ZINGATIENI MAADILI YA UPADRI-ASKOFU RUWA’ICHI
ASKOFU
mkuu wa Jimbo Kuu katoliki Mwanza Mhashamu Jude Thadeus Ruwa’ichi amewakumbusha
mapadri kuepuka kuweka ubunifu usiokuwa
na tija katika uinjilishaji bali ni lazima wafuate maadili ya upadri na misingi
ya kanisa bila kuchoka.
Amewataka
wajue kuwa huo ni utume na kwamba wametengwa kwa ajili ya kazi hiyo na sio kazi
nyingine.
Ameyaweka
hayo bayana katika misa takatifu ya kuazimisha uzinduzi wa Jubilei ya miaka 100
ya upadri Tanzania Bara katika Jimbo kuu katoliki Mwanza iliyofanyika katika
parokia ya Sumve jijini Mwanza na kuhudhuriwa na mapadri kutoka parokia zote.
Pia
Askofu Ruwa’ichi amewahimiza mapadri
kuwa kazi ya upadri ni wito na Mungu amewatumia wao kueneza injili ulimwenguni
kama alivyowatuma mitume kumi na wawili kutoka katika watu dhaifu ambao ni
binadamu ili kwenda ulimwenguni kueneza injili na wawe chombo cha uamsho.
Askofu
Ruwa’ichi pia amewasihi mapadri kuzidi kumwomba Mungu awape neema na ubunifu
bora ili wafanye kazi yao kwa amani ya Mungu, wajitahidi kutafakari juu ya
mapana na marefu katika ufanyaji kazi hiyo na wapate kuwa makuhani wa Mungu ili
wazishinde changamoto za nguvu za shetani maana “mavuno ni mengi lakini watenda
kazi ni wachache”.
Pamoja
na hayo Askofu Mkuu Ruwa’ichi amewapongeza mapadri wa kwanza kuinjilisha
Tanzania Bara kuwa walitenda kazi bila hofu na walikuwa mstari wa mbele kueneza
injili wakati wowote bila kuchoka kupitia utume huo huku akihimiza waamini wote
wasafiri pamoja kama familia ya Mungu ili
mwaka wa mapadri ukubalike.
Amewashukuru
wana Sumve na mapadri kwa utayari wa tukio hilo huku akiwasisitizia kusafiri
pamoja kwa mshikamano wa pekee ndani ya jimbo kuu katoliki Mwanza, katika
tafakari, sala na kulea miito ya upadri kwa Taifa lote la Mungu.
Na
Maria Emmanuel, Mwanza
Comments
Post a Comment