Simanzi yatawala mazishi ya Pardi Andrew Lupondya
Maaskofu
wa majimbo manne , mapadri , watawa na mamia ya waamini wameshiriki misa
ya mazishi ya Padri Andrew Lupondya (33) na watoto watano wa
shirika rafiki wa utoto wa Yesu (VIFRA) na mlezi wao Mama Judith
Kajwahula (63 ) wa jimbo Katoliki Kahama waliofariki katika
ajali ya gari.
Ajali
hiyo ilitokana na gari walilokuwemo kugongana uso kwa uso na roli aina ya fuso
Disemba 24 na marehemu wamezikwa katika eneo la kiwanja cha kanisa
kuu la Mtakatifu Karoli Lwanga parokia ya Kahama mjini.
Misa
ya mazishi imefanyika katika kanisa kuu la jimbo na imeongozwa
na Askofu Fravian Kasala wa jimbo Katoliki Geita, pamoja na Maaskofu
Liberatus Sangu wa Shinyanga, Joseph Mlola wa Kigoma na mwenyeji
Askofu Ludovick Minde wa Kahama.
Akihubiri
katika misa hiyo Askofu wa jimbo Katoliki Shinyanga Liberatus Sangu amesema “Kifo
ni fumbo la Kristo, alishinda mauti kwa kufa na kufufuka kwa imani tumeshirikishwa
toka tulipobatizwa ndani yake, hivyo kutokea kwa msiba huo mkubwa
uliowapata wana jimbo la Kahama uzidi kuwaimarisha katika imani
yetu kwa upendo na mshikamano.”
Askofu
Sangu ameongeza “Huruma ya Mungu haina mpaka, tuikimbilie siku zote katika
mateso, furaha na kudumu kwenye imani yetu kwa kuongozwa na Yesu Kristo
na Roho Mtakatifu na tuwaombee Padri Lupondya na watoto na mlezi wao
waliofariki katika ajali hiyo wakiwa kwenye utume wa sala ndani ya
kanisa Mungu aweze kuwapokea kwake mbinguni.”
Aidha
katika salamu za rambirambi zilizotolewa na Askofu Joseph Mlola wa
Kigoma amesema kamwe wasimruhusu shetani japo msiba huo ni mkubwa
ndani ya kanisa na inauma sana na kuwataka waumini wawe na imani
kwa kuwa kifo siyo mwisho wa maisha bali ndiyo mwanzo wa maisha ya milele
huko mbinguni huku akiwaalika wakristo kuwaombea.
Naye
Askofu Flavian Kasala wa jimbo Katoliki Geita amesema “Kwa kuwa kifo kimewapata
wakiwa katika harakati za sala katika kupokea kuzaliwa kwa Masiha Yesu
Kristo mkombozi wetu pamoja na masikitiko yetu tuwe na matumaini Bwana
hatatuacha, tuwaombee Mungu aweze kuwapokea katika makao ya milele.”
Katika
salamu zake za pole Askofu mkuu wa jimbo kuu Katoliki Dar-es-Salaam,
Mwadhama Polyicarp Kardinali Pengo alizomtumia Askofu wa jimbo Katoliki Kahama
Ludovick Minde na waamini wote, amewataka kupokea msiba huo kwa matumaini ya
kipasaka kwa kuwa wamepata waombezi wao huko mbinguni.
Mkurugenzi
wa mashirika ya kipapa Padri Jovitus Mwijage ametoa pole kwa kifo cha Padri na
kuwapoteza wamisionari hao wadogo na kusema kwa kuwa wamefariki wakiwa katika
utume huo mashirika yataendelea kuwaombea kwa sala wapumzike kwa
amani.
Askofu
wa jimbo Katoliki Kahama Mhashamu Ludovick Minde Katika shukrani zake,
amewashukuru Maaskofu, mapadri na watawa
wote kwa pole na faraja walizompatia yeye na waamini wote jimboni hapa na
kuwa hilo limekuwa kumbukumbu ya Huruma ya Mungu na kwa Krismasi ya mwaka huu
na kuwataka wana shirika kuendelea kukua na kuongeza siku zote Katika imani.
Marehemu
Padri Lupondya aliyekuwa paroko msaidizi katika kanisa kuu la jimbo la Mtakatifu
Karoli Lwanga parokia ya Kahama mjini amezaliwa mwaka 1983 akapewa daraja la ushemasi
17/ 11/ 2014 na kupewa daraja ya Upadri 25/7/2015 jimboni hapa .
Padri
Lupondya alifariki dunia jumamosi Disemba 24 alasiri kwa ajali ya gari
yake aliyokuwa akiendesha aina ya Toyota Hilux akiwa amewabeba watoto wa
shirika rafiki wa Yesu VIFRA na mlezi wao walipokuwa wakitoka parokia ya
Ekaristi Takatifu Kabuhima kwenda Karoli Lwanga Kahama mjini walipogongana uso
kwa uso na roli aina ya fuso na kusababisha vifo vya watoto watano na mlezi wao
Mama Kajwahula.
Watoto
waliofariki wa VIFRA ni Carolina Zacharia (11) Emiliana Boniphace (12) Anisia
Marco (14) Eva John (9) Paschal Bwile ( 16) na mlezi wao wa jimbo la Kahama
Mama Judith Kajwahula (63), kwa pamoja na Padri Lupondya wamezikwa
jumatano Disemba 28 katika eneo la kiwanja cha kanisa kuu la Mtakatifu Karoli
Lwanga parokia yao ya Kahama mjini.
Comments
Post a Comment