“Tuunge mkono juhudi za kanisa katoliki” Mbunge Sumbawanga
Mbunge wa viti maalumu mkoa
wa Rukwa Mheshimiwa Aida Joseph Khenani (Chadema) ameitaka serikali, taasisi
binafsi, vyama vya siasa na mtu mmoja mmoja kuunga mkono juhudi za kanisa
katoliki mkoani Rukwa katika kuboresha misingi ya elimu na maendeleo ya
kitaaluma katika sekta ya elimu.
Mheshimiwa Aida ameyasema
hayo katika mahafali ya kuhitimu elimu ya chekechea kwa wanafunzi wa shule ya Familia Takatifu yaliyofanyika hivi karibuni katika
ukumbi wa parokia ya Familia Takatifu jimboni Sumbawanga.
“Nalipongeza sana kanisa
Katoliki mkoa wa Rukwa kwa kujali na kuthamini watu wenye mahitaji mbalimbali
katika jamii kikiwemo kituo cha watoto yatima cha Mt. Martin De Pores Katandala
ambacho ni ukombozi kwa yatima mkoani Rukwa, kusaidia kujenga shule maalumu ya
msingi ya wasioona Malangali ambapo pia kwa sasa ni kituo cha kulelea ndugu
zetu walemavu wa ngozi yaani Albino, kuanzisha huduma za elimu ya chekechea
hata kwa watoto walemavu kupitia kituo cha chekechea cha Familia Takatifu,”
amesema mbunge huyo.
“Kanisa linaona mbali na ndio
maana katika masuala ya msingi kama hili la elimu, tudumishe taaluma ya watoto
wetu na si kuingiza siasa katika vitu vya msingi. Nadhani serikali,taasisi
zingine, makampuni na watu binafsi tuunge mkono juhudi hizi kwa nguvu zote,
‘ ameongeza.
Kwa kutambua mchango mkubwa
wa kanisa katoliki katika maendeleo ya jamii nchini na kwa kujali walemavu, Mheshimiwa
Aida Khenan ametoa mchango wa shilingi milioni mbili kwa ajili ya kuchangia
ujenzi wa miundombinu wa madarasa na vifaa vya kujifunzia kwa watoto wa
chekechea wenye ulemavu ambao wataanza kujiandikisha katika mhula wa masomo wa
mwaka 2017.
Akitoa mchango huo Aida
amesema kuwa serikali inatakiwa kuandaa mpango maalumu wa kutokomeza unyanyapaa
kwa walemavu kwa kuwajengea misingi bora ya elimu kuanzia chekechea hadi vyuo
kama ilivyo kwa wasio na ulemavu
Akimshukuru mgeni rasmi kwa
mchango huo mkuu wa shule hiyo ya ckekechea ya Familia Takatifu Sr. Rose
Kindimba amesema kuwa wameamua kuanzisha huduma ya kupokea watoto wenye ulemavu
mbalimbali shuleni hapo ili kuwajengea misingi kama ilivyo kwa wasio na ulemavu
na kuwaomba wazazi kutowanyanyasa watoto wao kwa kuwanyima elimu
na kuwaficha kwa kuogopa aibu suala ambalo linawanyima fursa za kujiendeleza
kupata ujuzi na kujitegemea kama ilivyo kwa watu wengine.
“Tunao walemavu katika familia
zetu, katika jamii zetu, taifa na hata dunia nzima ambao wanahitaji msaada
wetu. Lakini tukumbuke kuwa ulemavu hauna cha tajiri wala maskini, bosi wala
kibarua, hauna kabila wala rangi siyo wa wazungu tu au waafrika pekee isipokuwa
Mungu amewaweka wenzetu kati yetu ili tutambue ukuu wa uumbaji wake, nasi
tumeona tufanye maboresho kwa kuwawekea mazingira rafiki ya kujifunzia watoto
wenye ulemavu”. Amesema Sr. Rose.
Kituo hicho cha chekechea
kimeanza mwaka 1999 na kimekuwa kikipokea watoto wenye umri wa kuanzia miaka
mitatu kwa ajili ya kuwaandaa kwa masomo ya shule ya msingi.
Comments
Post a Comment