Katibu mkuu mteule wa Umoja wa Mataifa amekula kiapo!
Bwana Antonio Guterres aliyekuwa Kamishina wa Shirika la
Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa, tarehe 12 Desemba 2016 mjini New York,
Marekani amekula kiapo cha utii kama Katibu mkuu wa tisa wa Umoja wa Mataifa na
hivyo kuchukua nafasi ya Bwana Ban Ki-Moon anayemaliza muda wake wa uongozi kwa
vipindi viwili hapo tarehe 31 Desemba 2016. Katibu mkuu mpya wa Umoja wa
Mataifa ameahidi kufuata nyayo za mtangulizi wake Ban Ki-Moon pamoja na
kuendelea kushughulikia changamoto za Umoja wa Mataifa zinazoutaka Umoja wa
Mataifa kufanya mageuzi makubwa kwa kusoma alama za nyakati.
Bwana Antonio Guterres ambaye pia aliwahi kuwa ni Waziri mkuu wa
Hispania ataanza kushika rasmi madaraka kama Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa
hapo tarehe Mosi, Januari 2017. Katika hotuba yake anasema, Umoja wa Mataifa
hauna budi kufanya mageuzi makubwa ili kweli uweze kuwa ni chombo cha amani,
chachu ya kikolezo cha maendeleo endelevu ya binadamu; kwa kusimama kidete
kulinda, kudumisha na kutetea haki msingi za binadamu. Amesema, kutokana na uzoefu
wake kama Kamishina wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa,
taendelea kusimama kidete: kulinda, kutetea na kudumisha utu na heshima ya
binadamu kwa kuwa sauti ya maskini na wanyonge duniani. Anapania pamoja na
mambo mengine kutoa kipaumbele cha pekee kwa wanawake ili waweze kushiriki
katika kupanga na kutekeleza maamuzi mbali mbali katika Jumuiya ya Kimataifa.
Katibu mkuu mteule anasema, atasema kweli daima na wala hatasita
kuwaambia ukweli wakuu wa Jumuiya ya Kimataifa hata ikiwa ni Bwana Donald
Trump, Rais mteule wa Marekani. Anaendelea kukaza kwamba, umefika wakati kwa
Jumuiya ya Kimataifa kutoa suluhu ya kudumu kwa mgogoro wa Siria kwani vita hii
haina mshindi na badala yake inaendelea kupandikiza mbegu ya chuki, uhasama na
vitendo vya kigaidi. Anasema, tangu siku ya kwanza atakapoanza kushika
madaraka, mgogoro huu utauvalia njuga, ili kurejesha tena amani, usalama,
ustawi na maendeleo ya wengi nchini Siria.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
Comments
Post a Comment