Kanuni bora za mawasiliano kadiri ya Papa Francisko!
Alessandro Gisotti, mwandishi wa habari wa Radio Vatican
amechapisha kitabu kinachopembua kanuni kumi za mawasiliano bora mintarafu
mwelekeo wa Baba Mtakatifu Francisko, kitabu ambacho kitaanza kuuzwa
kwenye maduka ya vitabu kuanzia sasa. Mawasiliano ya jamii yanapaswa kusaidia
mchakato wa ujenzi wa madaraja ya watu kukutana na kusaidiana na wala si kuta
zinazowatenganisha watu! Wala kinzani na migawanyiko inayodhalilisha utu,
heshima na mafungamano ya kijamii.
Kardinali Luis Antonio Tagle, Rais wa Shirikisho la Mashirika ya
Misaada ya Kanisa Katoliki Kimataifa ndiye aliyeandika utangulizi wa kitabu
hiki. Fedha yote itakayopatikana itatumika kwa ajili ya kugharimia miradi ya
maendeleo endelevu inayotekelezwa na Wasalesiani wa Don Bosco. Baba Mtakatifu
amekuwa ni kielelezo cha ushuhuda na chombo cha kukutana na watu katika maisha
na utume wake, hata wale ambao kutokana na magonjwa na hali zao za maisha
wanajikuta wametengwa na jamii, kama ilivyokuwa ugonjwa wa Ukoma kwenye Agano
la Kale.
Kwa kukutana na kuwakumbatia watu waliotengwa na kusukumizwa
pembezoni mwa Jamii, Baba Mtakatifu anawarejeshea utu na heshima yao kama
binadamu walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu na kukombolewa kwa Damu Azizi ya
Kristo Yesu pale Msalabani. Baba Mtakatifu anafundisha kwa njia ya mfano wa
ushuhuda wa maisha yake jinsi ya kuwasiliana na kuhusiana na jirani. Kardinali
Tagle anasema, kuna haja ya kuwa na mbinu mkakati wa mawasiliano unaofumbata
mawasiliano ya kweli kati ya binadamu na Muumba wake na kati ya mtu na jirani
zake.
Mitandao ya kijamii haina budi kusaidia kuimarisha mchakato wa
mawasiliano, umoja, upendo na mshikamano kati ya Mungu na binadamu na kati ya
watu ndani ya jamii. Ni mwaliko wa kuwasiliana na wote pasi ya kujenga kuta za
utengano kama alivyofanya wakati alipokutana na na Waziri mkuu wa Israeli Bwana
Shimon Perez na Abu Mazen kwenye bustani za Vatican au pale Baba Mtakatifu
anapowatwangia simu wafungwa magerezani au watu wanaoogelea katika upweke na
hali ya kukata tamaa katika maisha! Mawasiliano ya Baba Mtakatifu katika
mwelekeo huu yanapania kujenga madaraja ya kuwakutanisha watu kwa kujikita
katika matumaini.
Kardinali Tagle anakaza kusema, kiini cha mawasiliani ya
binadamu ni utu, heshima na mafao ya wengi; mambo ambayo yanapewa kipaumbele cha
pekee katika maisha na utume wa Baba Mtakatifu Francisko. Ni mawasiliano
yanayolenga kugusa, kuponya na kumrejeshea mtu hadhi yake kama binadamu licha
ya mapungufu na udhaifu wake wa kibinadamu. Ni mawasiliano yanayopania kujenga
na kudumisha misingi ya haki, amani, upendo na upatanisho katika ukweli na
uwazi pasi na unafiki! Baba Mtakatifu ni mtu ambaye hapendi unafiki na maisha
ya ndumila kuwili!
Baba Mtakatifu Francisko si mtaalam sana wa lugha, lakini ni
kiongozi ambaye amebarikiwa kuwasiliana na watu hata katika matendo, ili
kuwaonjesha ukaribu, furaha, huruma na upendo unaobubujika kutoka kwa Kristo na
Kanisa lake. Kimsingi, mawasiliano bora yanawawezesha wadau kuwa kama Wasamaria
wema wanaothubutu kujitaabisha kwa ajili ya kuwahudumia ndugu zao kwa hali na
mali bila ya kujibakiza, changamoto endelevu kama sehemu ya kumwilisha matunda,
baraka na neema za maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya
Mungu.
Wadau wa tasnia ya habari wanapotekeleza dhamana na wajibu wao
wanapaswa kwanza kabisa kutanguliza utu, heshima, ustawi na mafao ya wengi. Hii
ndiyo nguvu ya mawasiliano ya jamii inayoweza kutekelezwa kikamilifu na vyombo
vya mawasiliano ya jamii anasema Baba Mtakatifu Francisko! Kabla ya jambo
lolote lile, kipaumbele cha kwanza ni utu na heshima ya binadamu! Haya ni
mawasiliano yanayopaswa pia kumwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu kila
siku na wala si kwa ajili ya wadau wa tasnia ya habari peke yao!
Injili ya familia inaboreshwa kwa maneno ya kawaida kabisa:
Tafadhali, Samahani na Asante asali wa moyo wangu! Haya ni maneno ya kawaida
lakini yanajenga ukaribu kati ya watu, badala ya kuoneshana na kupimana nguvu
na ubabe, utadhani kwamba, familia imegeuka kuwa ni uwanja wa masumbwi! Kanuni
za mawasiliano bora ni kitabu kinacholeta chachu ya kukuza na kudumisha
mawasiliano bora zaidi ili kusimama kidete kulinda utu na heshima ya binadamu
kwa kujenga madaraja yanayowakutanisha watu, tayari kuendeleza mchakato wa
maisha!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
Comments
Post a Comment