Majaliwa: Hatutawavumilia waajiri wasiotoa mikataba
WAZIRI MKUU
Kassim Majaliwa amesema kuwa Serikali haitawavumilia waajiri ambao hawatoi
mikataba ya ajira kwa wafanyakazi wao na amewaonya waache tabia hiyo mara moja.
Ametoa agizo hilo wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Sita wa Shirikisho la
Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) katika ukumbi wa Mwalimu Julius K.
Nyerere ulioko Chuo cha Mipango, nje kidogo ya mji wa Dodoma.
“Nitoe wito kwa waajiri wote ambao wamekuwa na tabia ya kutokutoa mikataba
ya ajira kwa wafanyakazi wao, waache tabia hiyo mara moja, kwani Serikali
haitamvumilia mwajiri wa namna hii,” ameonya.
Akijibu hoja ya waajiri kutokutoa mikataba ya ajira kwa wafanyakazi
ambayo iliibuliwa kwenye risala yao, Waziri Mkuu amesema kifungu cha 14 cha
Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini Na. 6 ya mwaka 2004 kinaelekeza aina
mbalimbali za mikataba inayotakiwa kutumika kuajiri wafanyakazi.
“Kisheria mwajiri anao wajibu wa kuhakikisha kila mtumishi wake ana mkataba
wa kazi kwa maandishi. Pia ninawaagiza maafisa wa kazi wanaohusika na
kaguzi za kazi kote nchini, wahakikishe kila mwajiri anafikiwa wakati wa
ukaguzi na hatua stahiki zinachukuliwa kwa wote wasiotekeleza matakwa ya Sheria
ya Ajira na Mahusiano Kazini,” amesisitiza.
Akijibu hoja kuhusu wafanyakazi kuwekwa ndani kiholela, kunyanyaswa,
kushushwa vyeo na kusimamishwa kazi na wanasiasa, Waziri Mkuu amesema Serikali chini
ya uongozi wa Dkt. John Pombe Magufuli itaendelea kuzingatia utawala wa sheria
na kanuni za utawala bora ili kuhakikisha kuwa haki za wafanyakazi zinalindwa
ipasavyo.
“Kimsingi
watumishi wanasimamiwa na mamlaka za kinidhamu na sheria mbalimbali ambazo
hazina budi kuangaliwa kwa pamoja kabla ya kuchukua hatua. Ninawaagiza viongozi
wenzagu wa kisiasa na walioko katika wizara na taasisi zote za Serikali,
mikoani, wilayani, kwenye idara za Serikali na Halmashauri wazingatie utawala
wa sheria wakati wa kushughulikia masuala mbalimbali yanayohusu wajibu na haki
za wafanyakazi,” amesema huku akishangiliwa.
Comments
Post a Comment