Waamini vuguvugu wanalitia kichefuchefu Kanisa!
Baba Mtakatifu Francisko katika
mahubiri yake wakati wa Misa Takatifu kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha
kilichoko mjini Vatican, siku ya jumanne, tarehe 15 Novemba 2016, amewaalika
waamini kuchukua tahadhari kuepuka kuwa watu vuguvugu. Kristo anawaonya,
anawarekebisha na anawaamsha kila mara ili wasije kuwa vuguvugu. Hivyo ni
muhimu kwa waamini kuepuka hatari hiyo na kufanya jitihada za kubaki motomoto
katika imani.
Wapo baadhi wanaojiona kuwa na
amani na utulivu kwa kujidanganya kwamba hawana hitaji lolote, wala hawamtendei
yeyote ubaya, kiuhalisia ni utulivu danganyifu, sababu katika kujidanganya
huko, Mungu hayupo mahali hapo, Mungu hayupo kati yao. Utulivu wa namna hii
unawafanya waamini hawa kujiona matajiri, lakini wanakosa utajiri wa kweli ulio
ndani ya Kristo, utajiri unaoendana na maisha ya msalaba, na mawimbi ya hapa na
pale katika hija ya imani. Huu ndio utajiri wa kweli ndani ya Kristo.
Kristo anatambua hatari ya kuanguka
katika uvuguvugu wa imani, kwa sababu hiyo anawakumbusha waamini kila wakati,
anawaamsha kiimani, amesimama mlangoni akibisha hodi ili kuwaamsha, ili
kujialika katika maisha yao, ili kuwafariji, ili kuwarekebisha.
Baba Mtakatifu Francisko anasema ni
jukumu la kila mwamini mbatizwa kujifunza kuchanganua sauti ya Kristo
anapogonga hodi, kutambua anagonga hodi ili kujialika maishani mwao, ili
kuwarekebisha, ili kuwafariji, au kuwashusha kutoka katika mahangaiko yao
fulani au kutoka katika udanganyifu wa uvuguvugu.
Na Padre Celestine Nyanda
Idhaa ya Kiswahili, Radio Vatican.
Comments
Post a Comment