Waamini wa Kanisa Katoliki Malawi waandamana hadi bungeni
WAAMINI wa Kanisa Katoliki Malawi wameandama hadi
bungeni kupinga kupitishwa sheria ya utoaji mimba na ndoa za jinsi moja.
Taarifa kutoka ofisi ya
Mawasiliano ya Baraza la Maaskofu Katoliki Malawi (ECM) zimeeleza kuwa, maandamano hayo ya
amani yamefanyika Desemba 6 mwaka huu yakiongozwa na Katibu Mkuu wa ECM Padri Henry Saindi.
Aidha imeelezwa kuwa, tukio hilo ni la kihistoria nchini humo kwa
waamini hao kuonesha ujasiri wa kiimani na kuthamini uhai na utu wa mwanadamu.
Katibu Mkuu wa ECM Padri Saindi ameeleza kuwa, dhamira kuu ya
maandamano hayo ilikuwa ‘kuwasha mshumaa’ mshumaa wa kumulika uhai na familia
ambazo chanzo chake ni Kristo.
“ Barabara zilifurika waamini
kutoka wilaya 28 wanaotaka bunge letu kupitisha sheria ya kulinda uhai yaani
kupinga sheria ya kuhalalisha utoaji mimba na ndoa za jinsi moja,” amesema
Padri Saindi.
Akihutubia maelfu ya watu
waliojitokeza katika maandamano hayo ya amani, Padri Saindi amesema kuwa, nchi
ya Malawi si ya kipagani. Ni nchi inayomuamini Mungu na kumcha Mungu kupitia
dini mbalimbali nchini humo, hivyo hakuna haja ya kuhalalisha utoaji mimba na
ndoa za jinsi moja kwani kufanya hivyo ni kwenda kinyume na matakwa ya Mungu.
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya
masuala ya Afya ya Bunge hilo Bi.
Julliana Lunguzi aliyepokea mapendekezo hayo ya Baraza la Maaskofu Katoliki
Malawi kupitia Katibu wake Padri Saindi amewahakikishia waamini hao kuwa
wamekubaliana na mapendekezo ya Kanisa Katoliki Malawi na watafanyia kazi
kulingana na mapendekezo yao.
“Mimi pia ni muumini wa
Kanisa Katoliki, mwanamke tena mwenye ujuzi wa utabibu. Sitakubaliana kupitisha
sheria ya utoaji mimba na ndoa za jinsi moja. Ninachowasihi ni kuendelea
kutuombea ili Roho Mtakatifu atuongoze tufanye maamuzi sahihi ndani ya bunge
letu,” amesema Bi. Lunguzi.
Comments
Post a Comment