Dini zina mchango mkubwa katika kudumisha haki, amani na maridhiano
Umuhimu wa kujizatiti katika kukuza na kudumisha misingi ya haki
na amani hata katika maeneo ya vita; kuheshimu na kuthamini maisha ya binadamu
kuwa ni matakatifu na zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu; uhuru wa kidini
na huduma makini kwa wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta hifadhi, usalama na
maisha bora ni kati ya mada tete zilizojadiliwa na Tume ya pamoja kati ya Rabi
mkuu na Tume ya Vatican ya Mahusiano ya kidini na Wayahudi, katika mkutano wao
uluiohitimishwa hivi karibuni mjini Roma.
Tamko la pamoja na wajumbe wa Tume hii limetiwa mkwaju na
Kardinali Peter Turkson, Rais wa Baraza la Kipapa la haki na amani kwa niaba ya
Vatican na kwa niaba ya Wayahudi, Rabi David Rosen. Viongozi hawa wa kidini
wanatambua mchango mkubwa ambao unaweza kutolewa na dini mbali mbali katika
medani za kimataifa kwa kujikita katika haki, amani, maridhiano sanjari na
utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Utakatifu wa maisha ya binadamu,
uhuru wa dhamiri pamoja na kuheshimu na kuthamini tofauti zinazojitokeza baina
ya waamini wa dini mbali mbali kama chachu ya umoja na mshikamano badala ya
kuwa ni chanzo cha kinzani, misigano na hata vita.
Ikumbukwe kwamba, binadamu wote ni sawa kwani wameumbwa kwa sura
na mfano wa Mungu. Katika changamoto mbali mbali zinazojitokeza katika uso wa
dunia, kuna haja kwa dini mbali mbali duniani kuwa ni mfano bora wa kuigwa
katika kukuza na kudumisha haki, amani na maridhiano kati ya watu. Viongozi wa
dini wajizatiti kuwalinda na kuwatetea wanyonge na maskini ndani ya jamii kwani
hili ni kundi ambalo halina sauti hata kidogo.
Waamini wa dini mbali mbali wanatakiwa kuwa ni vyombo na
mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu na kwamba, hakuna kitendo
chochote kinachoweza kuhalalisha vita, nyanyaso na ukatili dhidi ya utu na
heshima ya binadamu. Ni wajibu wa viongozi wa kidini kulaani kwa nguvu zote
wale wote wanaotumia jina la Mungu kuhalalisha vitendo viovu kama vile
mashambulizi ya kigaidi. Hii inatokana na ukweli kwamba, dini zinapaswa kuwa ni
chemchemi ya umoja, upendo na mshikamano kati ya watu wa mataifa na wala si
vinginevyo.
Wajumbe wa tume hii, wameungana kwa kauli moja kulaani vitendo
vya kigaidi vinavyodhalilisha utu na heshima ya binadamu. Hata katika nchi za
Kiislam, tofauti za kidini na kiimani zisiwe ni sababu ya kinzani na mipasuko
ya kijamii, bali wote kwa pamoja wanapaswa kusimama kidete kulinda, kutetea na
kudumisha utakatifu wa maisha ya binadamu, utu na heshima yake. Waamini wa dini
mbali mbali wanahamasishwa kushikamana ili kujenga familia kubwa ya binadamu,
ili kuziwezesha fadhili na kweli kukutana; haki na amani kubusiana, ili kweli
iweze kuchipua katika nchi na haki kuchungulia kutoka mbinguni kama anavyosema
Mzaburi.
Wajumbe wa tume hii ya pamoja wameonesha umuhimu wa kuwafunda
vijana wa kizazi kipya katika tunu msingi za maisha ya kiroho na kiutu, ili
kukuza na kudumisha haki, amani, maridhiano pamoja na kuheshimiana. Maeneo na
nyumba za Ibada zinapaswa kuheshimiwa kwani zinafumbata historia ya maisha ya
waamini wa dini husika. Historia ya Maandiko Matakatifu, Imani na Siasa za nchi
husika hazina budi kuheshimiwa kwani kuna uhusiano mkubwa katika historia na
imani ya watu!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
Comments
Post a Comment