Askofu Ngalalekumtwa awataka waamini kuwaombea Mapadri
ASKOFU wa Jimbo Katoliki Iringa Mhashamu
Tarcisius Ngalalekumtwa amezindua mwaka wa Jubilei ya miaka 100 ya mapadri
wazalendo na kuwataka waamini kuendelea kuwaombea mapadri popote walipo.
Uzinduzi wa jubilei
hiyo umefanyika kwenye kanisa Kuu la Moyo Mtakatifu wa Yesu Parokia ya Kihesa
kwa kuwashwa kwa mshumaa mara baada ya Askofu Ngalalekumtwa kumaliza
kutoa daraja la ushemasi kwa mafrateli Jerome Mtatifikolo wa parokia ya Ilole
na Jerome Mponzi wa parokia ya Nyakipambo.
Akitoa homilia
kwenye misa hiyo Mhashamu Ngalalekumtwa amesema kwamba, sambamba na utoaji wa
daraja hilo lakini pia waamini wanatakiwa kuwaombea viongozi wa Serikali ili
waweze kutenda kazi zao kiuaminifu.
Mhashamu
Ngalalekumtwa amesema Kristo ndiye mfalme wa amani, kwa hiyo wanapokumbuka hayo
katika historia kuuawa kwa watoto wadogo tena wasio na hatia wamuombe Kristo
ili aweze kuratibu kwa wale wanaosimamia maslahi ya ulimwengu kusudi hawa
watawala wawajibike ipasavyo.
“Leo ni siku ya
kuwaombea wote kuanzia rais John Pombe Magufuli na utawala wake na wote walio kama yeye
tuwaombee kusudi wawajibike ipasavyo waelewe kwamba hawapo pale kwa
ajili ya kuongeza dola kwenye akaunti zao au mitungi yao bali wapo
pale kusudi wongeze raha, amani na ustawi wa maisha yao, maana kuna maelekeo ya
kujisahau, akina Herode tumekuwa nao wengi wa kutosha,” amesema Mhashamu
Ngalalekumtwa
Aidha amesema kuwa
Mungu amewapatia zawadi ya mashemasi ili waweze kuwa wahudumu
katika ngazi ya ushemasi na imetokea tu wote ni akina Jerome, imetokea tu sasa
katika mapokeo na mfumo wa kanisa, mashemasi ni watumishi, mawakili wasimamizi,
walinzi na watunzaji wa familia ya Mungu wakiwa wasaidizi wa Maaskofu wao na
pia mapadri.
“Ili kazi hiyo
ifanyike na ilete baraka na izae matunda, Paulo anasema kwamba Mashemasi wawe
na wastahimilivu si watu wa kauli mbili au kutumia mvinyo sana, si watu wa
kutamani fedha ya aibu, wanapoingia huku si kwamba nawaajiri, hawa wanaajiriwa
na nyie waamini, muwatunze hawa mashemasi, mapdri na masista, lakini wao kama
wao wasiwe kama watu wa kutamani fedha ya aibu.
Wawe watu wasafi,
waandamane na Kristo ambaye kazi yake ni kutakatifuza, kuwatunza watu, wawe
watu wa Mungu, Mungu awakubali na nyie pia muwakubali.”
“Daraja wanalopewa
leo ni la mpito, wapo kwenye safari ya kuendea ukuhani (upadri), wanapitia huku
ili waweze kujua nini maana ya kuwa watumishi wa watu, tuwaombee wawe na
mwenendo safi kwa wote, ili kukutana wao iwe mwanzo wa baraka, tunawaombea wawe
watu wa sala na vitendea kazi tumewapatia, vitabu ambavyo vina sala maalumu ya
kanisa.
Watabatiza,
watatangaza injili watafungisha ndoa, watazika wafu, watu watakuja kuomba
ushauri kwenu, watu wajifunze kwenu, maisha yenu yawe mfano bora kwa wengine,
watu wajifunze kwenu maana ya kuwa wafuasi wa Kristo, shikeni kiaminifu maisha
ya useja kwa sababu yule ambaye anataka muendeleze kazi yake alikuwa mseja
Krito, ndiyo maana kanisa Katoliki linabaki na msimamo huo na usafi huo wa
ubikira, muige mfano wa Kristo mwenyewe.”
Comments
Post a Comment