Ask. Ruwa’ichi: Kutokujua Neno la Mungu ni utapiamlo wa Kiroho
ASKOFU Mkuu
wa Jimbo Kuu Katoliki Mwanza Mhashimu Yuda Thadei Ruwa’ichi amesema mkristo
yeyote asiyejua neno la Mungu ni sawa na kusakamwa na utapiamlo wa kiroho.
Ametoa
kauli hiyo katika Adhimisho la Misa Takatifu liliyofanyika sambamba na sherehe
ya kuadhimisha miaka kumi tangu kuanzishwa kwa Parokia ya Buzuruga iliyofanyika
parokiani hapo.
Askofu Ruwa’ichi
amesema mkristo akitaka kuwa thabiti ni lazima asome, atafakari na apende neno
la Mungu kila wakati maana baadhi ya waamini hawapendi kusoma neno la Mungu.
Amesema
Yesu Kristo ndiye mchungaji wao mkuu aliyejitoa pale msalabani na kufa kwa
ajili ya dhambi zao ili waokolewe na wawe na uzima tele, sasa basi wakristo
wasichoke kumwomba na kumwambia Mungu shida zao kila wakati.
Pia
katika misa hiyo kulikuwa na sakramenti ya ubatizo ambapo amewahimiza wazazi
kuzingatia umuhimu wake akinukuu maneno na kusema “….wakati akiwa na wanafunzi wake aliwaambia
enendeni ulimwenguni mkawafanye mataifa kuwa wanafunzi mkiwabatiza kwa jina la
Baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu, hivyo msibabaishwe kwa kukosa maarifa
someni neno la Mungu na kulielewa ili mpate ukweli,” Amesema.
Pamoja
na hayo Askofu Ruwa’ichi amewasihi waamini wapende kuikimbilia huruma ya Mungu
wasiogope sakramenti ya “kitubio” kwani Mungu ni Baba wa huruma kwa sababu hata
muumini akiacha kusimamia imani ya kweli na kuacha kufanya yale yanayopaswa
kufanya na kuwa katika upendo wake Mungu hatamtupa akija na kutubu, maana yeye
ni Baba wa huruma na siku zote anawasihi kurudi na kutubu dhambi.
Askofu
Ruwa’ichi pia ametoa sakramenti ya ndoa ambapo amesema kuwa sakramenti hiyo ni
wito wa msingi wa kupokea utume na fursa ya kumtumikia Mungu katika uumbaji na kuwakumbusha
wanandoa kuwa katika ndoa kuna mihimili minne, ambayo ni upendo, umoja, udumifu
na uaminifu na wapende kuyashika hayo na kuyatendea kazi ili ndoa zao zidumu
katika Kristo.
Sambamba
na hayo Askofu Mkuu amewaombea neema na Baraka wanaparokia ya Buzuruga
waendelee kustawi katika nyanja zote katika vigango, parokia na hata jimbo pia
akiwapongeza kwa kukamilisha nyumba ya mapadri kabla ya kuizindua nyumba hiyo
na kuibariki.
Comments
Post a Comment