Utabiri Wa Baba Mtakatifu Paulo Vi Watimia
Imekuwa ni kawaida sana
kwa Mababa Watakatifu wakaliapo kiti cha Petro kutoa mafundisho kwa njia ya
nyaraka, ziitwazo‘insiklika’ na
kusambazwa kwa Maaskofu wote na makanisa yote dunia nzima pamoja na vyombo vya
habari. Insiklika ni waraka unaosheheni mafundisho ya msingi ya kanisa.
Mafundisho haya ni ya imani yanayogusa matatizo ya kijamii na kutoa msimamo wa
kanisa mintarafu jambo fulani katika wakati fulani. Mfano wa insiklika hizi ni
kama insiklika ya‘Evangelium Vitae’(Injili
ya Uhai);‘Humanae Vitae’ (Juu ya Uhai), ‘Dignitatis
Humanae’ Juu ya Utu wa Mwanadamu, ‘Populorum
Progressio’ Juu ya Maendeleo ya Watu, ‘Evangelii
Gaudium’ Juu ya Injili ya Furaha na nyingine nyingi.
Mwaka 1968, Baba
mtakatifu Paulo VI aliandika insiklika iitwayo ‘Humanae Vitae' ikijibu kiu
ya watu ndani ya kanisa, mintarafu matumizi ya vidhibiti mimba, kama ni vyema
ama si vyema kutumia vidhibiti mimba, na kuainisha njia bora za kupanga uzazi
kwa njia ya maumbile kama Mungu alivyoratibisha.Hata hivyo ikumbukwe kuwa mnamo
mwaka 1930, Umoja wa Makanisa ya Kianglikana katika mkutano wao wa Lamberth,
ingawa walikubali kuwa, njia bora ya kupanga uzazi ni ile itumiayo mwenendo wa
maumbile, lakini waliruhusu matumizi ya vidhibiti mimba kwa wanandoa wenye
matatizo ya pekee. Ruhusa hii ilifungua milango kwa matumizi ya vidhibiti mimba
hata pasipo matatizo yoyote, na hatimaye ukawa ndio mtindo wa kupanga uzazi kwa
watu wa ndoa.
Kutokana na ruhusa hiyo ya Waanglikana na
kutokana na kuongezeka kwa vitisho dhidi ya taasisi ya ndoa, Baba Mtakatifu
Pius XI, mnamo Decemba 31, 1930 alitoa tamko la Kanisa Katoliki kuhusu matumizi
ya vidhibiti mimba.
"Kwa sababu
yoyote, hata kama ni kubwa kiasi gani, haitaruhusiwa matumizi ya njia ambazo
kwa asili yake ni ovu dhidi ya maumbile na kuzifanya zikubalike kimaadili kama
vile zingekuwa njema. Kwa vile tendo la ndoa limeelekezwa kimaumbile katika
uzao wa watoto, wale wanaoliharibu kwa makusudi na kuliondolea uwezo wake
wanatenda dhambi dhidi ya maumbile na wanajiletea aibu na uovu wa ndani. (Casti
Cannubii, Na 54)"
Katika kujenga hoja kwa
nini matumizi ya vidhibiti mimba, vitisho dhidi ya taasisi ya ndoa, na vitisho
dhidi ya ongezeko la idadi ya watu havikubaliki kiimani na kijamii Baba Mt
Paulo VI alisema:
Kwanza;
matumizi ya vidhibiti mimba yatafungua milango kwa watu kukosa uaminifu kwa
kiapo cha ndoa na pia wale walio nje ya
ndoa kukosa uaminifu katika maisha yao. Wakati mwingine wanandoa wanatumia
vidhibiti mimba bila kuwa na sababu. Mfano waweza kuta katika ndoa mume
amesafiri kikazi hata miezi miwili lakini huku nyuma mke anatumia vidhibiti
mimba hii ni kutokana na dhana kwamba haogopi uasherati wala magonjwa ya zinaa
bali anaogopa mimba. Tunayoyashuhudia sasa hivi kama kuongezeka kwa matumizi ya
vidhibiti mimba kama vitanzi, sindano na kusheheni kwa kondomu za aina
mbalimbali kwenye maduka ya dawa kunadhihirisha kuwa kukosa uaminifu katika
ndoa na wale wasio kwenye ndoa umekuwa mkubwa. Pia mambo kama kutoka nje ya
ndoa yaani uasherati kwa lugha ya kisasa 'mchepuko' nao umeongezeka sana
na kupelekea kuvunjika kwa ndoa hali ambayo huletwa na ubaridi wa vidhibiti
mimba na chuki kwa tendo la ndoa kwa mume.
