Mamlaka kwa mapadri waungamishi kuondoa adhabu ya utoaji mimba
Katika barua yake ya kitume Misericordia et misera,
yaani Huruma na amani, Baba Mtakatifu Francisko kaeleza kuwapa
mamlaka mapadri waungamishi wote kuondoa adhabu na kusamehe dhambi ya kutoa
mimba. Kufuatia utaratibu huo mpya, baadhi wametoa taarifa mkanganyiko juu ya
suala hilo katika maeneo mbali mbali duniani. Marcello Semeraro, Askofu wa
Albano Italia, kapeleka barua ya kichungaji kwa mapadri na watawa, akitoa
maelekezo kuwasaidia waamini kuelewa tofauti kati ya dhambi na adhabu.
Kanuni sheria za Kanisa, zinaitambua dhambi ya utoaji mimba kuwa
ni moja ya makosa makubwa dhidi ya uhai wa mwanadamu, hasa katika hali ya
unyonge wake. Kwa sababu hiyo adhabu iliyopo ni kwa wahusika kujitenga na
Kanisa, hivyo kujizuia kupokea Sakramenti yeyote mpaka adhabu hiyo iondolewe.
Adhabu ya namna hiyo katika Kanisa, ni Askofu au padri aliyeteuliwa na Askofu
ndiye mwenye mamlaka wa kuiondoa adhabu hiyo, sio katika taratibu za mahakama
kikanisa, bali katika Sakramenti ya kitubio. Mamlaka ya kuitoa adhabu hiyo
kimahakama, nje ya Sakramenti ya Upatanisho, ni mahakama kuu ya Kanisa.
Tangu mwaka 1983 adhabu hiyo ilipowekwa na sheria kanuni za
Kanisa, kumekuwa na magumu mengi na mahangaiko kwa upande mwingine, pale ambapo
inakuwa vigumu kumpata Askofu kwa wakati au mapadri wachache walioruhusiwa
kutoa adhabu hiyo. Hali kama hii ilipelekea waamini waliojutia dhambi hiyo,
kujikuta wakikaa muda mrefu kabla ya kupata kuondolewa adhabu hiyo.
Kilichofanyika katika barua ya kitume ya Baba Mtakatifu
Francisko, Misericordia et misera, Huruma na amani,
ni kurahisisha namna ya kuiondoa adhabi hiyo, kupitia Sakramenti ya Upatanisho.
Kumbe Mama Kanisa sasa anawapatia mamlaka kisheria mapadri wote waungamishaji,
kuweza kuondoa adhabu hiyo, na kisha kumuungamisha mhusika. Ieleweke vizuri
hapa kuwa, kuna tofauti kati ya dhambi na maungamo, na kosa na adhabu.
Yeyote mwenye kuhusika katika harakati za utoaji mimba, kwa
ushauri, kwa kuchangia fedha, kwa kuhudumu kwa namna yeyote, anakuwa ametenda
kosa dhidi ya uhai wa kitoto hicho, na adhabu yake ni kujitenga na kujizuia
kupokea Sakramenti yeyote, ikiwemo ya Upatanisho. Tendo hilo linabaki kuwa ni
dhambi mbele ya Mungu. Lakini ili aweze kuondolewa dhambi hiyo, mhusika au
mshiriki yeyote anapaswa kwanza aondolewe adhabu iliyomfunga kuungama, ndipo
aungame. Awali kama ilivyoelezwa, adhabu hii iliondolewa na Askofu au mapadri
wachache walioteuliwa. Kwa sasa adhabu hiyo inaweza kuondolewa na padri yeyote
muungamishi, na kisha kumuondolea dhambi.
Sheria kanuni za Kanisa zina lengo kubwa la kuokoa roho za
waamini, na sio kulipiza kisasi. Kila utaratibu, mazuio au adhabu zilizowekwa
zina lengo la kumsaidia mwamini, kumrekebisha, kumtakasa, ili aweze kuirithi
mbingu. Katika hali hii, utaratibu wa kuondoa adhabu ya wale walioshiriki
katika utoaji mimba umerahisishwa, ili kuepuka mwamini aliyejutia kweli kweli
kosa hilo kukaa na dhambi muda mrefu, na kuhatarisha wokovu wa roho yake.
Utaratibu huu haupunguzi uzito wa dhambi wala uzito wa kosa wala
uzito wa adhabu. Baba Mtakatifu Francisko amesisitiza juu ya uthabiti wa
mafundisho ya Kanisa kwamba, ni dhambi na kosa kubwa kutoa uhai wa mwanadamu,
na zaidi uhai wa mtoto aliye mnyonge au mzee au mgonjwa aliye katika mateso au
kufani. Adhabu ya kosa la utoaji mimba inabaki kuwa ni ile ile ya kujifungia
nje ya Kanisa na neema zinazoshirikishwa kupitia Kanisa. Kwa mwamini anayejutia
rohoni mwake kosa na dhambi hiyo, na kudhamiria kutorudia na kuwa tayari kwa
malipizi, Kanisa linamwekea sasa urahisi wa kufikia lengo hilo.
Kwa upande wa mapadri waungamishi, wakumbuke kuwa katika utume
wao huo, wanao wajibu kujiandaa vema kuwasaidia kweli waungamaji kupata neema,
kubadili mwenendo wao ili waweze kuokoka. Kwa sababu hiyo watawasindikiza kwa
upendo katika safari yao ya kujipatanisha na Mungu. Kila Padre muungamishaji ni
daktari wa kuiponya roho ya muungamaji, lakini pia ni hakimu wa haki,
anayepaswa kutoa malipizi ya kumfaa muungamaji kutakasika kutoka kwenye makosa
aliyotenda (Rej., Sheria Kanunbi za Kanisa, n. 978).
Mapadri wawabebe kondoo wa Kristo waliopotea, wawahangaikie ili
waweze kurudi kundini baada ya kuwatoa katika hali ya upotevu na kuwaosha
makosa yao. Wawafariji kwa upendo wa kibaba na utambuzi wao kuwa binadamu ni
dhaifu na anahitaji msaada wa wengine, hasa walioandaliwa ili kuweza kupiga
hatua. Hivyo ndivyo wataweza kuushinda uovu na udhaifu wao, kama asemavyo Mtakatifu
Paulo: nayaweza yote kwake yeye anitiaye nguvu (Rej., Wafilipi 4:13).
Kwa utaratibu huu mpya wa kuondoa adhabu ya utoaji mimba, uwe
fundisho kwa kila mmoja kuiona huruma ya Mungu na kuepuka dhambi. Isidhaniwe
hata mara moja kana kwamba imehalalishwa au imerahisishwa utendaji dhambi huo.
Hapana, dhambi hiyo ni kubwa na ya kuogopwa, na kila mmoja aepuke kabisa
kujiingiza katika mazingira ya utendaji dhambi hiyo.
Na Padre Celestine Nyanda
Idhaa ya Kiswahili, Radio Vatican.
Ni muhimu hasa katika kipindi hiki ambacho kanisa lina sisitiza huruma ya mungu kwa wanadamu.
ReplyDelete