‘Tusipokee Ekaristi Takatifu kwa mazoea’
“Acheni kupokea Ekaristi Takatifu ili muonekane kuwa mmekomunika, ili
hali mnajua kuwa hamustahili, kama haujaenda
kwenye kitubio halafu ukapokea Ekaristi Takatifu, unakuwa umeiba sakramenti”.
Hayo
yameelezwa na Makamu wa Askofu wa Jimbo Katoliki Morogoro Padri Patrick
Kung’alo alipokuwa akitoa sakramenti ya komunyo ya kwanza kwa vijana zaidi ya
30 pamoja na kuweka jiwe la msingi kwenye kanisa la Kigango cha Kristo Mfalme
Parokia ya Bikira Maria wa Mlima Karmeli iliyopo Kihonda Magorofani
linalotarajia kujengwa karibuni.
Padri
Kung’alo amesema kuwa asilimia kubwa ya waamini wamekuwa wakikomunika
kama “fasheni” ili aonekane aidha kwa mavazi aliyovaa na muonekano wake
kwa ujumla huku wakisahau kuwa Ekaristi Takatifu siyo ya kufanyia mchezo.
“Wengi
tunawaona wanakomunika ili waonekane walivyovaa na kupendeza au kwa kuwa
wanaona kuwa kubaki peke yao kwenye viti watafikiriwa vibaya, matokeo yake
wanaenda kukomunika hali ya kuwa wanajua matendo hayo hayastahili.”
amesema.
Ameongeza
kuwa waamini wanapaswa watafakari kabla ya kwenda kukomunika ama sivyo
sakramenti hiyo itawapeleka pabaya, kwa kuwa wanapoungamisha unakuta wanaoungama
hawafiki hata 30 hawafiki lakini kwenye kukomonika wanakuwa wengi.
“Unakuta
tunaungamisha waamini hawafiki 30 lakini kwenye kukomonika unajikuta unamaliza
yale makombe hata matatu sasa unajiuliza hawa watu wamefanya wapi kitubio au
ndio wapo safi hawajatenda dhambi?,” amesema Padri Kung’alo.
Ameongeza
kuwa kama kweli waamini hawatendi dhambi kwa nini unakuta mtu na jirani yake
hawasalimiani kufikia kuapizana vibaya , ndoa zinafuka moshi, umbea, masimango
mawazo mabaya na mengine mengi ambayo ni dhambi lakini unakuta muumini anafukia
hayo yote pasipo kutafakari kwa hayo yote kama anastahili kukomunika au la.
“Tusicheze
na Ekaristi Takatifu, kama utaipokea ukiwa katika hali ambayo inatakiwa kwa
kufanya kitubio ndipo upokee, itakupa uzima wa milele lakini kama na wewe
ni mmoja wa wale wanaopokea kwa fasheni itakupeleka pabaya. Hivyo tubu na
uhakikishe uko safi na usikomunike kwa kuwa unahisi utasemwa kwa nini
haujakomunika, hali ya kuwa unajua moyoni unatakiwa utubu ndipo ukomunike,”
amesema Padri Kung’alo.
Comments
Post a Comment