitisho vya mashambulizi ya silaha za kinyuklia, kinzani na
migogoro inayoendelea kujitokeza sehemu mbali mbali za dunia kana kwamba, ni
Vita ya Tatu ya Dunia. Vyombo vya mawasiliano ya jamii vinaendelea kuonesha
jinsi ambavyo dunia imesambaratika kutokana na kinzani na mipasuko ya kijamii
inayoendelea kusababisha mateso na mahangaiko ya watu wengi. Vita, ugaidi,
vitendo vya kihalifu na mashambulizi ya silaha ni mambo ambayo hayawezi
kutabirika. Wakimbizi na wahamiaji wananyanyaswa na kudhulumiwa; kuna wahanga
wa biashara haramu ya binadamu pamoja na uharibifu wa mazingira.
Baba Mtakatifu Francisko anauliza, Je, lengo na uharibifu wote
huu ni nini? Bila shaka ni kwa ajili ya mafao ya “Mabwana wa vita”. Vita kamwe
haitaweza kuwa ni suluhu ya ulimwengu uliomeguka vipande vipande kwani matokeo
yake ni: uhamiaji wa nguvu, mateso na mahangaiko na kiasi kikubwa cha
rasilimali kinaelekezwa kwenye masuala ya kivita na kuondolewa katika: huduma
za afya, elimu, ustawi na maendeleo ya watu wengi duniani. Na mbaya zaidi vita
inapelekea vifo vya watu: kiroho na kimwili, kwa wengi na kama si kwa watu
wote.
Baba Mtakatifu anaendelea kukaza kwa kusema, Yesu Kristo ni
kiini cha Habari Njema ya Wokovu anayekazia amani inayobubujika kutoka katika
sakafu ya moyo wa mwanadamu, kwa kuonesha upendo wa Mungu usiokuwa na
mipaka, upendo unafumbatwa katika msamaha kwa kutoa na kupokea, kwa kuwasamehe
hata wale waliowakosea bila kulipiza kisasi. Habari Njema inawarejeshea
wadhambi maisha mapya, inawataka Mitume kurejesha panga zao alani mwake na
kuendelea na Njia ya Msalaba pale ambapo amani itavunjilia mbali uadui; kwa
kuiachia Habari Njema ya Wokovu ifanye kazi yake, ili huruma ya Mungu igange na
kuponya majeraha ya vita, ili hatimaye, waweze kugeuka na kuwa ni vyombo na
mashuhuda wa upatanisho na amani inayobubujika kutoka katika sakafu ya maisha
ya watu!
Wafuasi wa Kristo wanapaswa kushuhudia upendo na wema
unaobubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu na kwamba, kutokubali kutumia nguvu ni
njia ya kuonesha utu unaodhihirisha upendo na nguvu ya Mungu ambao inapambana
na ubaya kwa kutumia upendo na ukweli. Upendo kwa adui ni kielelezo cha mageuzi
katika maisha ya Kikristo; kwa kujibu ubaya kwa wema na wala si kujisalimisha,
ili kuvunjilia mbali mnyororo wa ukosefu wa haki msingi! Mama Theresa wa
Calcutta anasema familia ya binadamu inahitaji kukaa pamoja na watu kupendana
ili kujenga na kudumisha amani na wala si silaha za mahangamizi, kwani biashara
ya silaha inaendelea kuwatajirisha wahusika wakati ambapo kuna mashuhuda wa
amani wanaendelea kuwasaidia jirani zao. Hawa ni watu wanaosimama kidete:
kushuhudia kulinda, kutetea na kudumisha uhai wa binadamu; wanaendeleza moyo wa
ukarimu na mapendo; wanaohudumia kwa huruma na upendo; kwa kutambua utu na
heshima ya binadamu.
