Ujumbe wa Papa Francisko kwa washiriki wa mkutano wa COP22
Uharibifu wa mazingira ni matokeo
ya mmong’onyoko wa tunu msingi za maisha ya binadamu, kimaadili na kijamii,
changamoto kwa kila mtu kuhakikisha kwamba, anatekeza wajibu wa kulinda
mazingira kadiri ya uwezo na nafasi yake katika jamii; hii ni dhamana inayowawajibisha
wote. Mkutano wa kimataifa kuhusu mazingira nchini Morocco, COP22 unafanyika
baada ya kuanza utekelezaji wa Itifaki ya utunzaji bora wa mazingira
iliyopitishwa mjini Paris, Ufaransa kunako mwaka 2015. Athari za mabadiliko ya
tabianchi zinahitaji uwajibikaji wa pamoja, ili kushiriki kikamilifu katika
utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote.
Huu ni wajibu wa kuhakikisha
kwamba, Jumuiya ya Kimataifa inatumia kikamilifu maendeleo ya sayansi na
teknolojia ili kudhibiti kikamilifu athari za mabadiliko ya tabianchi sanjari
na kutumia nguvu kwa ajili ya mchakato mbadala wa maendeleo endelevu na bora
zaidi, unaojikita katika tunu za kiutu na kijamii. Lengo ni kuhakikisha kwamba,
uchumi wa dunia unakuwa ni kwa ajili ya huduma kwa binadamu, ili hatimaye, kujenga
msingi wa haki na amani, ili kulinda na kutunza mazingira, nyumba ya wote.
Hii ni sehemu ya ujumbe wa Baba
Mtakatifu Francisko kwa Bwana Salaheddine Mezouar, Waziri wa mambo ya nchi za
nje na ushirikiano wa kimataifa nchini Morocco, kwa niaba ya wajumbe
wanaoshiriki katika mkutano wa kimataifa wa tabianchi mjini Marrakech kuanzia
tarehe 7- 18 Novemba 2016. Baba Mtakatifu katika ujumbe huu, anaendelea kusema,
Itifaki ya Paris imeonesha dira na njia ambayo inapaswa kutumiwa na Jumuiya ya
Kimataifa kwa ajili ya kulinda na kutunza mazingira. Itakumbukwa kwamba,
waathirika wakubwa wa mabadiliko ya tabianchi ni maskini na kizazi kijacho,
jambo linalohitaji uwajibikaji unaozingatia kanuni maadili bila kuchelewa wala
kuwa na mashinikizo ya kisiasa na kiuchumi, tayari kuvuka mipaka ya mafao
binafsi.
Ni matumaini ya Baba Mtakatifu
Francisko kwamba, wajumbe katika mkutano huu watashikamana ili kuweza kupata
matunda yanayokusudiwa kama ilivyokuwa kwa Itifaki ya Paris, COP21, tayari
kuanza utekelezaji wa itifaki hii, kipindi tete sana kinachohitaji sheria, sera
na mikakati ya kitaasisi itakayoiwezesha Jumuiya ya Kimataifa kutekeleza
itifaki si tu kiufundi kwa kuungwa mkono pia na sera za kisiasa kwa kutambua
kwamba, wote wanaunda familia moja ya binadamu isiyokuwa na mipaka ya kisiasa
na kijamii inayoweza kuwagawa au kwa kujikita katika utandawazi usiojali wala
kuguswa na mahangaiko ya wengine.
Lengo la utekelezaji wa itifaki hii
ni kusaidia kukoleza mchakato wa maendeleo kitaifa na kimataifa kwa kujikita
katika utunzaji bora wa mazingira unaofumbata mshikamano na maskini
wanaoendelea kujizatiti kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi pamoja
na umaskini. Hili ni jukumu pevu ambalo haliwezi kushughulikiwa kikamilifu
mintarafu mwelekeo wa kiufundi na kiuchumi peke yake. Hapa kuna haja ya
kujikita katika kanuni maadili na kijamii, ili kuleta maendeleo endelevu. Elimu
makini isaidie kuleta mabadiliko katika mtindo wa maisha katika uzalishaji na
ulaji wa bidhaa na huduma, kwa kuzingatia kanuni za utunzaji bora wa mazingira,
nyumba ya wote. Hapa wadau wote wanahamasishwa kushiriki kikamilifu katika
utunzaji bora wa mazingira kila mtu kadiri ya uwezo na nafasi yake.
Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko
anasema ni matumaini yake kwamba, wajumbe wa mkutano wa mazingira kimataifa
huko Marrakech wataongozwa na dhamiri ya uwajibikaji kwa ajili ya utunzaji wa
mazingira nyumba ya wote na upendo kwa jirani. Ni changamoto ya kuondokana na
mtindo wa maisha yasiyojikita katika elimu na maendeleo endelevu, changamoto
kubwa kwa Jumuiya ya Kimataifa katika ulimwengu mamboleo. Ni wakati wa
kutekeleza kwa dhati kabisa Itifaki ya Paris kwa ajili ya mafao na ustawi wa
wengi.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio
Vatican.
Comments
Post a Comment