SIKUKUU YA BIKIRA MARIA MKINGIWA DHAMBI YA ASILI NA MSIMAMIZI WA TANZANIA
Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania katika mkutano wake mkuu wa
mwaka uliofanyika Juni 2016 liliamua kwamba, kuanzia sasa Siku kuu ya Bikira
Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili itakuwa inaadhimishwa kitaifa nchini ifikapo
tarehe 9 Desemba. Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa katika barua yake kwa ajili ya
tukio hili anasema, uamuzi huu ni utekelezaji wa zawadi iliyotolewa na
Mtakatifu Yohane Paulo II kunako mwaka 1984 kwa kuiweka Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania nchini ya ulinzi na usimamizi wa Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya
Asili.
Kumbe, kwa mara ya kwanza, katika historia ya Tanzania, Siku kuu
ya Bikira Maria mkingiwa Dhambi ya Asili kitaifa nchini Tanzania inaadhimishwa
rasmi tarehe 9 Desemba 2016. Hii ni nafasi ya kuombea familia ya Mungu nchini
Tanzania ili iweze kudumisha misingi ya haki, amani, upendo, umoja na
mshikamano wa kitaifa, nguzo msingi ambazo daima zimewatambulisha watanzania
katika Jumuiya ya Kimataifa.
Itakumbukwa kwamba, wakati wa mkesha wa uhuru wa Tanzania kunako
mwaka 1961, Baba Mtakatifu Yohane XXIII alitunga sala maalum kwa ajili ya
kuiombea Tanzania ili uhuru wake uwawezesha watanzania kuishi maisha mema zaidi
kadiri iwastahilivyo watoto wa Mungu. Aliwaombea viongozi wa Serikali na
watunga sera na sheria ziwe ni kwa ajili ya mafao ya wengi. Aliwaombea
Watanzania paji la imani, hekima, ukweli na uaminifu kwa Amri za Mungu.
Aliwaombea upendo wa Kimungu ili kujenga na kudumisha umoja na mshikamano wa
kitaifa ili kushinda: utengano, ushindani, ukabila, utaifa ili watanzania wote
waweze kuwa ndugu wamoja na katika Fumbo la Utatu Mtakatifu. Mtakatifu Yohane
XXIII aliombea amani na maridhiano kati ya Tanzania na majirani zake; viongozi
wa Serikali ili waweze kutimiza wajibu wao kama inavyostahili; raia kujipatia
maisha bora zaidi na hatimaye, waweze kuwa ni raia katika Ufalme wa mbinguni
milele na milele!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
Comments
Post a Comment