Ask. Minde: Tujitathmini na kuidhihirisha huruma
ASKOFU wa Jimbo
Katoliki Kahama, Mhashamu Ludovick Minde amesema kuwa kila
mkristo anapaswa kufanya tathmini ya kina baada ya kuhitimishwa kwa
Yubilei ya Huruma ya Mungu, huku akitoa angalizo Huruma ya Mungu ipo kila
wakati.
Askofu Minde
ameeleza hayo katika maadhimisho ya kufunga na kufungua mwaka Endelevu wa
Huruma ya Mungu, Jimbo Katoliki Kahama, yaliyofanyika Novemba 19, 2016 siku
moja kabla ya kufunga mwaka wa huruma ya Mungu katika Kanisa la Ulimwengu.
Amesema kuwa kitendo cha kufungua mlango wa Kanisa
Kuu kama ishara ya kufungua rasmi mwaka wa huruma ya Mungu ni tendo la nje.
Tendo hili linawaalika waamini wafungue mioyo yao na maisha yao ili kujitakasa
na kujisafisha.
“Hiki ni
kipindi cha toba, tutoe nafasi, tujisafishe, tujitakase,tuwe donge jipya kwa
Mungu aweze kumwaga huruma yake kwetu” ameeleza.
Aidha
Askofu Minde ametoa rai kwa waamini kuwa tayari kutoa huruma kwa wengine.
“Tunapopokea
huruma ya Mungu hapohapo tuwe vyombo vya kutoa huruma kwa wengine. Kama
hatufanyi matendo ya huruma kwa wengine tusitegemee kamwe kupata huruma ya
Mungu”.
Ameongeza kuwa huruma ya Mungu ni njia mbili
zinazotegemezana na kufanikishana, yaani Mungu anatoa Huruma yake kwa binadamu ambao nao hawana budi kutoa huruma kwa
wanadamu wenzao hasa katika yale
maeneo
magumu na yaliyosahaulika.
“Nina amini kwamba wakristo wote wa Kahama
ambao ni wahitaji wakubwa wa huruma ya Mungu; watakuwa na neema na furaha ya
kujitambua na kuzaa matunda mengi na mazuri ya huruma ya Mungu”, amesema.
Comments
Post a Comment