Viongozi wakuu wa Jumuiya ya Kimataifa wanasutwa na maneno ya
Mtakatifu Theresa wa Calcutta kwa kujitambua kuwa ni wahalifu pamoja na
ongezeko la umaskini duniani kwani wao pia wamechangia hali hii. Hii ni
changamoto ya kuwahudumia wahanga kwa ukarimu, moyo wa majitoleo, kwa kugusa na
kuganga madonda yao; kwa kuponya maisha yaliyotikiswa na kusambaratishwa na
vita! Duniani kuna mashuhuda na wajenzi wa amani kama vile Mahatma Gandhi na
Khan Abdul Ghaffar waliojisadaka kupigania uhuru wa India pasi na kumwaga damu;
Martin Luther Mdogo aliyepambana ubaguzi wa rangi kwa njia ya amani: Hawa ni
watu ambao kamwe hawataweza kusahaulika duniani!
Kuna mifano ya wanawake kama Leymah Gbowee na wanawake kutoka
Liberia waliosimama kidete kupinga vita kwa njia ya sala pamoja na kuchochea
majadiliano yaliyopelekea kuhitimishwa kwa vita ya pili ya wenyewe kwa wenyewe
nchini Liberia. Kuna viongozi kama Mtakatifu Yohane Paulo II waliosimama kidete
hadi kuta za utawala wa Kikomunisti zitaanguka chali! Ni kiongozi aliyewataka
watu kusimamia na kuwa ni mashuhuda wa ukweli na haki kwa kupambana bila
kumwaga damu sanjari na kupinga mapambano ya makundi ya kijamii na vita vya
kimataifa. Kanisa daima limesimama kidete kutangaza na kushuhudia Injili ya
amani kwa kuwataka wahusika kuwa ni wajenzi wa amani ya kudumu!
Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kufafanua kwamba, huduma kwa
wahanga wa ukosefu wa haki msingi za binadamu ni utajiri na amana ya dini zote
duniani na wala si kwa Kanisa Katoliki peke yake kwani hii ni dira
inayowaelekeza watu katika njia ya maisha. Ikumbukwe kuwa, hakuna dini
ambayo ni ya kigaidi na kwamba, vita ni kufuru ya Jina la Mungu na kwamba,
haiwezekani kutumia jina la Mungu kuhalalisha vita vitakatifu kwani hakuna vita
vitakatifu, isipokuwa amani peke yake ndiyo takatifu.
Familia inapaswa kuwa ni mahali muafaka pa kukuza na kudumisha
siasa ya kutotumia nguvu kwa kuambata furaha ya upendo. Kwani, familia ni
mahali pa kujisadaka na kuhudumiana kama ndugu pamoja na kuvuka kinzani na
migogoro si kwa kutumia jazba, nguvu au mkong’oto; bali kwa njia ya
majadiliano, heshima na kwa kutafuta mafao ya jirani, huruma na msamaha! Furaha
ya upendo ndani ya familia inapaswa kushamiri na kuambata jamii nzima, kwa
kujikita katika kanuni maadili na udugu ili kuondokana na mantiki ya woga na
wasi wasi; kinzani na vita.
Hapa kinachotakiwa ni kudumisha mchakato wa uwajibikaji, heshima
na majadiliano katika ukweli na uwazi. Baba Mtakatifu anaiomba Jumuiya ya
Kimataifa kuzuia na hatimaye kupiga rufuku kabisa utengenezaji na utumiaji wa
silaha za kinyuklia.
Ikiwa kama Jumuiya ya Kimataifa itaaminiana na kuthaminiana
mintarafu kanuni maadili hakuna sababu ya kuwa na hofu ya mashambulizi ya
kinyuklia. Kuna haja pia ya kuondokana na mashambulizi dhidi ya wanawake
majumbani pamoja na watoto ili kujenga na kudumisha amani.
Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu,
ulikuwa ni mwaliko kwa waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema
kuchunguza dhamiri zao, ili kuruhusu huruma ya Mungu iweze kupenya nyoyoni
mwao. Ni mwaliko wa kujenga utamaduni wa kuwashirisha wengine badala ya
kujikita kwenye utandawazi unaowatenga wengine, kwa kuwaonesha upendo, ukarimu,
tabasamu pamoja na kutekeleza matendo madogo madogo yanayopandikiza mbegu ya
amani na urafiki, ili kuvunjilia mbali mnyororo wa vita, unyonyaji na ubinafsi.