Matumizi ya vidhibiti mimba humjengea mtumiaji uhuru na
mtumiaji kujisemea mwenyewe kuwa, mume au mke wangu hatajua, sitaweza kupata au
kumpa mimba. Nitaendelea na masomo yangu kama kawaida. Nitaweza kubadilisha wanaume au wanawake nipendavyo.
Pili;
matumizi ya vidhibiti mimba yatasababisha mmomonyoko wa maadili kutokana na
udhaifu wa kibinadamu, na hasa miongoni mwa vijana ambao wanakuwa katika hatari
kubwa ya vishawishi vya ngono katika umri wao. Vijana wamekuwa wahanga wakubwa
katika mmomonyoko wa maadili, huko mashuleni vijana na wanafunzi wetu pamekuwa
sio mahali salama tena kwani wamekuwa wakifundishwa elimu ya ngono katika umri
wao mdogo ambapo matumizi ya vidhibiti mimba yanahimizwa, elimu ya ushoga, kama
katika kipindi cha mwezi mmoja uliopita katika taarifa iliyotolewa na Waziri wa
Katiba na Sheria Mheshimiwa Dk Harrison Mwakyembe namna baadhi ya mashirika ya
kigeni kwa kushirikiana na watu matajiri hapa nchini wanavyofanya vikao vyao
usiku katika utekelezaji wa kuwafundisha wanafunzi mambo ya ushoga huko
mashuleni. Jambo hili linatuogofya wazazi na walezi kwamba watoto wetu hawako
salama tena.
Uzinzi na biashara ya
ngono inaongezeka kila kukicha. Tunashuhudia katika jamii na sehemu tunamoishi
jinsi vijana na watoto wetu walivyoharibika kwa kujikita katika mambo ya
umalaya na uzinzi. Kumomonyoka huku kwa maadili kwa vijana kumesababisha kijana
kukosa tunu ya usafi wa moyo pamoja na tunu nyingine kama kujikatalia,
kujishinda na kujiheshimu.
Tatu;
watu wanapozama katika mazoea ya vitendo vya kuepa mimba kwa matumizi ya
vidhibiti mimba, hatimaye wanapoteza heshima kwa mwanamke, na hivyo kushindwa
kumjali katika mahitaji yake ya kimwili na kisaikolojia, wanaweza kufikia
mahali pa kumwona mwanamke kama chombo cha starehe, yaani cha kujifurahisha
kibinafsi na tena si mwanamke anayepaswa
kuheshimika na mwenzi wa maisha. Mwanamke anafanywa kuwa chombo cha biashara za
ngono, mfano tovuti mbalimbali zinatangaza biashara hii ya ngono, pamoja na
mashirika mbalimbali ya biashara ya ngono yameanzishwa mfano nchini Ujerumani
kwa sababu kuna anayeuza na anayenunua. Kwa sababu ya matumizi ya vidhibiti
mimba inamfanya mwanamke wakati wote kuwa tayari katika kufanya tendo la ndoa,
kwa kuwa hana hofu ya kupata mimba kitu kinachopelekea thamani yake kupotea.
Nne;
ifahamike kuwa silaha hatari zinawekwa mikononi mwa watawala ambao hawajali
mahitaji ya kimaadili. Kwa hiyo viongozi wa serikali watanyang’anya mamlaka
wanandoa katika kupanga uzazi, badala yake serikali itawalazimisha watu kupanga
uzazi kwa kutumia njia zile zisizokubalika kimaadili yaani kutumia vidonge vya
majira, sindano za depo-provera, vitanzi, vipandikizi na kondomu.
