HURUMA YA MUNGU YATAKIWA KUWA DHAMANA YA MAISHA YA WAAMINI
Baba Mtakatifu Fransisko, amekutana na kuzungumza na waandaaji, waratibu na watu walioshiriki kwa karibu zaidi katika mchakato wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, uliofungwa hivi karibuni na hivyo kutoa nafasi kwa waamini sasa kuendelea kumwilisha matunda ya huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao. Mwaka wa huruma ya Mungu umekuwa ni kipindi cha neema na baraka kwa maisha na utume wa Kanisa na kwamba, watu wengi wameonja na kuguswa na huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao.
Baba Mtakatifu anasema, kazi yake kubwa ilikuwa ni kuitisha maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu na kumwachia Mwenyezi Mungu mwenyewe atende kazi yake. Dhamana hii imewawezesha waamini wengi kuweza kuadhimisha Mwaka wa huruma ya Mungu kwa imani na furaha! Malango ya huruma ya Mungu sehemu mbali mbali za dunia, yameondoa vikwazo kwa waamini kiasi kwamba wote waliojibidisha kupitia Lango hili wameonja upendo wa Mungu. Hili limekuwa ni tukio la aina yake, sasa linapaswa kumwilisha katika uhalisia wa maisha ya kila siku, ili kweli huruma ya Mungu iweze kuwa dhamana na mtindo wa maisha endelevu miongoni mwa waamini!
Baba Mtakatifu anawashukuru waandaaji, waratibu na wote walioshiriki kwa namna moja au nyingine kufanikisha maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma. Vyombo vya ulinzi na usalama nchini Italia vimekuwa mstari wa mbele kuhakikisha kwamba, mwaka wa huruma ya Mungu unaadhimishwa katika hali ya amani na utulivu. Kumekuwepo na ushirikiano wa hali ya juu kati ya Vatican na wawakilishi wa Serikali ya Italia wakati wote wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, chini ya uongozi wa Professa Claudio de Vincent, Katibu msaidizi wa tume hiyo.
Baba Mtakatifu amevishukuru na kuvipongeza vyombo vya ulinzi na usalama vya Vatican; huduma ya afya ya mkoa wa Lazio; timu ya ufundi ya mapokezi iliyokuwa chini ya Kamanda Paola Basilone pamoja na Baraza la Kipapa la Kuhamasisha Uinjilishaji mpya, linaloongozwa na Askofu mkuu Salvatore Rino Fisichella, ambalo lilipewa dhamana ya kuratibu maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Baba Mtakatifu anasema, ikiwa kama mtu anataka kupata huruma, lazima mwenyewe awe na huruma. Haya ni maneno ya faraja ambayo Baba Mtakatifu amewatakia wadau mbali mbali waliowezesha kufanikisha mchakato wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma. Huruma hii iwe ni faraja tosha kabisa katika maisha yao!
Kwa msaada wa Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
Comments
Post a Comment