Baba Mtakatifu anatumia maadhimisho ya Siku ya Kuombea Amani
Duniani kwa Mwaka 2017 kuwaalika viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa kujikita
katika kanuni maadili na Heri za Mlimani, muhtasari wa mafundisho makuu ya Yesu
katika kupambana matumizi ya nguvu. Watu wenye heri ni wale wenye: rehema,
wapole, wenye njaa na kiu ya haki; wenye moyo safi na wapatanishi. Hii ni
changamoto kubwa kwa viongozi wa kisiasa, kidini na kijamii ili kujenga jamii
kwa mtindo wa ushuhuda wa amani; huruma kwa kukataa utandawazi usiojali
mahangaiko ya watu; unaharibu mazingira nyumba ya wote pamoja na uchu wa mali na
madaraka kwa gharama yoyote ile.
Ili kuweza kujikita katika ujenzi wa mfumo mpya kuna haja ya
kuambata mshikamano, kwa kuandika historia mpya pamoja na kujenga urafiki wa
kijamii, ili kuonesha kwamba, umoja una nguvu zaidi kuliko hata vita na
kinzani; kwani, ulimwengu wote kimsingi umeshikamana. Hapa Jumuiya ya Kimataifa
inapaswa kupambana na changamoto hizi kwa kuungana ili kuanza mchakato
mpya wa maisha kwa kuheshimu na kuenzi tofauti zinazojitokeza.
Baba Mtakatifu anapenda kuihakikishia Jumuiya ya Kimataifa
kwamba, Kanisa Katoliki litaendelea kuunga mkono mchakato wa ujenzi wa amani
duniani. Tarehe Mosi, Januari 2017, Baraza Jipya la Kipapa Huduma ya Maendeleo
Endelevu linazinduliwa rasmi, ili kulisaidia Kanisa kukuza na kudumisha haki,
amani na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote; kwa kuwahudumia wakimbizi,
wahitaji, wagonjwa, waliotengwa na jamii; wahanga wa vita na majanga asilia;
wafungwa na wasiokuwa na fursa za ajira pamoja na waathirika wa utumwa mamboleo
na mateso; mambo yanayodhalilisha utu na heshima ya binadamu! Vitendo vyote
vyenye mwelekeo huu vinapania kujenga ulimwengu usiokuwa na vita, hatua muhimu
katika haki na amani.
Baba Mtakatifu Francisko anasema, alitia mkwaju ujumbe huu wa
Siku ya 50 ya Kuombea Amani Duniani hapo tarehe 8 Desemba 2016 wakati wa
maadhimisho ya Siku kuu ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili, na Malkia wa
amani. Kuzaliwa kwa mwanaye wa pekee, Malaika walikuwa wanamtukuza Mungu na
kuitakia dunia amani kwa watu wote wenye mapenzi mema. Baba Mtakatifu anawaalika
waamini kumwomba Bikira Maria ili aweze kuwaongoza katika mchakato wa kutafuta
amani duniani. Kila mtu anatamani amani na kuna mamillioni ya watu wanaoshiriki
mchakato wa ujenzi wa amani kwa matendo yao ya kila siku na kwamba, kuna watu
wanaojitahidi kufa na kupona kujenga amani.
Mwaka 2017, waamini na watu wote wenye mapenzi mema wanahimizwa
kujenga amani kwa njia ya sala na maneno yanayomwilishwa katika matendo
yanayobubujika kutoka katika sakafu ya nyoyo za watu. Lengo ni kujenga Jumuiya
isiyokuwa na vita na inayojitaabisha kutunza mazingira, nyumba ya wote. Hakuna
jambo lisilowezekana ikiwa kama watu watamkimbilia Mwenyezi Mungu kwa njia ya
amani. Watu wote wanaweza kuwa ni wajenzi wa amani!
Ujumbe huu umehaririwa na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
Comments
Post a Comment