Utabiri huu wa Baba
Mtakatifu Paulo VI aliutoa katika insiklika, JUU YA UHAI au 'Humanae Vitae'
iliyotolewa tarehe 25 Julai 1968 hatimaye umekamilika. Hii inatokana na mkutano
wa kimataifa juu ya uzazi wa mpango
uliofanyika kwa wiki moja hapa Tanzania kuanzia Oktoba 31 na kumalizika Novemba
4, 2016. Mkutano huu uliandaliwa na shirika lisilo la kiserikali la FP 2020 kwa
kushirikiana na GFF, ni ufuatiliaji wa utekelezwaji wa maazimio ya mkutano
uliofanyika katika jiji la London mwaka 2012 uliofadhiliwa na Bill and Melinda
Gates Foundation; likiwa na lengo ifikapo mwaka 2020 wanawake milioni 120
kutoka nchi za Afrika na Kusini Mashariki Asia ambao hawajapata huduma ya uzazi
wa mpango wawe wamepata.
Katika ufunguzi wa
mkutano huo wa FP2020 gazeti moja la hapa nchini la kila siku la tarehe 2
Novemba 2016 limemnukuu Waziri wa Afya alipokuwa anaufungua akisema, “Kiwango
kikubwa cha mimba kati ya wasichana walio chini ya miaka 18 limekuwa tatizo
kubwa ambalo tunahitaji kulishughulikia”. Kwa hiyo matumizi ya vidhibiti mimba kwa Tanzania ili
kufikia malengo ya kidunia ya uzazi wa mpango ifikapo 2021 sasa yataelekezwa kwa vijana.
Baba Mtakatifu Paulo VI
aliposema kuwa serikali itaingilia uhuru wa wanandoa katika kupanga uzazi; hili
tunaliona sasa namna serikali inavyotumia nguvu nyingi katika kufanikisha hili,
na tayari unabii umetimia. Serikali kwa kupitia Wizara ya afya imekuwa mstari
wa mbele katika kuhamasisha watanzania watumie vidhibiti mimba yaani kondomu,
vitanzi, vipandikizi na sindano za depo-provera chini ya mwavuli wa afya ya
mama na mtoto na vijana. Hili limethibitika pale FP 2020 na Global Financial
Facility walipoahidi kutoa fedha kiasi cha dola za kimarekani milioni 40 ili
kuboresha vituo vya afya 100 vitakavyotoa huduma ya uzazi wa mpango.
Suluhisho la mimba za
utotoni sio kuongeza matumizi ya vidhibiti mimba; la hasha! Matumizi ya
vidhibiti mimba yanachangia ongezeko la vijana kujihusisha na umalaya na uhuni
jambo linalochangia kuongezeka kwa mimba za utotoni. Suluhisho la kweli ni
kuacha kuwafundisha watoto wetu na wanafunzi wetu elimu ya ngono.
Ndugu zangu Watanzania
wote bila kujali dini, itikadi zetu tuje pamoja kuangalia ni namna gani
tutasimama kidete juu ya matumizi ya vidhibiti mimba kwa watoto na vijana wetu.
Matumizi ya vidhibiti
mimba kwa Tanzania ili kufikia malengo ya kidunia ya uzazi wa mpango ifikapo
2020 sasa yataelekezwa kwa vijana.
Ni lazima tufanye
jitihada ili kuwaepusha watoto wetu na madhara yatokanayo na hivi vidhibiti
mimba.
Jambo la kuihimiza
serikali yetu kupitia Wizara ya Elimu ni kuwa hapa tulipofika tunahitaji somo
la maadili litakalofundishwa kuanzia shule ya msingi mpaka vyuo vikuu, ili
tuwafundishe watoto wetu maadili mema na siyo umalaya kupitia vidhibiti mimba.
Kauli kuwa tuelekeze
matumizi ya vidhibiti mimba kwa vijana ni kuhalalisha uzinzi na umalaya kwa
watoto na wanafunzi wetu. Ni kusema fanyeni tuu uzinzi na umalaya lakini
angalieni msipate mimba.
Erasto
Kimonge
Mkufunzi,
Pro-life
Tanzania.
Comments
Post a Comment