‘Ukristo umekomesha utumwa na ujinga Tanzania’ Ask. Lebulu
IMEELEZWA
kuwa ujio wa Wamisonari walioleta ukristo Tanzania Bara miaka 150 iliyopita,
uliwezesha mapambano dhidi ya biashara ya utumwa, ujinga, umasikini na maradhi.
Hayo yameelezwa na Askofu wa
Jimbo Kuu Katoliki Arusha Mhashamu Josaphat Lebulu, katika mahojiano maalum na
Kiongozi, miezi miwili baada ya uzinduzi wa Yubilei ya miaka 150 ya
Uinjilishaji Tanzania Bara, na miaka 100 ya upadri.
Akielezea huduma za Kanisa katika
kipindi cha miaka 150 ya uinjilishaji, Askofu Lebulu amesema kuwa wamisionari
hawakuishia tu katika kuinjilisha, bali walijikita katika kuendeleza hadhi ya
mwanadamu mzima, kiroho na kimwili.
“Ukristo unaelekeza kutambua
hadhi ya ubinadamu, hivyo pamoja na kufanya shughuli za uinjilishaji,
wamisionari walipinga biashara ya utumwa, ili kulinda hadhi ya ubinadamu”
ameeleza.
Aidha Askofu Lebulu amebeinisha
kuwa Kanisa la Tanzania limefanikiwa kuwa taasisi inayosaidia watu katika
uinjilishaji kimwili na kiroho, kupitia huduma mbalimbali ikiwa ni pamoja na
afya, elimu na miradi ya maendeleo.
Ameeleza kuwa ndani ya kipindi
cha miaka 150 Kanisa limekomaa, na hii imedhihirisha uwepo na utendaji wa
Kristo mfufuka Tanzania Bara na Afrika. Amesema kuwa Huruma ya Mungu ndiyo
iliyowawezesha wamisionari kuwafikia watu wengi, hadi Tanzania na kuwa msaada
kwa watu wenye shida.
“Tunapoadhimisha miaka 150 ya
ukristo, tunashuhudia ukomavu wa kanisa, yaani uwepo wake Kristo katika ngazi
mbalimbali, kuanzia kwenye familia, jumuiya ndogo ndogo, parokia hadi majimbo”
amesema.
Amewaasa waamini kujitoa katika
kulitegemeza kanisa ili kazi ya umisionari iendelee. Amesema kuwa Kanisa ambalo
halijitegemei kifikra, kihuduma na kiuchumi ni fukara.
“Waamini ni kiini cha kufaulu
kwa Kanisa, waamini ndiyo kanisa na sehemu ya msingi katika kanisa.
Kulitegemeza kanisa siyo mzigo, ni jukumu letu” ameasa.
Comments
Post a Comment